WARIOBA ASEMA JAMBO KWA CCM



Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba amesema CCM inakabiliwa na kazi ngumu ya kupata mgombea wa urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka huu, akionya kuwa makundi ya urais yasipomalizwa yanaweza kufika hadi ngazi ya kata.
Makada 38 wamejitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho tawala ya kugombea urais katika kipindi ambacho kuna ongezeko kubwa la nguvu ya vyama vya upinzani, huku vyama vinne vikiwa vimeamua kusimamisha mgombea mmoja.
  
Tayari vikao vya kujadili jinsi ya kumpata mteule wa kupeperusha bendera ya chama hicho vimeshaanza kwa wenyekiti na makamu wao kukutana na jana Kamati Kuu ilikuwa inakutana mjini Dodoma.
Akiangalia hali hiyo, Jaji Warioba aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho tawala kinatakiwa kuwa makini katika mchakato huo, kwa maelezo kuwa unaweza kuacha majeraha makubwa kutokana na makundi yaliyoibuka.
“CCM inakabiliwa na wakati mgumu wa kupitisha jina la mgombea urais kutokana na waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 38, na mpaka sasa imekuwa ni vigumu kutabiri atakayepitishwa, jambo ambalo halikujitokeza wakati wa upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995 na 2005,” alisema Jaji Warioba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kila unapofika Uchaguzi Mkuu kunakuwa na changamoto zake, lakini mwaka huu CCM inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kwa sababu uchaguzi huo utamleta rais mpya na mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Alisema jambo la kwanza lililotokea katika mchakato wa kumpata mgombea urais litakalokifanya chama hicho kuwa na wakati mgumu ni kitendo cha baadhi ya wagombea kueleza sera zao, wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya uchaguzi.
“Waliotangaza nia wamekuwa wakieleza sera zao na ukiwasikiliza unaona kama walikuwa wagombea binafsi hivi kwa sababu CCM ina sera, wanayo ilani ambayo ipo tayari na yeyote atakayepeperusha bendera ya CCM lazima ajikite kwenye ilani ya chama,” alisema jaji Warioba.
“Kama mtu ametangaza sera na vipaumbele vyake na havifanani na vipaumbele vya ilani ya chama unafanyaje? Ni mtihani mwingine huo.”
Alisema jambo la pili ni kukiukwa kwa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote anayehusika kwenye ngazi ya maamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais, huku akiwatolea mfano wajumbe wote wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao ndio humchagua mgombea urais wa chama hicho.
“Nimeambiwa kwamba wajumbe wa mkutano mkuu walikatazwa kudhamini wagombea, lakini tulivyoona ni kwamba viongozi wengi wameonyesha waziwazi wapo kundi gani, wapo waliojitokeza na kusema na wengine hawakusema lakini wanajulikana wanamuunga mkono mgombea gani,” alisema.
“Hawa ndio watakwenda kuchuja, sasa hapa itakuwa kazi ngumu na inawezekana kukawa na mgongano wa maslahi na hilo lisipoangaliwa linaweza kufanya mchujo ukaonekana kuwa haukuwa wa haki. Jambo hili linatakiwa kuangaliwa na hasa kwa kuwa kuna makundi.”

Comments