CHARLES HILLARY AFUNGUKA KUHUSU KULEJEA TANZANIA



Dar es Salaam. Ilitokea, lakini haikuandikwa. Charles Hilary ndiye Mtanzania wa kwanza kutangaza kwa Kiswahili mechi za fainali za Kombe la Dunia akiwa uwanjani.
Ziko redio nyingi zilizowahi kutangaza fainali hizo kwa Kiswahili, lakini zote zilifanya hivyo kwa kuangalia mechi hizo kwenye runinga na si kutokea uwanjani.
Hilo ndilo linalomtofautisha mtangazaji huyo mkongwe wa zamani wa Redio Tanzania na watu wengine wote kwenye fani hiyo. Charles alikuwa ameshikilia microphone akiwa viwanjani.
Rekodi yake inanogeshwa na ukweli kwamba hata fainali hizo za Kombe la Dunia zilikuwa za kwanza kufanyika barani Afrika baada ya taifa la Afrika Kusini kupewa uenyeji wa michuano hiyo mikubwa katika mchezo wa soka duniani.
“Ilikuwa ni furaha zaidi kwangu,” anasema Hilary akikumbuka fainali hizo ambazo hushirikisha timu za taifa za wawakilishi wa mabara yote duniani.
“Mwaka 2010 ndiyo fainali za Kombe la Dunia zilifanyika kwa mara ya kwanza Afrika. Mimi nilikuwa Mtanzania pekee niliyepata nafasi ya kutangaza ‘live’ kwa Kiswahili. Sikutarajia. Hiki ni kitu cha furaha sana kwangu.
“Hakuna Mtanzania mwingine aliyewahi kutangaza ‘live’ na sijui kama itatokea tena hivi karibuni. Kwa kuweka kumbukumbu ya furaha hiyo nilinunua na kurejea na vitu mbalimbali ikiwamo mavuvuzela, nembo za timu za taifa ambazo manahodha wa timu hubadilishana na vitu vingine vingi.”
Hilary anaweza kutangaza vipindi vingine vingi, lakini anajulikana zaidi kutokana na umahiri wake wa kutangaza mpira, kuelezea mwenendo wa mchezo, kueleza haiba za wachezaji, lakini zaidi ana msamiati mkubwa, sitiari na misemo inaomtofautisha na watangazaji wengi wa enzi zake, akiwaacha mbali zaidi watangazaji vijana wa sasa.
Lakini gwiji huyo, ambaye baada ya kufanya kazi Ujerumani na Uingereza amerejea na kujiunga na Azam Media, sasa anasema wakati wake wa kuonyesha umahiri wake kwenye utangazaji mpira, umeisha.
“Mie tena, wakati wa mpira umefika ukingoni. Nimestaafu kutangaza soka, ila sasa nataka kufundisha vijana kutangaza,” anasema Hilary.
“Nilipokuwa Uingereza nilikuwa nawafuatilia (watangazaji mpira wa sasa). Wengi hawatangazi vizuri na sasa nimerudi jukumu langu ni kuwafundisha, sifa nilizopata kwa utangazaji kwa miaka 33 zinatosha,” anasema Hilary, mmoja wa watangazaji wa kwanza wa kituo cha Radio One Stereo alichojiunga nacho mwaka 1994.
“Tatizo katika utangazaji ni radio binafsi kutaa faida ya haraka. Hata hao wanaotangaza mpira ni juhudi zao, hawana A, B, C (mafunzo) za utangazaji; ni vurugu mechi. Wanazungumza sana, wanataka kuwa wachambuzi zaidi badala ya kutangaza.

Comments