JE UNAMKUMBUKA KIGOGO WA IKULU ALIE KILI KUPOKEA FEDHA ZA ESCROW HUYU HAPA
SHABANI Gurumo- mtumishi wa Ikulu mwenye
cheo cha mnikulu, leo amefikishwa mbele ya Baraza la Sekretarieti
Maadili ya Viongozi wa Umma akikabiliwa na kosa la kukiuka maadili kwa
kupokea sh. 80,850,000.
Mnikulu huyo anadaiwa kupokea mgawo huo
kutoka kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and
Marketing Ltd, James Rugemalira, Anaripoti Deusdedit Kahangwa…(endelea).
Mbele ya Baraza linalokutana katika
ukumbi namba 2 wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Gurumo alisomewa
mashtaka kadhaa na mwanasheria wa sekretarieti hiyo, Hassan Mayunga.
Kwa mujibu wa Mayunga, Gurumo anatuhumiwa kukiuka vifungu mbalimbali vya sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995 kama ilivyorekebishwa mwaka 2001.
Katika shitaka la kwanza, Gurumo alidaiwa
kufanya kazi bila kuzingatia viwango vya juu vya maadili na hivyo
kushindwa kulinda na kuimarisha imani ya wananchi na matumaini katika
uadilifu, haki na kutopendelea kwa serikali, jambo ambalo ni kinyume cha
ibara ya 6 (a) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Katika shitaka la pili, Gurumo alidaiwa
kushindwa kupanga mambo yake kwa namna ambayo ingezuia kutokea kwa
mgongano halisi wa maslahi au kuwepo na uwezekano wa mgongano au
kuonekana kuwepo mgongano wa mashali katika utendaji kazi wake, jambo
ambalo ni kinyume cha ibara ya 6(e) ya sheria ya maadili ya viongozi wa
umma.
Katika shitaka la tatu, Gurumo alidaiwa
kuomba na kupokea fadhila za kiuchumi ambazo sio zawadi ndogo, wala
ukarimu wa kawaida au fadhila ya thamani ya kawaida, jambo ambalo ni
kinyume cha ibara ya 6(f) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Katika shitaka la nne, Gurumo alidaiwa
kupata kwa makusudi manufaa makubwa ya kifedha, jambo ambalo ni kinyume
cha ibara ya 12(1)(e) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Na katika shitaka la tano, Gurumo
alidaiwa kupokea zawadi yenye thamani inayozidi shilingi 50,000 na
kukataa kuitaja na kuikabidhi zawadi hiyo kwa Afisa Mhasibu wa ofisi
inayohusika kinyume cha ibara ya 12(2) ya sheria ya maadili ya viongozi
wa umma.
Mwansheria wa Sekretarieti alilieleza
Baraza lenye wajumbe watatu, chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu Hamis
Msumi, kwamba Gurumo alipokea shilingi 80, 850,000 kutoka kwenye Kampuni
ya VIP Engineering and Marketing Ltd tarehe 05 Februari 2014.
Mwanasheria lisema kuwa fedha hizo
zilipokelewa kupitia akaunti namba 00110102645401 inayomilikiwa na
Gurumo katika Benki ya Mkombozi Dar es Salaam baada ya akaunti hiyo
kufunguliwa tarehe 04 Februari 2014.
Pia, mwanasheria huyo aliliambia Baraza
kwamba, kufikia 18 Desemba 2014, tayari kigogo huyo wa Ikulu alikuwa
amechukua kiasi cha shilingi 77,529,100 kutoka kwenye akaunti hiyo kwa
ajili ya matumizi binafsi.
Kadhalika, mwansheria alilieleza Baraza
kwamba, tayari sekretarieti ya maadili ilikwisha mhoji Gurumo kuhusu
fedha hizo na akakiri kumiliki akaunti hiyo ambako fedha hizo
ziliingizwa.
Baraza liliarifiwa kuwa Gurumo alikiri
kwamba ndiye aliyehusika na miamala ya kuchukua kiasi cha shilingi
77,529,100 kutoka katika akaunti hiyo.
Mara tu baada ya Gurumo kusomewa mashtaka
hayo, huku akiongozwa na wakili wake, Lucas Charles kutoka Kamanija and
Co Advocates ya Buguruni Malapa Dar es Salaam, alisema mambo matatu
makubwa.
Kwanza, alikanusha kupokea “zawadi”
kutoka kwa mfanyibiashara James Rugemalira; pili alikanusha kupokea
“zawadi” kutoka kwenye kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd; na
tatu alikiri kupokea “fedha” kiasi cha shilingi 80,850,000 kutoka kwa
James Rugemalira.
Kwa mujibu wa Gurumo alichopewa ni “fedha” lakini sio “mshahara, posho, urithi, na wala zawadi”.
Majibu haya tata yalizua mshangao kwa
wananchi waliokuwepo. Pia yalizua mvutano mkubwa kati ya Gurumo na
wanasheria wa sekretarieti ya maadili, kwa upande mmoja, na pia mvutano
kati ya wanasheria hawa na wakili wa Gurumo, kwa upande mwingine.
Baada ya mahojiano hayo ya kusisimua
Mwenyekiti wa Baraza aliahirisha kikao na kuwataka wanasheria wa
sekretarieti na wakili wa Gurumo kuwasilisha utetezi wao wa mwisho kabla
ya 13 Machi 2015. Baada ya hapo ataandika hukumu na kuiwasilisha kwa
Rais Kikwete. Alisema kuwa hukumu ya aina hiyo haisomwi hadharani na
Gurumo pamoja na wakili wake hawatapata nakala.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na
Baraza la Maadili viongozi mbalimbali serikalini wanaendelea kuhojiwa
kwa tuhuma za kukiuka taratibu za utumishi wa umma katika kutekeleza
majukumua yao.
Kufikia 04 Machi 2015, tayari Mbunge wa
Bariadi Magharibi, Andrew Chenge; aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Makazi, Prof. Profesa Anna Tibaijuka; Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujuna; na Mnikulu
Shaban Gurumo wamehojiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na
Udhamini (RITA), Philip Saliboko; Naibu Kamishna Upelelezi na Kodi
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo; Mkurugenzi Mdhibiti
Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Dk. Benedict Diu; Meya wa Halmashauri
ya Manispaa ya Tabora, Gulam Remtullah; na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya
ya Korogwe, Mrisho Gambo ni miongoni mwa watu ambao wanatarajiwa
kuhojiwa na Baraza la Maadili muda wowote kuanzia sasa.
Comments
Post a Comment