WABUNGE WA UPINZANI WAMSUSIA TENA RAIS



Dodoma. Historia inaelekea kujirudia, kama ilivyokuwa wakati Rais Jakaya Kikwete akizindua Bunge la 10 na wabunge wa Chadema kususia hotuba yake, ndivyo itakavyokuwa atakapolihutubia Bunge kwa mara ya mwisho Alhamisi bila kuwapo wabunge hao na wenzao kutoka NCCR – Mageuzi na CUF wanaounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).
Wabunge wa Chadema wakati huo wakiunda KUB peke yao, walisusia hotuba ya Rais Kikwete Novemba 30, 2010 wakipinga matokeo ya uchaguzi uliomweka madarakani.
Safari hii wakati Rais Kikwete akitarajia kulihutubia Bunge hilo kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja rasmi kwa tangazo la Serikali (GN) litakalotolewa baadaye, hali inaelekea kuwa vilevile, lakini kutokana na sababu tofauti.
Kiongozi wa KUB, Freeman Mbowe alisema jana kwamba wabunge wanaounda kambi hiyo hawatahudhuria vikao vilivyosalia kwa sababu ya Serikali kupitisha miswada mitatu ya petroli na gesi kinyume cha kanuni na sheria.
“Miswada hii inahitaji umakini mkubwa kabla ya kuigeuza kuwa sheria,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa utaratibu uliotumika utazaa sheria mbaya.
Alisema KUB na viongozi wote wa vyama vinavyounda Ukawa walikubaliana kuishauri Serikali, uongozi wa Bunge na wabunge wa CCM wasiwe na haraka katika kuipitisha miswada hiyo lakini hawakusikilizwa.
Mbowe alisema walikubaliana kuiacha miswada hiyo ipitishwe na Bunge la 11 litakaloanza Novemba ili kufanya uchambuzi wa kina kwa kuzingatia masilahi mapana ya Taifa.
Alisema licha ya semina mbalimbali kati ya wabunge wa pande mbili, kwa sababu wanazozijua wenyewe, Serikali na uongozi wa Bunge waliamua kuendelea kuvunja kanuni za Bunge kwa kupitisha miswada hiyo kwa utaratibu wa “voda fasta.”
“Tunatambua kuwa pamoja na maudhui mengine katika miswada hii, kuna kipengele muhimu ambacho kinalazimisha mikataba yote iliyosainiwa awali, ya gesi na mafuta, isibatilishwe.
“Mikataba ambayo leo hii ipo katika utekelezaji imekuwa ikilalamikiwa na watu wengi kuwa ina mapungufu makubwa na hivyo inalikosesha Taifa mapato mengi,” alisema Mbowe katika mkutano uliohudhuriwa pia na baadhi ya wabunge wa CUF na Chadema.
Alisema kwa sababu uongozi wa Bunge umewadhalilisha kwa kuwatoa wabunge 43 bungeni kinyume cha taratibu, ni dhahiri ulikusudia kuipitisha miswada yote bila kujali ushauri.
Mbowe alisema uongozi unaomaliza muda wake una agenda ya siri inayoufanya kulazimisha sheria hizo kupitishwa katika utaratibu huo.

Comments