CCM WAGOMBEA 38 CHUJIO KUPITA KESHO
Dodoma. Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM itakutana kesho mjini Dodoma kuanza shughuli yake ya kupitia taarifa za wagombea 38 wanaoomba kuwania urais na kisha kuwasilisha ushauri wake kwenye kikao cha Kamati Kuu inayokutana keshokutwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa kamati
hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete
wakati mwingine hukasimisha shughuli zake kwa kamati ndogo inayoketi
chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Mangula amekaririwa mara kadhaa akisema chama
hicho kitatumia vigezo 13 vilivyowekwa na chama kuwachuja wagombea hao,
akisisitiza kuwa watateua mgombea mwadilifu, mwenye uzoefu na
atakayeuzika kwa wananchi.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walioko tayari
mjini hapa kwa kazi hiyo walilieleza gazeti hili kuwa jukumu kubwa la
kamati hiyo ni kuishauri Kamati Kuu juu ya masuala yote yanayohusu
maadili ya wanachama na wagombea wa nafasi mbali ndani ya chama na
kwenye vyombo vya Dola.
Mjumbe mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe
gazetini kwa kuwa si msemaji alieleza kuwa kama kuna jambo kubwa, kamati
ndogo huwa haikutani, badala yake kamati kubwa ikiwa chini ya Rais
ndiyo hukutana na kuandaa taarifa za kuwasilisha kwenye Kamati Kuu.
Alitolea mfano wa mambo makubwa kuwa ni kama vile
kupitia majina ya wanaowania kuteuliwa kugombea urais, kwamba kazi ya
kamati ni kueleza taarifa za kila mwombaji, mazuri yake, mabaya yake na
ushauri inaoutoa kwa wajumbe wa Kamati Kuu.
Mjumbe huyo alisema, Kamati ya Maadili na Usalama
haina mamlaka ya kukata au kuongeza majina ya wagombea na kwamba mambo
yanayopelekwa kwenye Kamati Kuu ni yale mazito tu.
Kuhusu mambo ya madogo yanayoishia kwenye kamati ndogo, alisema ni yale yanayoonekana yana viashiria vya majungu.
Mangula hakupatikana jana kuzungumzia majukumu ya
kamati hizo lakini Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa
alipoulizwa kwa simu alisema majukumu na mipaka ya Kamati ya Maadili na
Usalama vimeelezwa ndani ya Katiba ya CCM.
Hata hivyo, katika katiba ya CCM matoleo ya 2005
na 2010 kamati hiyo haikuonekana na mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu
ambaye pia hakupenda kutaja jina lake, alisema haijatajwa kwenye kanuni
za uchaguzi wala katiba ya CCM.
Alisema badala yake mchakato wa kumteua mgombea
urais kwa mujibu wa kanuni na katiba unaanzia kwenye Kamati Kuu ambayo
hata hivyo, haiwezi kufanya kazi ya kutoa na kupokea fomu za wagombea
urais, badala yake kamati kama hizo (za maadili) zikawepo kwa ajili ya
kuisaidia Kamati Kuu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye
alipotafutwa kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo, alijibu kwa mkato kuwa
yuko kwenye kikao
Comments
Post a Comment