MAGUFULI na kampeni, utata wa kauli ya MKAPA, Kituo cha Polisi kuchomwa


Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli
HABARILEO
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema katika sehemu kubwa ya kampeni yake, atatumia zaidi usafiri wa barabara ili apate fursa ya kuzijua kwa karibu kero za wananchi katika maeneo mengi ya nchi.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa maeneo mengine yenye ulazima wa kutumia usafiri mbadala, anaweza kufanya hivyo, lakini dhamira yake ni kutumia zaidi barabara.
Aidha, amezitaja sifa ya waziri ajaye wa ujenzi, ambaye atarithi wizara aliyoitumikia kwa miaka 15, iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza tangu kuzinduliwa kwa kampeni za chama hicho katika Kijiji cha Mishamo, kilichopo Kilometa 150 kutoka mkoani Katavi, Dk Magufuli alisema amekataa kutumia helikopta katika baadhi ya sehemu atakazofanya ziara, ili kujionea mwenyewe kero ya barabara inayowakabili Watanzania.
Moja ya barabara alizoahidi kujenga ni pamoja na kutoka Tabora mpaka Mpanda, ambayo ina kilometa zaidi ya 356 na ya Mpanda mpaka Uvinza yenye urefu wa karibu kilometa 190.
Ataka mchapakazi ujenzi Kwa mujibu wa Magufuli ambaye amejipatia sifa ya uchapakazi katika wizara hiyo, kazi ya kwanza atakayofanya atakapochaguliwa kuwa rais, ni kuteua Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Katiba.
Amesema kutokana na kazi kubwa ya ujenzi wa barabara iliyopo mbele yake, Waziri ajaye wa Ujenzi ni lazima awe na uwezo wa kuchapa kazi kuliko yeye, na kuongeza kuwa atamsimamia yeye mwenyewe kuhakikisha anatekeleza majukumu hayo.
Akizungumza kijijini Mishamo, Magufuli pia aliwahakikishia wananchi wa maeneo hayo, ambao baadhi yao waliokuwa wakimbizi waliotoka Burundi wakati wa machafuko ya mauaji ya kimbari, lakini wakapewa uraia wa Tanzania, kwamba uongozi wake utaheshimu na utawatambua kuwa wao ni Watanzania.
Huku akizungumza lugha mbalimbali ikiwemo Kiha, Kifipa na Kirundi, Magufuli pia aliahidi kujenga shule katika kata ambazo zimegawanywa na kujikuta zikitegemea shule moja ya sekondari, kutatua kero ya maji na umeme.
Magufuli alisema waziri atakayemteua wa umeme, akishindwa kupeleka umeme Mpanda, atoke mwenyewe huku akisema atakuwa rais wa wanaChadema, wana ACT, wana CUF na wasio na chama kwa kuwa maendeleo hayana chama.
Kuhusu reli, alisema atajenga reli ya kisasa na uwezo wa kufanya hivyo anao, ikiwemo katika kuzuia mafisadi wasitumie fedha za umma kwa kuunda Mahakama ya Maalumu ya Kushughulikia Rushwa.
HABARILEO
Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), kimeomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuandaa karatasi maalumu za kupigia kura kwa wasioona ili kuondoa uwezekano wa mtu aliyeteuliwa kupiga kura kwa niaba ya asiyeona kumrubuni.
Mwenyekiti wa TLB, Luis Benedicto alisema, kura ni siri ya mtu na ni haki ya kila mtu kupiga kura kumchagua kiongozi amtakaye.
Alisema katika chaguzi za nyuma walikuwa wanalazimika kuwa na watu wa kuwasaidia lakini hawana imani ya asilimia 100 na watu hao kwani wanaweza kuwadanganya na hivyo kuchagua kiongozi wanayemtaka.
“Naweza nikamwamini mtu lakini pia anaweza kunidanganya. Mimi sioni na yeye anaona hivyo anaweza kunidanganya kuwa amemchagua mtu niliyemtaka mwisho wa siku unakuta kadanganya na kumchagua mtu tofauti,”  Benedicto.
Aliongeza kuwa zipo changamoto mbalimbali walizokutana nazo kipindi cha kujiandikisha katika daftari la kupiga kura ambazo wasingependa kukutana nazo siku ya kupiga kura.
“Tume inapaswa kutumia muda huu kuhakikisha wanashughulikia changamoto hizo ili zisitokee tena. Tulisumbuka sana sababu ya kutoona kwetu. Hatupendi yatokee tena, watumie muda huu kutuandalia mazingira rafiki,” alisema.
Aidha alisema katika mipango ya NEC ya sasa, inapaswa kuona umuhimu wa kuweka wawakilishi wa walemavu wa aina mbalimbali ili kuondoa mkanganyiko uliopo kuhusu haki na fursa zao.
Pia alisema Tume ya Taifa ya uchaguzi inatakiwa kutoa elimu ya uraia, vifaa vya kupigia kura na miundombinu itakayowawezesha wao kufika kwa uraisi katika vituo vya kupigia kura. “Tumezungumza mara nyingi sana juu ya suala hili, lakini mpaka sasa hatujapatiwa majibu. Tuko njiapanda, hatujui itakuwaje,” Benedicto.
HABARILEO
Mkazi  wa Tabata Msimbazi, Dar es Salaam, Goodluck Aloyce wiki hii ameanza kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kumlawiti shemeji yake mwenye umri wa miaka 11 mara kwa mara.
Akisoma hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan alisema, mashahidi sita walioletwa na upande wa mashitaka waliisaidia mahakama kuthibitisha kwamba mshitakiwa alimbaka na kumlawiti mtoto huyo.
Pia alisema ripoti kutoka kwa daktari (PF3) iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo, ilionesha kuwa mtoto huyo alikuwa akiingiliwa kimwili mara kwa mara na mshitakiwa.
“Mahakama inakutia hatiani kwa mashitaka mawili uliyoshitakiwa nayo. Kila kosa utatumikia kifungo cha miaka 30 hivyo kwa mashitaka yote utatumikia kifungo cha miaka 60 jela (isiyoenda kwa pamoja). Kama hujaridhika (na hukumu hii) ana haki ya kukata rufaa,’’ alisema hakimu.
Kabla ya kusomewa adhabu, Wakili wa Serikali, Felista Mosha aliitaka mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili liwe fundisho kwa wengine wanaofanya vitendo hivyo. Lakini mshitakiwa aliiomba mahakama hiyo imwachie awe huru, ombi ambalo halikutiliwa maanani na mahakama hiyo.
“Kitendo ulichokifanya kinapaswa kupingwa kwa hali zote kwa kuwa mtoto huyu alihitaji ulinzi wa kutosha kutoka kwako,” Hakimu Hassan.
Katika kesi hiyo, mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka mawili ya kubaka na kulawiti mtoto huyo mwenye umri wa miaka 11 kinyume na sheria.
HABARILEO
Polisi mkoani Morogoro wanashikilia watu 11, wakazi wa Kijiji cha Mpofu wilayani Kilombero kwa tuhuma za kuvamia na kuchoma moto kituo kidogo cha polisi na ofisi ya serikali ya kijiji hicho.
Watuhumiwa hao ni sehemu ya zaidi ya watu 100 wanaodaiwa kufanya uhalifu huo katika kituo hicho cha polisi Mbingu, katika taarifa ya Mgeta.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya tukio hilo wakishinikiza polisi wamwachie mtuhumiwa aliyewekwa mahabusu katika kituo hicho, Bashiri Kadugula , kwa tuhuma za kumshambulia mkewe, Veronica Chabula ili wamwadhibu.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema jana kuwa, Kadugula aliwekwa ndani kwa kumkata mkewe kwa panga sehemu mbalimbali za mwili kutokana na wivu wa mapenzi.
Alisema katika tukio hilo ni la Agosti 20, mwaka huu saa 4:00 usiku, mtuhumiwa huyo baada ya kufanya kitendo hicho kwa mkewe akitoroka na ndugu wa Veronica walifanikiwa kumkamata na kumfikisha kituo kidogo cha Polisi Mb ingu, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Alisema baada ya ndugu kuondoka kituo cha polisi, kitambo kidogo kulitokea kundi la watu wakirusha mawe kituoni hapo, wakitaka wamuue mtuhumiwa huyo kwa kukerwa na kitendo chake cha kinyama.
Kamanda Paulo alisema, askari waliokuwepo kituoni hapo walijitahidi kuwazuia watu hao lakini walizidiwa nguvu.
Alisema polisi walifanikiwa kumtoa mtuhumiwa mahabusu na kumwokoa sambamba na kuokoa silaha za kituo hicho.
Alisema, watu hao waliokadiriwa kuwa zaidi ya 100, walivamia kituo hicho kidogo cha Polisi na kukichoma moto ambapo nyaraka mbalimbali zilizokuwa ndani ya kituo hicho ziliungua na kuteketea kabisa.
Alisema, kundi la watu hao baada ya kukichoma moto kituo kidogo cha polisi, lilivamia pia Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Mpofu na kisha kuchoma moto nyaraka mbalimbali, ambapo katika matukio hayo watuhumiwa 11 walikamatwa.
Kamanda huyo wa Polisi wa mkoa alisema kwamba watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika na kwamba polisi wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine waliotoroka na kusisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutii sheria na kuacha kujichukulia sheria mkononi.
NIPASHE
Nchi za Afrika Mashariki na kati ikiwamo Tanzania zipo katika wasiwasi wa kukumbwa na mvua za El-nino kutokana na kuongezeka kwa joto katika Bahari ya Pacific.
Akizungumza kwenye mkutano wa 41 wa masuala ya hali ya hewa na utabiri unaofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dk. Agness Kijazi , alisema kitaalam kuna uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa katika nchi za Afrika Mashariki katika kipindi cha Septemba mpaka Desemba, mwaka huu.
Alisema  mkutano huo unawahusisha wataalam mbalimbali kutoka katika nchi 11 na unaangalia mifumo ya hali ya hewa kwa Afrika Mashariki na tayari wameona viashiria vya kutokea kwa mvua hizo.
“Mvua hizo hutokea pale kiwango cha joto kinapoongezeka kwa kiasi kikubwa kwenye bahari na mpaka sasa tumeona joto limeongezeka kwa kiasi kikubwa katika bahari ya Pacific,”Kijazi.
Alisema baada ya kuangalia mifumo ya hali ya hewa katika eneo la Afrika Mashariki, wataalamu watarudi katika nchi zao na kuangalia mifumo ya hali ya hewa katika maeneo yao na kutoa utabiri kwa wananchi husika kwa kipindi Septemba mpaka Desemba.
“Hapa kwetu Tanzania tutatoa utabiri wa mvua kwa miezi mitatu yaani Septemba mpaka Desemaba ifikapo Septemba Mosi mwaka huu,” aliongezea kusema.
Kijazi alitoa wito kwa wananchi na wadau wa hali ya hewa kufuatilia utabiri utakaotolewa Septemba Mosi, mwaka huu ili kujua hali itakavyokuwa.
NIPASHE
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amefungua pazia la kampeni mikoani huku akisema kipaumbele chake kikubwa ni huduma muhimu zikiwamo barabara za lami.
Dk. Magufuli aliyeanza kampeni zake juzi jijini Dar es Salaam, jana alianza kampeni zake katika kambi ya Mishamo iliyokuwa ya wakimbizi wa Burundi kmkoani Katavi.
Dk. Magufuli pia ameahidi huduma muhimu za jamii kwa wakazi wa mkoa huo zikiwamo za elimu, afya na umeme.
Alisema kuwa Waziri wake wa Ujenzi, atakuwa na kibarua kikubwa kwani atatakiwa kufanya kazi zaidi yake.
Akiwa mjini Mpanda katika viwanja vya Azimio, Dk. Magufuli alisema serikali yake haitakuwa na shida ya fedha kwa kuwa kwa sasa zinachotwa na mafisadi, lakini akiwa rais, wote watakuwa wamekamatwa na kufungwa na kuwaacha wananchi kufurahia maendeleo.
Aidha, alisema Waziri wa Nishati na Madini atakayemteua kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha umeme wa uhakika mkoani humo na iwapo atashidwa atamuondoa.
“Nitaunda Baraza la Mawaziri la kuwahudumia wananchi ili Tanzania yenye neema na maendeleo makubwa ipatikane, mimi ni mkali ila kwa Mawaziri nitakuwa mpole ili wafanye kazi kwa kasi,”  alisema.
Dk. Magufuli ambaye msafara wake ulimjuisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiwa katika vijiji vya Majalila, Vikonge na Luhafwe, alisema akiwa Rais, atahakikisha barabara ya Mpanda hadi Uvinza yenye urefu wa kilomita 194, inajengwa kwa kiwango cha lami na kwa kuanzia zitajegwa kilomita 30.
“Nawahakikishia nikiwa rais, barabara hii itawekwa lami, umpembuzi yakinifu, michoro imekamilika kilichobaki ni kutengeneza. Sisemi uongo bali kweli tupu na msema kweli ni mpenzi wa Mungu, naongea haya jua linawaka,” alisisitiza Dk. Magufuli.
Alisema katika kijiji cha Vikonge na Luhafwe, atawapelekea majisafi na salama, umeme na zahanati na malengo ni kuhakikisha kila kijiji na kata kunakuwa na zahanati na hospitali.
Alisema maendeleo hayana chama, kabila, dini bali kinachotakiwa ni maendeleo na yeye ndiye mtu wa kuyaleta maendeleo hayo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Ifumbura, Dk. Magufuli alisema anatambua mahitaji ya wananchi hao kuwa ni maji, umeme na barabara kuu ya Mpanda hadi Uvinza na kutoka eneo hilo hadi Ziwa Tanganyika.
“Nawaahidi jua likiwa linawaka, sitawaangusha nitaleta barabara ya lami, nipigieni kura mimi (Magufuli) na wagombea ubunge na udiwani wa CCM…nimeambiwa eneo lenu lina shule moja ya sekondari, tutajenga nyingine pamoja na nyumba za walimu,” alisema na kuongeza:
“Mnachotakiwa ni kunipa kura zenu, maji, umeme, zahanati, vituo vya afya na hospitali mtapata, wakulima kukopwa mazao yao itakuwa ndoto, itakuwa ni pesa kwa pesa, ukienda sokoni urudi na hela yako nyumbani.”
Pia aliahidi umeme,maji shule na zahabati katika eneo hilo.
Wakati Dk. Magufuli akijinadi hivyo mkoani Katavi, Mgombea Mwenza wake, Samia Suluhu Hassan, yuko mkoani Kilimanjaro ambako ameahidi kutatua migogoro ya ardhi, kuleta huduma bora za afya, maji na kugawa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji fedha hizo ziwasaidie wanawake na vijana.
MTANZANIA
Wakati mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, akizindua kampeni zake juzi jijini Dar es Salaam kwa mkutano wa hadhara, mpinzani wake mkubwa ambaye ni mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, ameanza kwa mtindo wa aina yake wa kuwafuata wananchi mitaani.
Katika hali ambayo haijazoeleka katika siasa za Tanzania, jana Lowassa alifika kwenye kituo cha daladala kilichopo eneo la Gongo la Mboto, Ilala jijini Dar es Salaam saa 1:50 asubuhi, na kusalimia wasafiri na wafanyabiashara mbalimbali wanaofanya shughuli zao eneo hilo.
Takribani dakika 21 ambazo Lowassa alizitumia kwenye eneo hilo, zilitosha kujaza mamia ya wananchi kila mmoja akitaka kumsalimia.
Lowassa anayewania nafasi hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), aliwasili kituoni hapo akiwa na gari aina ya Noah yenye namba T 607 DDR.
Mara baada ya gari hilo kusimama kituoni hapo na Lowassa kushuka, baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walionekana kupata mshangao kutokana na ziara hiyo ya kushtukiza, wakiwa hawaamini wanachokiona, huku wengine wakishangilia.
Muda mfupi baada ya Lowassa kufika akiwa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji, baadhi ya watu waliacha shughuli zao na kufurika kwenye eneo hilo.
Kwa madereva wa bodaboda na daladala, walisitisha shughuli zao na kusogea eneo hilo huku wakishangilia kwa kusema ‘rais… rais… Lowassa… Lowasssa’ na kupiga miluzi.
Kadiri Lowassa alivyokaa kwenye eneo hilo, watu waliendelea kufurika huku baadhi yao wakisema tangu taifa hili lipate uhuru, hawajawahi kushuhudia kiongozi mkubwa akiwatembelea kwenye maeneo yao.
“Hata waziri mwenyewe hajawahi kuja huku,” alisikika mmoja wa wananchi wa eneo hilo akisema na kuongeza: “Baba wewe ndiye unafaa, na miaka yote tulikuwa tunamhitaji mtu wa aina yako.”
Pia baadhi ya wananchi walisikika wakimweleza kwamba akifanikiwa kuwa rais, wanaitaka Katiba ya Jaji Joseph Warioba.
Katika hali ya kushangaza, mwanafunzi mmoja aliibuka na kumfuata Lowassa, huku akimwambia kuwa anacho kichinjio – kitambulisho cha kupigia kura.
Ilipotimia saa 2:11 asubuhi, Lowassa alipanda daladala yenye namba za usajili T 917 CWS inayofanya safari zake kati ya Buguruni na Nzasa na kwenda nayo hadi eneo la Pugu Shule ambako alifika saa 2:24 asubuhi.
Wakati anapanda ndani ya daladala hiyo, wananchi walijazana eneo hilo walizidi kupatwa na mshangao, wengine wakisema hawaamini wanachokishuhudia.
Kitendo hicho kilisababisha baadhi wa wananchi kuvamia daladala hiyo na kupanda, huku wengine wakipitia madirishani kutokana na msongamano wa kugombania ulivyokuwa mlangoni.
Wananchi hao walijaa kwenye daladala hiyo hadi wengine wakaning’inia mlangoni na kisha kuanza safari yake kuelekea Pugu.
Kitendo cha daladala hiyo kuondoka eneo hilo, vijana waendesha bodaboda walianza kuifuata kwa nyuma na  wengine wakitangulia mbele yake.
Baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye kituo hicho, nao waliifuata daladala hiyo wakikimbia hadi Pugu, takribani umbali wa mita 400.
Akiwa ndani ya daladala hiyo, Lowassa aliyekuwa ameketi kiti kimoja na mwanafunzi, alitoa Sh 2,000 kwa ajili ya nauli yake na abiria waliokuwa karibu naye.
Baada ya kufika katika eneo hilo la Pugu Shule, Lowassa alishuka na kupanda kwenye gari lake ambapo msafara uliendelea hadi Mbagala Rangi Tatu.
Dereva wa daladala hiyo, Steven Zunga, alisema amefurahi sana kwa kitendo cha mgombea huyo wa Ukawa kupanda gari lake.
“Furaha niliyonayo siwezi kuelezea, nimefurahi sana… sijui kama leo nitalala, sikutegemea kama siku moja ningemwendesha Edward Ngoyai Lowassa. Imeingia katika historia yangu na nitaiandika kwenye kumbukumbu zangu,” alisema dereva huyo.
MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli ameanza rasmi kampeni akiwa Mkoa wa Katavi na kuahidi kuacha kuwakopa wakulima mazao akisema atatumia mtindo wa “pesa kwa pesa”.
Mgombea huyo aliwasili Mpanda saa 4.10 asubuhi na kuanza safari ya kuelekea Mishomo ambako aliahidi kuboresha huduma za barabara, umeme, maji, elimu na kukomesha kitendo cha Serikali kuwakopa wakulima mazao yao.
“Suala la Serikali kuwakopa wananchi mazao yao katika Serikali ya awamu ya tano nitalikomesha, itakuwa pesa kwa pesa. Nafahamu mnalima sana tumbaku, hivyo nitahakikisha mazao yenu mnapopeleka sokoni kama ni tumbaku lazima upate fedha zako,” alisema.
Alisema akipatiwa ridhaa ya kuwa rais, atajenga barabara za Mpanda hadi mpakani  mwa Uvinza, Mpanda hadi Tabora na Mpanda-Kanoge-Ukala kwa kiwango cha lami.
“Tukitengeneza barabara, vijana na kina mama watapata ajira, wawekezaji wataanzisha viwanda ama vya karanga au tumbaku,” alisema.
Alisema akichaguliwa ataunda baraza la mawaziri la kuwahudumia wanyonge atakalosimamia kikamilifu.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Mpanda katika Viwanja vya Azimio, Dk Magufuli alisema: “Nitakuwa rais mkali kweli kwa baraza langu. Nataka baraza nitakalolichagua liwe kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hasa wanyonge. Nataka Tanzania yenye neema, Tanzania yenye maendeleo, nataka Tanzania itakayotoa ajira kwa Watanzania wote. Mimi siyo mkali sana lakini nikichaguliwa nitakuwa mkali sana kwa mawaziri ili niwafukuze harakaharaka,” alisema na kushangiliwa.
Akiwa katika Kijiji cha Majalila aliposimama kwa muda, alisema Serikali imeshafanya usanifu na upembuzi yakinifu wa Barabara ya Mpanda-Uvinza yenye urefu wa kilomita 194 lakini itaanza na kilomita 30 na kumalizia zilizobaki.
Alisema anataka Waziri wa Ujenzi atakayemteua afanye kazi kuliko yeye.
MWANANCHI
Siku moja baada ya ufunguzi wa kampeni za CCM, wasomi na wananchi wamesema kauli ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa wanaosema wanataka kuikomboa Tanzania ni “wapumbavu na malofa” haikustahili kutolewa na kiongozi huyo.
Katika ufunguzi huo, Mkapa alisema wapinzani wanaodai  vyama vyao ni vya ukombozi ni wapumbavu na malofa kwa  kuwa Watanzania walikwishakombolewa na ASP na Tanu na kwamba chama pekee cha ukombozi kilichobaki sasa ni CCM.
Profesa wa Uchumi katika Kilimo wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Damian Gabagambi alisema kauli kama hizo zinatokana na mabadiliko yanayoonekana kwenye siasa za Tanzania yanayosababishwa na kutimia kwa unabii wa Mwalimu Julius Nyerere kuwa ‘mpinzani wa kweli atatoka ndani ya CCM.’
Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi wakubwa wa CCM hawajiamini, wanalazimika kutumia lugha zisizo na staha kupunguza msongo walionao.
“Kuhama kwa viongozi waandamizi kunawaumiza kichwa na huenda hawajui sababu. Wameanza kampeni na matusi na pia, wamechelewa kumaliza mkutano, kwa hali hii watatoa wapi nguvu ya kuwakemea wengine?” Profesa Gabagambi.
Alishangazwa na kitendo cha polisi kuendelea kutoa ulinzi bila ya kukemea baada ya ufunguzi huo kupitiliza muda wa saa 12.00 unaoruhusiwa na akaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa kauli juu ya suala hilo.
“Walipoteza muda mwingi kwa burudani za wasanii, nilitarajia wangetumia muda ule kutueleza wamefanya nini kwa muda waliokuwapo madarakani na kufafanua walivyotekeleza ilani iliyopita. Kwa mgeni angeweza kudhani kuwa lilikuwa tamasha la burudani,” alisema.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alipoulizwa alisema: “Suala la muda limeainishwa kwenye kanuni, navikumbusha vyama vyote vya siasa kuzingatia maadili ya uchaguzi kwa kipindi chote cha kampeni. Mwisho wa kampeni ni saa 12.00 jioni na hili linapaswa kufuatwa na vyama vyote.”
Jaji Lubuva alisema vyama vyote vinatakiwa kuzingatia maadili waliyosaini na kuzungumza mambo yanayohusu sera na ilani zao badala ya kushambuliana na kutoleana maneno ya kuudhi majukwaani.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa alisema: “Nyie Mwananchi mkoje? Shughuli imeandaliwa na CCM, halafu mnataka CCM watoe maoni, inawezekanaje?
Hata alipofafanuliwa kuwa kauli za viongozi hao zimehojiwa na watu mbalimbali alisema, “basi endeleeni na hao.”
Wakati Nape akisema hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Allan Simba alisema kauli hizo ni za woga na zinataka kuwatisha wananchi ili wasiwachague wapinzani.

Comments