MAWAZIRI WAWILI WATUPWA JELA
Dar es Salaam. Mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), wamehukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh5 milioni baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.5 bilioni.
Akisoma hukumu hiyo kuanzia saa 7.15 mchana hadi
saa 8.11 mchana, Hakimu Mkazi, Sam Rumanyika alisema baada ya jopo la
mahakimu watatu kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 13 wa upande wa
mashtaka na wengine sita wa utetezi wakiwamo washtakiwa wenyewe,
wameamua kumwachia huru mshtakiwa wa tatu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa
zamani wa Fedha, Gray Mgonja. Hakimu Rumanyika alisema wanamuachia huru
Mgonja kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka
yote 11 yaliyokuwa yakimkabili.
Hakimu Rumanyika alisema wanamtia hatiani Mramba katika mashtaka yote 11 yaliyokuwa yakimkabili.
Alisema katika shtaka la kwanza hadi la 10 ambayo
ni ya matumizi mabaya ya madaraka, atakwenda jela kifungo cha miaka
mitatu jela kwa kila shtaka na vifungo hivyo vitakwenda sambamba, hivyo
atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Katika shtaka la 11 ambalo ni la kuisababishia
Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni pia alitiwa hatiani na kuhukumiwa ama
kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa fidia ya Sh5 milioni na kuwa
vifungo hivyo vyote vitakwenda sambamba hivyo Mramba atatumikia kifungo
cha miaka mitatu jela. Wakili wake Peter Swai alisema atakata rufaa.
Kuhusu Yona, Hakimu Rumanyika, alisema naye
wanamtia hatiani katika shtaka la kwanza, la pili, la tatu na la tano
ambayo ni ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na la 11 la
kuisababishia hasara Serikali ya Sh11.7 bilioni.
“Yona katika kila kosa atatumikia kifungo cha
miaka mitatu jela na adhabu zote zinakwenda sambamba hivyo atatumikia
kifungo cha miaka mitatu jela.
“Katika shtaka la kusababisha hasara atalipa fidia
ya Sh5 milioni na iwapo atashindwa atakwenda jela miaka mitatu,”
alisema Hakimu Rumanyika.
Ilivyokuwa
Kabla ya hukumu kutolewa, mawakili wanaowatetea
washtakiwa hao, Swai anayemtetea Mramba na Eliasa Msuya anayemtetea Yona
waliiomba Mahakama iwape adhabu nyepesi washtakiwa hao kwa sababu hilo
ni kosa lao la kwanza, umri wao ni mkubwa Yona (76) na Mramba (75),
wanaumwa na walikuwa wakitibiwa India wakati wa usikilizwaji wa kesi
hiyo.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumain
Kweka aliiomba Mahakama kutoa adhabu kulingana na matakwa ya sheria ili
iwe fundisho kwa watu wote ambao wanakwenda kinyume na majukumu
waliyopewa.
Baada ya kusomewa hukumu hiyo, Mgonja aliondoka
mapema katika eneo la Mahakama, Mramba na Yona wao wakiwa chini ya
ulinzi walipelekwa eneo la chini na walionekana wakizungumza na ndugu na
jamaa zao, akiwamo aliyekuwa Balozi wa Italia, Profesa Costa Mahalu
wakati wakisubiri kupelekwa gerezani.
Comments
Post a Comment