DK SHEIN AVUKA HATUA YA KWANZA
Zanzibar.Kamati Kuu ya Halmashauri ya CCM Zanzibar imempendekeza Dk Ali Mohamed Shein kwa kauli moja kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar baada ya kuchukua fomu na kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo kupitia chama hicho, Zanzibar
.
Kabla ya wajumbe wa kamati maalumu kuanza kujadili
ajenda ya mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar katika kikao
kilichofanyika Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar jana,
walimchagua kwa kauli moja Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal kuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alisema kikao hicho kilipokea na kujadili jina la Dk Shein baada ya
kujitokeza kwa mara ya pili akiiomba CCM imchague kuwa mgombea wa nafasi
ya urais wa Zanzibar.
“Kikao cha Kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya
CCM Zanzibar kwa kauli moja imempendekeza kwa Kamati Kuu ili ateuliwe
kugombea tena kiti cha urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
huu,” alisema Vuai.
Alisema hatua inayofuata baada ya kupendekezwa,
jina lake litawasilishwa na kujadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu na
Halmashauri Kuu ya CCM kabla ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama
hicho.
Wakizungumza baada ya kikao, Wajumbe wa NEC
akiwamo Dk Maua Daftari alisema DK Shein ameonyesha uadilifu katika
kipindi cha uongozi wake pamoja na kufanikiwa kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.
Alisema DK Shein amekuwa karibu na watendaji wakuu
wa Serikali kwa kufanya vikao vya tathimini kila baada ya miezi mitatu
ili kuangalia mafanikio na matatizo, utaratibu ambao umesaidia kuwapo
kwa uwajibikaji wa pamoja katika utekelezaji wa kazi za Serikali.
Upande wake Rashid Ali Juma alisema Dk Shein
katika kipindi cha miaka mitano ameonyesha uwezo mkubwa na amefanikiwa
kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa umakini mkubwa licha ya
kuwapo kwa changamoto zilizokuwa zikijitokeza.
Mjumbe wa NEC, Alex Simon Marangira alisema Dk
Shein ameleta mabadiliko makubwa ya viwango vya mishahara kwa
wafanyakazi na watendaji wakuu wa Serikali, hatua ambayo imewasadia
kupunguza ukali wa maisha katika kipindi chote cha uongozi wake.
Marangira alisema wakulima wa zao la Karafuu kwa
mara ya kwanza wameshuhudia bei ya zao hilo ikipanda kwa kiwango kikubwa
kutoka Sh3,500 hadi Sh 14,000 kwa kilo hatua ambayo imesadia kuinua
kipato cha wakulima wa Unguja na Pemba pamoja na kupunguza kwa kiwango
kikubwa biashara ya magendo ya zao hilo.
Dk Shein ni miongoni mwa wagombea sita
waliotangaza nia ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi
wa mwaka huu wote wakitokea Kisiwani Pemba akiwamo mwanasiasa mkongwe,
Seif Sharif Hamad, (CUF) Hamad Rashid Mohamed (ADC), Juma Ali Khatibu
(Tadea) Ambary Khamis Haji (NCCR- Mageuzi) na Soud Said Soud wa (AFP)
Zanzibar.
Comments
Post a Comment