MESS AWAGALAGAZA SIMBA SC

SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF), leo limeamua mchezaji Ramadhani Yahya Singano 'Messi' ni huru na sasa anaweza kujiunga na timu yoyote- maana yake milango iko wazi kusaini Azam FC.
Taarifa kutoka kwenye kikao cha Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF kilichofanyika leo,
imesema kwamba Simba SC walishindwa kutekeleza baadhi ya vipengele vya Mkataba, hivyo wanapoteza haki za kummiliki mchezaji huyo.
Chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa, Kamati hiyo imejiridhisha Messi hakuwahi kupewa nyuma ya kuishi na Simba SC jambo ambalo ni kinyume cha Mkataba baina yake na klabu hiyo.
Simba SC iliwakilishwa na Mwenyekiti wake wa Kamati yake ya Usajili, Zacharia Hans Poppe na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collins Frisch wakati Messi alifika na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA), Mussa Kisoky.  
Maamuzi haya ni faraja kwa Messi ambaye anahusishwa kwa kiasi kikubwa na kuhamia Azam FC.
Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka minne iliyopita, hivi karibuni ameibua shutuma dhidi ya klabu yake hiyo kwamba imeghushi Mkataba wake.
Messi anadai Mkataba wake halali ulikuwa unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika mwakani.
Lakini Simba SC imeendelea kusistiza mchezaji huyo alikuwa ana Mkataba wa miaka mitatu.
Awali, Sekretarieti ya TFF, chini ya Katibu wake, Selestine Mwesigwa ilizikutanisha pande zote mbili, mchezaji na Simba SC na kuamuru waketi chini na kutayarisha Mkataba mpya baada ya kuona huu wa sasa una mushkeli.
Hata hivyo, Messi akakataa na kuamua kulihamishaia suala hilo Kamati ya Sheria ambayo leo imempa kile alichotaka ‘kuwa mchezaji huru’.

Comments