RISASI ZALINDIMA ZANZIBAR
Vurugu hizo zimetokea baada ya watu waliokuwa
wamekusanyika katika Msikiti wa Kubini kwa madhumuni ya kupinga kazi
hiyo ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura wakituhumu kuwapo kwa
mamluki waliokuwa wakiandikishwa, lakini wakajikuta wakivamiwa na kundi
la askari wasiokuwa na sare ambao walikuwa na silaha za moto.
Waliojeruhiwa kwa risasi ni Kheri Makame Hassan
(42) na Ramadhani Hija Hassan (29) wote wakazi wa Makunduchi wakati Ali
Seif Issa (38), Ali Hassa Hassan (70) kutoka Paje akiwa amepigwa kwa
magongo na nondo na kuumia vibaya miguuni, na Hassan Ali Ameir (43).
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati
tofauti hospitalini hapo, majeruhi wao walisema walikuwa katika kituo
cha Nganani, Shehia ya Nganani Kusini Unguja ndipo walipokuja watu
waliovaa vinyago na kuwaamuru waondoke eneo hilo wakati uandikishaji
ukiendelea.
“Ilikuja gari na watu waliojifunika nyuso zao
wakatuambia tuondoke na sisi tukakataa kwa sababu tulikuwa tunazuia
kuandikishwa mamluki katika eneo letu. Baada ya kubishana pale wakaenda
kuchukua gari nyingine wakaanza kutupiga,” alisema Kheri ambaye amepigwa
risasi ya pajani.
“Watu waliojifunika nyuso walikuja mara mbili na
kuondoka kabla ya kufanya shambulio na kufanikiwa kuondoka katika eneo
la tukio la Nganani kwa kutumia magari mawili,’ alisema Faki huku
akilalamika kusikia maumivu.
Shuhuda wa tukio hilo, Ameir Mussa, mkazi wa
Makunduchi, alisema kwamba waliamua kukusanyika eneo la msikiti
wakitafakari jinsi ya kuzuia uandikishaji wa wapigakura mamluki, ambao
ni pamoja na walio na umri mdogo.
“Lilikuja kundi la watu mara mbili na kuondoka.
Walikiwa wamefunika nyuso zao na waliporudi kwa mara ya mwisho
walitushambulia kwa kutumia silaha za kienyeji na baadaye kufyatua
risasi za moto na kujeruhi watu wawili,” alisema Mzee Ameir.
Daktari wa zamu wa Hospitali ya Al Rahma, Seif
Suleiman alithibitisha kupokea majeruhi na kusema kwamba katika hatua za
awali wanazuia damu kuvuja kutoka kwenye majeraha.
Alisema wanaendelea na vipimo ili kujua majeraha
hayo yamesababishwa na nini. “Tumewafanyia x-ray ili kujua majeraha yao
yanatokana na nini lakini yanaonesha wazi kuwa ni majeraha kama ya
risasi kwa kuwa risasi jeraha lake linakuwa ni kitobo kidogo inapoingia
lakini kitobo kikubwa inapotokea risasi.” Dk Suleiman alisema majeruhi
hao wanaendelea vizuri baada ya kutibiwa na wengine wataruhusiwa
watakapopata nafuu.
“Wapo walioumia sana hao wataendelea kuwepo
hospitali kwa sababu wametokwa damu nyingi sana na kutoka Makunduchi
hadi Mjini ni mbali kwa hivyo wanahitaji kupumzishwa kwanza hadi hapo
watakapopata nafuu,” aliongeza Dk Suleiman.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Juma
Saadi alisema kuwa katika mkoa wake kuna uandikishaji wananchi
kuwaingiza kwenye Daftari la Wapigakura, lakini hana taarifa za watu
kupigwa risasi na kwamba anachojua ni risasi hizo kupigwa hewani na
hivyo hazijajeruhi mtu.
Comments
Post a Comment