DK. SLAA KULEJEA OFISIN CHADEMA

slaa
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, anatarajiwa kuwasili ofisini kwake leo, baada ya kutoweka tangu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alipojiunga na chama hicho hivi karibuni.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Baraza Kuu la chama hicho kuridhia apumzike kwa muda, baada ya kutofautiana na Kamati Kuu kwa kile kilichoelezwa kumkaribisha Lowassa.
Vyanzo vya uhakika ndani ya Chadema vilivyozungumza na MTANZANIA juzi na jana, vilisema Dk. Slaa huenda akarejea ofisini leo kutokana na mazungumzo yaliyofanyika kwa nyakati tofauti na viongozi waandamizi wa chama hicho.
“Jana (juzi) mzee Philemon Ndesamburo na makada wengine wa chama walikwenda nyumbani kwa Dk. Slaa kwa ajili ya mazungumzo, na kwamba amekubali, amesema atarejea ofisini kesho (leo),” alisema mtoa habari huyo.
Vyanzo hivyo vilisema Dk. Slaa amekubali kurudi ofisini na kuendelea na shughuli za chama baada ya Ndesamburo na makada wengine wanaoheshimika ndani ya chama hicho kuzungumza naye.
Mazungumzo hayo yanadhihirishwa pasipo shaka na picha zilizosambaa mitandaoni juzi, zilizomwonyesha Ndesamburo akiwa na Dk. Slaa na makada wengine wa chama hicho.
Mmoja wa makada wa chama hicho aliyeshiriki mazungumzo hayo juzi, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alilidokeza gazeti hili kuwa walielewana na Dk. Slaa na akaahidi kuwa atarejea ofisini muda wowote.
“Ni kweli tumezungumza na Dk. Slaa, na amekubali atarejea ofisini muda wowote, mengine tuliyozungumza siwezi kukwambia,” alisema kada huyo.
Akihutubia wajumbe wa Baraza Kuu wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema amekutana na Dk. Slaa kwa mazungumzo na kwamba wameelewana apumzike.
“Nilichukua uamuzi wa kukutana na Dk. Slaa kwa sababu ni kiongozi anayeheshimika na kupendwa, na ameshiriki katika hatua zote na vikao vya ujio wa Lowassa kikiwamo cha Kamati Kuu.
“Tulikubaliana kwa pamoja baada ya kupitia mawasiliano ya kitakwimu, kisayansi na tafiti mbalimbali, kwamba kiongozi huyo (Lowassa) ni mpango wa Mungu, na atatusaidia kuwaunganisha wenzetu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Wakati nimezungumza naye aliomba muda wa kupumzika huku akitoa ruhusa ya chama kuendelea na mipango yake ya kuelekea uchaguzi mkuu, tukatumia usemi unaosema maji yakikupwa na kujaa hayamsubiri mtu, hivyo hatuwezi kumsubiri mtu ili tuendelee.
“Tumekubaliana na Katibu Mkuu, apumzike kwa muda na sisi tuendelee, na pindi atakapokuwa tayari ataungana nasi mbele ya safari. Sisi hatuwezi kuzuia mabadiliko kwa sababu ya Mbowe au Slaa,” alisema Mbowe.

Comments