STEVEN KESHI ATUPIWA VILAGO NIGERIA


SHIRIKISHO la Soka Nigeria (NFF) limemfukuza kocha Stephen Keshi (pichani) ukocha Mkuu wa timu ya taifa, Super Eagles. Taarifa ya Kamati ya Utendaji ya NFF jana imesema kwamba uamuzi huo umechukuliwa baada ya kupitiwa taarifa za Kamati ya Nidhamu, Ufundi na Maendeleo za NFF. Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Utendaji, Makamu wa kwanza wa Ras wa NFF, Seyi Akinwunmi amewahakikishia Wanigeria kwamba uamuzi huo haujachukuliwa kwa kukurupuka, bali umezingatia maslahi ya soka ya Nigeria. Amemshukuru Keshi kwa huduma zake kwa nchi yake na kumtakia kila la heri popote atakapokwenda. “Kwa muda, Super Eagles itakuwa chini ya makocha Salisu Yusuf aliyekuwa Msaidizi wa Keshi na Kurugenzi ya Ufundi ya NFF chini ya kocha Shuaibu Amodu, hadi hapo Shirikisho litakapomteua mwalimu mwingine kubeba jukumu hilo,” alisema Akinwunmi.    Keshi, ambaye ni Nahodha wa zamani Super Eagles amekuwa kocha wa timu ya taifa kwa vipindi vitatu tofauti kati ya mwaka 2011 na 2015, na mafanikio yake makubwa yakiwa ni kuwapa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013 Afrika Kusini na kufika Raundi ya Pili katika Kombe la Dunia mwaka jana Brazil. Keshi anafukuzwa miezi miwili kabla ya Nigeria kusafiri kuja Tanzania kumenyana na Taifa Stars katika mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ta Afrika 2017.

Comments