LOWASSA AREJESHA FOMU YA URAIS KWA KISHINDO WATU MILIONI 1.6 WAMDHAMINI
Dar es Salaam. Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa jana amerejesha fomu ya kuwania urais, huku akifanikiwa kupata wadhamini milioni 1.6, zaidi ya nusu ya kura za urais ambazo chama hicho kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Naibu
katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema idadi hiyo ya
wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa maelezo kuwa inakaribia
idadi ya kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa
alipogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Katika
Uchaguzi huo, Dk Slaa alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura
2,271,941 sawa na asilimia 26.34, huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura
5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Lowassa alipochukua
fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, kabla ya
kuhamia Chadema, alidhaminiwa na wanachama 870,000 nchi nzima.
Dk
Slaa, ambaye hajaonekana hadharani tangu Lowassa ajiunge Chadema, jana
hakuwapo kwenye ofisi za chama hicho wakati mbunge huyo wa Monduli
alipokuwa akirejesha fomu.
Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala lake, lakini baadhi ya maofisa wa Chadema walisema wanaendelea kuchapa kazi.
Kama
ilivyokuwa juzi katika hafla fupi wakati Lowassa akichukua fomu, umati
mkubwa ulifurika na kusababisha Mtaa wa Ufipa uliopo Wilaya ya Kinondoni
kufungwa, watu walijazana tena na safari hii umati huo ukiwa umebeba
mabango ya kumsifu Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Katika
hafla ya jana, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah
Safari alieleza jinsi Chadema ilivyojipanga kuchukua nchi na siyo
kushinda ubunge na udiwani pekee na kwamba Lowassa amebakiza hatua mbili
tu kuingia Ikulu, jambo walilodai kuwa limeichanganya CCM.
Wakati
Lowassa ambaye alitangaza rasmi kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema
Julai 28 mwaka huu akisubiri kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho
utakaofanyika Agosti 4, habari za ndani zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wa
CCM watatambulishwa katika mkutano huo.
Habari hizo
zinaeleza watakaotambulishwa siku hiyo ni wenyeviti wa CCM wa mikoa,
wilaya na waliokuwa wabunge wa chama hicho ambao wanamuunga mkono
Lowassa.
Jana Lowassa, aliyekuwa amevaa shati jeupe na
suruali nyeusi na aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser VX,
alifika makao makuu ya Chadema saa 9:35 alasiri akiwa pamoja na familia
yake na alipokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamebeba mabango
yenye ujumbe mbalimbali.
Baadhi ya ujumbe huo ni “Chini
ya Lowassa umaskini haupo”, “Kwa Lowassa hata maskini atapata ajira” na
“Kingunge Ngombare-Mwiru karibu Ukawa”. Kingunge ni kada mkongwe wa CCM
na anamuunga mkono Lowassa.
Mbali na kubeba mabango,
watu hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu Lowassa na
kushangilia pale ilipokuwa ikitajwa mikakati ya chama hicho kushika
dola.
Kura milioni 1.6
Akieleza
taratibu na kanuni za kudhamini mgombea urais, mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira alisema mgombea
urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama wasiopungua 200.
“Naamini
fomu za Lowassa zitakuwa na idadi hiyo ya wadhamini. Ila baada ya
mgombea kuchukua fomu jioni yake wanachama wa Chadema, wapenzi na
Watanzania walifurika katika ofisi za Kanda, mikoa na majimbo nchi nzima
wakiomba kumdhamini,” alisema Kigaira.
Alisema
wanachama hao walidhani fomu hizo zimepelekwa kila mkoa, kutokana na
kuepuka kuwanyima fursa hiyo chama hicho kilipeleka fomu ili wanachama
wamdhamini na kupewa masharti kuwa lazima wawe wamejiandikisha kupiga
kura, wataje namba zao za simu.
Huku akionyesha fomu
chache za wadhamini kutoka mikoa mbalimbali nchini, Kigaira alitaja
idadi ya watu waliomdhamini Lowassa katika mikoa yote 32 kuwa ni
1,662,397.
Akizungumzia udhamini wa wanachama Mwalimu
alisema: “Lowassa alitakiwa azunguke mikoani kusaka wadhamini ila siku
zilikuwa zimebaki mbili. Tuliwataka wanachama wanaotaka kumdhamini
(Lowassa) wafike makao makuu, siku uliyochukua fomu. Wanachama 700
walikuja kukudhamini.”
Alisema kitendo hicho kiliiibua
malalamiko kutoka kwa wanachama wa mikoa mbalimbali nchini, hivyo
kuagizwa fomu za udhamini zipelekwe mikoani.
Safari ya Lowassa haitavurugwa
Katika
maelezo yake, Mwalimu alisema CCM inafanya vikao ili kuivuruga Chadema,
lakini akasema kuwa hilo halitafanikiwa na hakuna wa kuivuruga safari
ya Lowassa.
“Tunajua kuna mikakati na vikao
vinavyoendelea kwa nia ya kumzuia Lowassa katika safari hii ya Chadema
na Ukawa, lakini tunawaambia Lowassa kuja Chadema ni mpango wa Mungu.
Hatujamuokota barabara, ni Mungu amemuongoza kuja chama chetu kwa sababu
Mungu ameshakiandikia neema chama hiki kutokana na falsafa
inazokisimamia tangu kuanzishwa kwake.”
“Njama zozote
za kishetani, kihafidhina na kifedhuli zitalegea na kupotezwa. Lowassa
amebakiza hatua mbili, ya kwanza ni kumaliza mchakato wa ndani ya chama
kupitia Mkutano Mkuu na hatua ya pili ni kuapishwa.”
Mwalimu
alisema Chadema inaunga mkono kauli ya Lowassa ya kuuchukia umaskini,
kwamba nchi imeshindwa kupata maendeleo kutokana na kuongozwa na
viongozi wa CCM wenye fikra za kimaskini, za kuamini ili uwe kiongozi
lazima uwe maskini.
Alisema baada ya Lowassa kupitishwa
na Mkutano Mkuu chama hicho, atazunguka mikoa mbalimbali nchini kuanzia
Dar es Salaam Agosti 9.
Lengo ni kuchukua nchi
“Kuna
watu walidhani Lowassa hawezi kurejesha fomu. Safari ya kuelekea
uchaguzi mkuu imefikia hatua muhimu. Kinachofuata ni Kamati Kuu
kupitisha fomu hizi. Naamini hakuna pingamizi lolote maana mpaka sasa
hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu za kugombea urais kupitia Chadema na
Ukawa,” alisema Profesa Safari.
Alisema wapo wanaosema
mwaka huu wapinzani wataambulia wabunge na madiwani tu siyo rais, jambo
alilodai kuwa si kweli na kwamba lengo lao ni kushinda kiti cha urais.
“Wazanzibari wana msemo wao kwamba goli unafungwa, lakini chenga twawala. Sisi chenga tutapiga na magoli tutafunga,” alisema.
Vigogo CCM
Habari
za ndani kutoka chama hicho zinaeleza kuwa vigogo wa CCM
watatambulishwa kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho,
wakiwemo wabunge mashuhuri.
“Siku ya mkutano mkuu
watatambulisha wabunge na viongozi wa CCM. Ni wengi na wengine
watawashangaza watu kwa kweli kwa sababu si watu wanaotarajiwa kuihama
CCM, “ alisema mpashaji habari wetu.
Mbunge wa Arumeru
Magharibi, Goodluck Ole Medeye ndiye anayeambatana na Lowassa na
amehudhuria hafla zote za uchukuaji na urejeshaji fomu, mara zote
akiulizwa amekuwa akijibu kuwa ni mshauri wa mbunge huyo wa Monduli wa
masuala ya kupambana na rushwa.
Chizii agoma kuzungumza
Naye
kada mkongwe wa CCM, Matson Chizii ambaye naye amekuwa bega kwa bega na
Lowassa tangu ahamie Chadema, alipoulizwa kama amehamia katika chama
hicho kikuu cha upinzani nchini alisema hana cha kujibu, kusisitiza kuwa
atajibu suala hilo siku mbili zijazo.
Comments
Post a Comment