WALEMAVU WA NGOZI WAZICHAPA IKULU KABLA YA KUONANA NA RAIS
KIKAO baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi viongozi
wa Chama Cha Watu Wenye Ulemavu wa ngozi (Albino), nusura kishindwe
kufanyika baada ya Albino kuvurugana na viongozi wao katika lango kuu la
Ikulu.
Sababu ya vurugu hizo ni wanachama
kupinga uwakilishi wa viongozi wao, wakidai muda wa kuwa madarakani
ulikoma tangu mwaka jana na hivyo kutaka waruhusiwe waingie wote kuonana
na rais.
Wamesema kuwa wawakilishi hao wamekuwa
mstari wa mbele kutetea maslahi yao kila wanapopata fursa ya kukutana
naviongozi wakuu badala ya kueleza matatizo ya wenzao.
Ilikuwa kama “sinema” kuona watu
waliopata fursa ya pekee ya kuonana na rais kuzungumzia hoja zao
kutokana na mauaji ya yanayoendelea nchini dhidi yao, badala yake
wanageuka kuchapana makonde wenyewe kwa wenyewe.
Lakini heka heka iliyotokea katika eneo la mapokezi iliwalazimu maafisa wa Ikulu kuwatawanya walemavu hao.
Ni muda mfupi baada ya ukaguzi kuanza
kufanyika katika moja ya lango la kuingilia Ikulu, kundi moja la
walemavu hao waliokuwa katika moja ya chumba wakaanzisha malalamiko kwa
sauti huku viongozi wao wakiwa wanajiandaa kuruhusiwa kuingia ndani.
Kelele hizo na mabishano hayo miongoni
mwao kwa mbali ikaanza kuonekana ni dosari hasa baada ya kila mmoja
kuanza kusema lake kupinga ushiriki wa viongozi hao.
Kutokana na vurugu hizo, maafisa wa Ikulu
waliwatawanya na kutoka nje ya lango na hapo ikawa mwanzo wa sakata
jipya baada ya kuanza kulumbana na viongozi wao na hatimaye kupigana.
Wateta na JK
Baada ya rabsha hizo kutulizwa, maafisa
wa Ikulu waliwaongoza wawakilishi wa walemabu hao hadi kwa Rais Kikwete,
ambaye katika mazungumzo yake amesema Serikali inasikitishwa na
kufedheheshwa sana na mauaji dhidi yao na kwamba itafanya kila
linalowezekana kukomesha mauaji haya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais
Kikwete amewaeleza viongozi hao walioongozwa na Mwenyekiti wao, Ernest
Kimaya kuwa; “Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha
sana”.
“Msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo,” amesema rais.
Katika kikao hicho viongozi hao, wamesoma
risala ambayo imetoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali na
hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda kamati ya pamoja ambayo
itajumuisha Serikali, viongozi wa Albino, viongozi wa waganga wa jadi na
wadau wote wakuu katika suala hili ili kupata mapendekezo na mkakati wa
pamoja ambao hatimaye mauaji haya kukomeshwa kabisa nchini.
Rais Kikwete amesema mauaji hayo
hayafanywi na serikali bali watu ambao wako katika jamii kwa
kushirikiana na waganga wa jadi na watu wengine wenye tamaa mbalimbali
katika jamii hivyo na kwamba ni lazima yakomeshwe.
“Kwenye familia, jamii na hatimaye
vyombo vya ulinzi na usalama na hilo ndiyo jukumu kubwa ambalo serikali
inapaswa kulisimamia na tutalisimamia kwa ushirikiano wa pamoja,”
ameahidi.
Rais amesisitiza kuwa kamati hiyo ya
pamoja itaweka mikakati ya kuwabaini wale wote wanaohusika kuanzia
wakala, waganga na hatimaye wale wanaonufaika na viungo vya walemavu
hao.
Pia, aliahidi kuwa serikali itasaidia
familia na wahanga wa vitendo vya mauaji kwa hali na mali ili waweze
kujimudu na pia kuwapa ushauri nasaha ili kuondokana na majonzi
yanayosababishwa na vitendo hivyo kwani vinawaletea waathirika na watu
wanaoishi nao mfadhaiko na msongo wa mawazo katika jamii.
Katika kikao hicho, viongozi wametoa
kilio chao kwa serikali kuziangalia na kuzimulika taasisi zisizo za
kiserikali ambazo pamoja na kujipambanua kuwa zinatetea haki za Albino
nchini bado hazina mkakati wa pamoja na hazipo wazi kwa walengwa hapa
nchini.
Naye Ernest Kimaya-mwenyekiti wa walemavu
hao, ameelezea masikitiko yake kwa rais kuhusu vurugu zilizojitokeza
muda mfupi miongoni mwa kabla ya kikao hicho.
Kwa mujibu wa Kimaya, uchaguzi haukuweza
kufanyika kutokana na ukosefu wa fedha na wamemuomba rais awasaidie
kutimiza azma yao ya kuitisha mkutano na kuchagua viongozi wa chama
chao.
Kimaya ameongeza kuwa wamepanga kufanya
mkutano huo wa kuchagua viongozi katikati ya mwaka huu ambapo pia dunia
itakua inaazimisha siku ya watu wenye Albino duniani
Comments
Post a Comment