SUNDAY OLISEH KUINOA NIGERIA

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Sunday Oliseh (pichani) amethibitishwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles baada ya Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) kuthibitisha mazungumzo yanaendelea vizuri baina yao.
Taarifa zilivuja juzi kwamba NFF ipo katika majadiliano na Oliseh kufuatia kufukuzwa kwa Stephen Keshi mwishoni mwa wiki baada ya kukiuka Mkataba wake.

"Shirikisho la Soka Nigeria limethibitisha lipo kwenye mazungumzo na Nahodha wa zamani wa Super Eagles, Sunday Oliseh ili kuchukua nafasi iliyo wazi ya Ukocha Mkuu wa timu," taarifa ya NFF imesema katika tovuti yake jana.

Maelezo zaidi yamesema kwamba, Rais wa NFF, Amaju Pinnick alikutana na Oliseh mjini London kwa mazungumzo juzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya NFF na Kamati ya Maendeleo amethibitisha; “Ofa imetolewa, na kuna maelewano, lakini tunafanyia kazi mambo machache ya mwishoni ya makubaliano kwa siku chache. Wazi, Kamati Kuu inatakiwa kutoa baraka zake kwa uteuzi wake baada ya makubaliano yote kukamilika,".

NFF imesema kwamba Oliseh pia anatarajiwa kuja na Msaidizi wa kigeni na majukumu yake kwa ujumla yatahusu mipamgo ya maendeleo,".

Pamoja na hayo, kocha wa muda, Salisu Yusuf atabakia kwenye benchi la Ufundi na kwa mujibu wa NFF, yeye atasimamia mchakato wa uteuzi wa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani.

NFF inatarajiwa kuingia Mkataba wa muda mrefu na Oliseh ambao unaweza kuwa wa miaka mitano, ili atengeneze vizuri mipango ya maendeleo.
Pinnick amevutiwa na wasifu (CV) wa Oliseh a upeo wake kisoka tangu enzi zake anacheza na amesema; “Sunday Oliseh ana uzoefu wa kutosha na uelewa wa mchezo, na wazi atatusaidia juu ya tunachokifanya. Anaendana na dira yetu katika kuendeleza soka ya Nigeria. Atalinda heshima ya wachezaji na tunaamini ni muwajibikaji mzuri atakayefanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Kamati ya Ufundi na Maendeleo,"amesema.
NFF inatarajiwa kumtambulisha Oliseh wiki ijayo na moja kwa moja kuanza kazi Eagles ambayo Septemba itasafiri hadi Dar es Salaam kuja kumenyana na Tanzania mechi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.  

Nahodha huyo wa zamani wa Nigeria ana leseni ya UEFA Pro na amewahi kufundisha timu ya daraja la chini Ubelgiji, Vervietois kati ya mwaka 2008 na 2009.

Comments