MBUNGE AJIVUA UANACHAMA CHADEMA
Sumbawanga. Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi ametangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza mjini Mpanda katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kashaulili, jana Arfi
aliwaeleza wananchi wa Mpanda kuwa uanachama wake ndani ya Chadema
utakoma mara tu baada ya kuvunjwa Bunge Julai 9.
Pia, alitumia mkutano huu kuwaaga wananchi wa jimbo hilo akisema hatagombea tena nafasi hiyo aliyoitumikia kwa miaka 10.
Arfi alifafanua kuwa hayuko tayari kugombea jimbo
hilo kupitia chama chochote cha siasa na kauli hiyo imelenga kuondoa
uvumi uliokuwa umeenea kwamba alikuwa na nia ya kugombea kupia ama ACT –
Wazalendo au CCM.
Alisema amekuwa akishangazwa na kauli ambazo
zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wanachana na wapenzi wa Chadema kuwa
hajafanya lolote kwenye chama hicho.
Alisema kama kuna mtu anayekifahamu vizuri chama hicho ni yeye, hivyo haoni sababu za watu kumbeza.
Alisema alikuwa ameamua kukaa kimya na kuwa akiamua ‘atamwaga mboga’ ili watu wafahamu upungufu ulioko ndani ya chama hicho.
Alisema hagombei katika jimbo hilo na kama kweli
chama hicho kina nguvu, basi kilitetee, akisisitiza kuwa ana uhakika
jimbo hilo litakwenda CCM kwa kuwa wananchi wa Mpanda Mjini walikuwa na
mapenzi na mtu siyo chama.
Arfi aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema
kabla kujiuzulu wadhifa huo, aliwahi kuhusishwa kusuka mpango wa
kumwezesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupita bila kupingwa katika
kinyang’anyiro uchaguzi wa mwaka 2010 katika Jimbo la Katavi kwa
kuwashawishi baadhi ya wagombea kuondoka majina yao.
Hata hivyo, Arfi amekuwa akikanusha tuhuma hizo,
hali ambayo pia ilisababisha kutokuelewana na baadhi ya viongozi wenzake
na kusababisha kujiuzulu nafasi yake ya umakamu mwenyekiti.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili
walionyesha kushtushwa na kauli ya mbunge huyo kujiondoa Chadema lakini
wakasema ametimiza haki yake ya kikatiba kuchagua sehemu iliyo sahihi
kwake.
Mmoja wa wananchi hao, Abdallah Hussein alisema:
“Arfi amekuwa mvumilivu sana ndani ya Chadema lakini anayo ya moyoni
sasa kwa muda mrefu amekaa kimya aliogopa ya Zitto Kabwe yasimtokee,
sasa ameweka bayana msimamo wake acha tuheshimu mawazo yake.”
Comments
Post a Comment