MAUZAUZA KURA ZA MAONI CCM
Dar es Salaam. Mauzauza jana yalitawala mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kupata wagombea ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM kutokana na kuwapo kwa vitendo vya rushwa, vurugu, kura kuchomwa moto, makada kukamatwa, wanachama kutoruhusiwa kupiga kura na kugundulika kwa karatsi zilizokwishapigwa kura.
Kwenye
baadhi ya maeneo kazi hiyo iliahirishwa hadi leo kutokana na vifaa
kuchelewa na pia tatizo la kugundulika kwa shahada ambazo zimeshapigwa
kura zikiwa ndani ya maboksi.
Lakini matukio
yaliyotawala kura za maoni ni makada kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha
na vitendo vya rushwa kwa kugawa fedha au kuchapisha karatasi bandia za
kupigia kura.
Dar es Salaam
Wilayani
Kinondoni jijini Dar es Salaam, Takukuru inawashikilia wagombea sita
kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe ili wachaguliwe kwenye kura za
maoni.
Makamu mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni,
Denis Manumbu aliwataja waliokamatwa kuwa ni katibu wa kata ya Kibamba,
Denisi Kalela, katibu wa itikadi, Babu Kimanyo, diwani wa viti maalumu
wa Goba, Rehema Luhanja,
Wengine ni mwenyekiti kata ya
Goba, Pili Mustafa, mgombea udiwani, Msigani Mwasha na Eliasi Nawera
ambaye anagombea ubunge Jimbo la Kawe.
Alisema kuwa
Kalela, na Kimanyo walikamatwa juzi saa 4:00 usiku maeneo ya Kibamba
CCM, huku Mustafa na Luhanja wakikamatwa maeneo ya Goba Kati na Kawe.
“Walikamatwa
wakiwa wanatoa rushwa na wengine walikamatwa wakiwa na kiasi cha pesa
ambazo bado walikuwa wanazigawa huku wengine wakiwashawishi wajumbe
kupokea rushwa,” alieleza Manumbu.
Manumbu alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi ofisi yao inafanya kazi saa 24 ikipokea taarifa zote zinazohusu rushwa.
Kondoa
Lakini
hali ilikuwa mbaya wilayani Kondoa, Dodoma ambako CCM ililazimika
kuchoma moto makasha sita ya kupigia kura baada ya kubainika kuwa baadhi
ya wanachama walitumia kadi ya CCM pekee bila ya kitambulisho cha
kupigia kura.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Shaaban Kissu,
mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Othman Gora na kamanda wa polisi wa wilaya,
Nyantora walikubaliana kuchomwa moto baada ya kubaini tatizo hilo.
Hatua
hiyo, inatokana na wanachama kuanzisha zogo kuwa vitambulisho vya kura
havikutumika kabla ya uamuzi huo kufikiwa. Tayari zaidi ya wanachama 200
walikuwa wamepiga kura hizo.
Maboksi hayo yalichomwa
mbele ya kituo cha kupigia kura cha Ubembeni na kushuhudiwa na wananchi,
wananchama wa CCM, polisi na uongozi wa CCM.
Baada ya kuyachoma, Kissu alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya dosari hiyo na kwamba utarudiwa leo.
Baadaye kamanda wa polisi wa wilaya aliamrisha watu wote kutawanyika eneo hilo hadi leo.
Awali
kulitokea vurugu baada ya baadhi ya wanachama kunyakua sanduku
lililokuwa na kura na kutaka kukimbia nalo kwa tuhuma kuwa mawakala
hawakuwa wakitenda haki kwa wapiga kura
Mbeya
Kashfa
ya matumizi ya rushwa pia ilijitokeza mkoani Mbeya ambako mgombea
udiwani mmoja kulalamikiwa kwa madai ya kuwakodisha wanafunzi wampigie
kura kwa malipo ya Sh2,000 kwa kila mmoja.
Mgombea huyo
wa udiwani wa Kata ya Mbalizi Road analalamikiwa pia alikwenda kwenye
kilabu za pombe kuwatafuta watu wanaotaka kumpigia kura ili awanunulie
kinywaji.
Miongoni mwa walalamikaji ni Ally Salum na
Aziza Mbika wa eneo la Sabasaba ambao walisema walimwona mgombea huyo
akitoa fedha na pombe kwa vijana mbalimbali .
Msimamizi
wa uchaguzi wa Kituo cha Meta, Ndoni Mwakalukwa alikiri kupokea
malalamiko ingawa hakushuhudia utoaji wa fedha hizo na kwamba
atayazungumza baada ya kumaliza kazi ya upigaji kura.
Vituo
vingine, vikiwamo vya Kata za Ruanda na Sinde, vilikosa wanachama wa
kupiga kura na badala yake walifika mmoja mmoja kila baada ya saa
kupita.
Wasimamizi wa uchaguzi maeneo hayo walikuwa na
kazi ngumu ya kuwaita watu waliokuwa wakipita wakiwaomba wakapige kura
kama ni wanachama wa CCM.
“Tatizo ni kwamba vituo vya
kupigia kura havijawekewa alama yoyote, hivyo wanachama wengi hawajui,’’
alisema msimamizi wa kituo cha Soweto, Ambakisye Kitunga.
Lindi
Rushwa
pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Mchinga (CCM) ambako mbunge wa viti
maalumu, Fatuma Mikidadi alikamatwa na Takukuru kwa tuhuma za kutoa
rushwa kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo waliomkamata kwa tuhuma za hongo.
Habari zinasema kuwa mgombea huyo alikutwa na wafanyakazi wa Takukuru akitoa rushwa kwa wanachama wa Kata ya Mchinga.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mikidadi alikasirika akisema: “Uongo, uongo, huu ni uzushi kabisa.”
Alipoulizwa
kwa nini anafikiri wamemsingizia, alisema: “sijui hawa wanasingizia
singizia tu, uongo.” Hata hivyo, kamanda wa Takukuru wa mkoa wa Lindi,
Steven Chami alisema Fatuma alikamatwa saa 5:00 usiku Kata ya Mchinga
akigawa fedha kwa wanachama.
Chami alisema akiwa ofisi
za Takukuru baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo alitoa tena Sh780,000 kwa
ajili ya kuwahonga maofisa hao ili wasiendelee na suala hilo.
Alisema
kutokana na kitendo hicho, Takukuru itamfikisha mahakamani muda wowote
baada ya mwanasheria kutafsiri na kubainisha tuhuma zake.
Wakati
huohuo, kamanda huyo alisema mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini,
Mohamedi Utali alishikiliwa kwa muda wa saa kadha kwa mahojiano na
Takukuru baada ya kukutwa na Sh4milioni saa 8:30 usiku akiwa Kata ya
Mbanja.
Chami alisema kukamatwa kwa mgombea huyo kulitokana na ushirikiano baina ya wananchi na taasisi hiyo.
Shinyanga
Mjini
Shinyanga, katibu wa Kata ya Mjini Shinyanga, Ramadhani Majani
amenusurika kipigo baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa
ofisini kwake na mmoja wa wagombea udiwani na ubunge katika Jimbo la
Shinyanga Mjini.
Mashuhuda wa tukio hilo waliwaeleza
waandishi wa habari jana kwamba Majani alikutwa na kadhia hiyo baada ya
watu waliotilia shaka nyendo zake kwa kitendo chake cha kuongozana na
mmoja wa wagombea nyakati za usiku kuingia ofisini na hivyo kuhisi kuna
jambo lisilokuwa la kawaida walilopanga kufanya.
Walisema
waliamua kuwapigia simu wagombea wengine waliokwenda ofisi hizo na
kumkuta mgombea mmoja (jina limehifadhiwa) akiwa anaongea naye, hata
hivyo walishituka ghafla baada ya kuona kundi la wana-CCM wakijongea
ofisini hapo.
“Sisi tulipigiwa simu usiku saa 4:45 na
baadhi ya watu wanaoishi jirani na ofisi yetu ya kata kwamba wamemuona
katibu kata wetu akiwa na mgombea udiwani pamoja na wapambe wake.
Walidai inavyoelekea walikuwa wakipanga mikakati mibovu ya kutaka kuiba
kura,” alisema Rashidi Abdalah.
“Taarifa hizo
zilitushangaza sana. tuliamua kuchukua gari na kwenda katika eneo la
ofisi na kweli tulimkuta katibu kata akiwa na mgombea (anamtaja jina)
wakiwa nje ya ofisi za CCM wakitaka kuingia ndani, ghafla walipotuona
mgombea na wapambe wake walikimbia na katibu kata aliingia ofisini na
kuufunga mlango,” alieleza aliongeza.
Abdalah alidai
kitendo cha Majani kukimbilia ofisini kilisababisha baadhi ya watu
kushikwa na hasira na kutishia kuvunja mlango ili kumtoa nje na
kumshushia kipigo, lakini mgombea
mwingine alimsihi ajisalimishe na kufanikiwa kutuliza ghasia.
Majani
alikiri kutaka kupigwa na kundi la wana-CCM na kwamba ni kweli muda huo
wa usiku alikuwa ofisini akifanya kazi ya kugonga muhuri kwenye
karatasi za kupigia kura japo hakuweza kufafanua kitendo cha mmoja wa
wagombea kuwa katika maeneo hayo nyakati hizo za usiku.
“Nilikuwa
naendelea na kazi zangu lakini baadaye nilishangaa watu wanakuja na
fimbo wakidai niko na mgombea ilibidi nijifungie ofisini kwangu,”
alisema Majani.
Handeni
Hali
ya sintofahamu ilitanda kwenye tawi la Bomani, Kata ya Vibaoni wakati
zaidi ya wanachama 60 walipogoma kupigia kura wagombea udiwani kwa
maelezo kuwa hawawafahamu kwa kuwa hawakufika eneo hilo kujinadi na
badala yake kuamua kupiga kura ya wagombea ubunge.
Wakizungumza
jana wakati wa kuwasubiri wagombea, wanachama hao walisema kuwa
walikutana kuanzia saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kuwasubiri, lakini
hawakutokea hadi saa 12:00 jioni, kitu ambacho walidai kuwa ni dharau.
Mwenyekiti
wa mtaa wa Bomani, John Mohamed alisema kuwa walikubaliana kukutana na
madiwani hao kwa mara ya kwanza, lakini akidi ya wanachama haikutimia
ikawabidi kuahirisha kikao hicho hadi jana lakini kitu cha ajabu
wagombea hao hawakutokea hadi jioni.
Arusha
Sakata
la karatasi bandia za kupigia kura pia liliibuka mkoani Arusha, ambako
viongozi wawili wa CCM walikamatwa kwa tuhuma hizo. Waliokamatwa ni
katibu wa Kata ya Mjini Kati, Ally Meku na mwenyekiti wa Mtaa wa
Bondeni, Yakub Shaban.
Katibu wa Wilaya ya Arusha,
Feruz Bano alisema: “Ni kweli wamekamatwa, lakini tunafuatilia kujua
kosa lao kwa kuwa hawana ofisi, hivyo walikuwa wanapeleka karatasi hizo
kwenye chumba cha kupigia kura kidogo kidogo,” alisema.
Dodoma
Rafu
iligubika uchaguzi huo mkoani Dodoma ambako baadhi ya wanachama
walikamatwa na shahada bandia, huku vurugu zikiripotiwa maeneo kadhaa.
Waliokamatwa
na tuhuma kuwa walikuwa na shahada bandia ni katibu wa vijana Tawi la
Chang’ombe, Nasra Salum akiwa na shahada 20 za kupigia kura, 20 za
udiwani, Bakari Fundikira (za ubunge), na David Malolle.
Mwingine aliyekamatwa kwa tuhuma hizo ni Faisi Mussa ambaye CCM imeeleza alikutwa na shahada 15 bandia.
Aidha,
baadhi ya kata zilishindwa kufanya uchaguzi kutokana sababu mbalimbali
ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na karatasi za kupigia kura kuwa na makosa.
Miongoni mwa kata zilizoshindwa kufanya uchaguzi huo ni Tambukareli na
Kilimani mjini Dodoma.
Katibu wa CCM wa mkoa, Albert
Mgumba alisema kata ambazo hazijafanya uchaguzi, kazi hiyo itafanyika
leo kabla ya saa 4:00 asubuhi. Kuhusu makada waliokamatwa, katibu huyo
alisema jambo hilo waulizwe makatibu wa wilaya kwa kuwa ndiyo wasimamizi
wa uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, vurugu
zimetokea katika tawi la Mji Mpya lililoko Kata ya Uhuru kutokana na
baadhi ya wanachama kudai kuna mamluki wameingia kupiga kura.
“Asubuhi
walikuja watu kutoka Tawi la Uhuru wakidai kuwa kuna mamluki wanataka
kupiga kura kwenye tawi letu, lakini baada ya viongozi kufika
tulirekebisha na zoezi likaendelea kwa amani na utulivu,” alisema
msimamizi wa kituo hicho, Mariam Jumbe.
Bukoba
Hali
ilikuwa tofauti mkoa Kagera ambako uchaguzi huo majina ya wanachama
waliofariki dunia yalikuwapo kwenye orodha ya wapiga kura Jimbo la
Nkenge huku kukiwa na hofu ya kuanguka kwa vigogo.
Hali
hiyo ilitokea katika vituo vya Mutemba na Igayaza. Hata hivyo, katibu
wa CCM wa Wilaya ya Missenyi, Mwajuma Mboha alisema kujulikana kwa
majina hayo, ni matunda ya uwepo wa mawakala katika uchaguzi huo.
Pia
kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa majina ya baadhi ya watu waliofika
kupigakura. Katika kata hiyo ya Nsunga kulikuwa na watu saba
waliolalamikia kutoorodheshwa.
Mtwara
Kukosekana kwa majina katika orodha ya wapigakura pia ilijitokeza kwenye Manispaa ya Mtwara Mindindani.
Wakiongea
na Mwananchi, Shangani Aisha Ismail na Salima Nassoro wa Tawi la
Vigaeni walisema wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa CCM kuwapa kadi
za chama bila kuweka majina yao katika daftari la wapigakura.
“Sisi
tumepewa kadi tunazo mikononi hatujui kama nyingine zimesajiliwa au la.
Nyingine tumezilipia na majina yetu hayapo. Kuna kadi nyingine za mwaka
2000 hadi mwaka 1950 zipo na majina yao yapo na sisi majina yetu hayapo
kuna nini hapa?” alihoji Aisha
Katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya, Mohamed Watanga alikiri kuwapo na tatizo hilo, akieleza kuwa wanalitafutia ufumbuzi.
Njombe
Pia
mkoani Njombe, wanachama walishindwa kupigakura kutokana na kadi zao za
uanachama kuonekana kuwa zilikatwa baada ya Julai 15, siku ambayo CCM
ilifunga kazi ya kuandikisha wanachama wapya.
Msimamizi
wa uchaguzi wa kituo cha Mpechi, Sarah Nyandoa alisema licha ya
uchaguzi kufanyika kwa amani, alikiri kuwapo kwa wanachama waliokuwa na
kazi walizopata baada ya Julai 15.
“Ni kweli kuna
baadhi ya watu wanakuja na kadi zao zilizochukuliwa baada ya Julai 18,
lakini tumewarudisha baada ya kuwaelimisha wameridhika,” alisema Nyadoa.
Pwani
Mchakato
kura za maoni umeingia dosari katika vituo kadhaa baada ya baadhi ya
wanachama kukatwa majina yao kwenye daftari la orodha ya wanachama wa
chama hicho.
Mbali ya kuwepo majina yaliyokatwa, pia
baadhi ya wanachama walikutwa wakipiga kura kwa kutumia stakabadhi ya
malipo ya wanachama maarufu badala ya kutumia kadi ya uanachama wa CCM.
Kasoro
hizo zilisababisha vurugu kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura mjini
Kibaha na kumlazimu mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid Bundala
kusitisha uchaguzi huo kwenye vituo kadhaa vilivyokua na kasoro.
Bundala
alisema jana mchana kuwa vituo vilivyofutiwa kufanya uchaguzi ni
Morning Star na Machinjioni vilivyoko Kata ya Tangini mjini Kibaha.
Uchaguzi huo utarudiwa leo.
Alipoulizwa sababu za
kuwepo tofauti ya idadi ya majina yaliyomo kwenye daftari la uanachama
na idadi ya wenye kadi za chama eneo hilo, alisema wamebaini kasoro hiyo
imesababishwa na baadhi ya mabalozi kutowasajili kwenye daftari la
chama la wapigakura.
Katika hatua nyingine, baadhi ya
wanachama waliokuwa wakipiga kura Kibaha Mjini wamelalamikia kuwepo rafu
katika mchakato wa upigaji kura wakisema baadhi ya matawi yaliweka
orodha kubwa ya wanachama wanaoruhusiwa kupiga kura ikilinganishwa na
idadi ya awali iliyobandikwa kwenye kuta za ofisi za matawi yao.
Tarime
Mjini
Tarime mkoa wa Mara, uchaguzi ulilazimika kuahirishwa hadi leo baada ya
kukamatwa kwa karatasi bandia za kupigia zilizokuwa zimeshawekewa alama
ya ndiyo kwa wagombea wa ubunge Jimbo la Tarime, na Tarime Mjini.
habari
kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa karatasi hizo zinazoendelea
kukusanywa, zilitengenezwa na mmoja wa viongozi wa wilaya, Bernard
Nyerembe ambaye amekamatwa na kufikishwa Takukuru kwa mahojiano zaidi.
Habari hizo zinasema kuwa karatasi hizo zilikuwa zichanganywe na karatasi halali baada ya wanachama kupiga kura za maoni.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Rashid Bogomba alithibitisha kukamatwa kwa karatasi hizo jana asubuhi.
Alisema
kwa Jimbo la Tarime, kura hizo zimekamatiwa katika vijiji vya Nyamwaga,
Masanga na Nyamongo na kwa Jimbo la Tarime Mjini zimekamatwa Mtaa wa
Bomani, Magena na Romori.
Bogomba alisema kutokana na kukamatwa kwa karatasi hizo, uchaguzi umeahirishwa.
Kamanda
wa polisi wa Tarime/Rorya, Benadict Mambosasa pia alithibitisha
kukamatwa kwa Nyerembe na kwamba amepelekwa Takukuru kuhojiwa. Alisema
Nyerembe alikamatwa akiwa ofisi ya CCM ya wilaya baada ya wanachama
kumtuhumu kuwa alikuwa na karatasi zilizokwishapigwa kura kwa ajili ya
wagombea wawili wa majimbo hayo.
Mwananchi ilipomtafuta
Nyambari Nyangwine anayetetea ubunge wa Tarime, na Waziri Gaudensia
Kabaka (Tarime Mjini) wote wwalikanusha kuhusika na kudai hizo ni njama
zilizopikwa dhidi yao.
Makada wengine wanaowania ubunge
wa Tarime ni Christopher Kangoye ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Arusha,
Nyambari Nyangwine (mbunge), Pius Marwa, John Gimunta, Maseke Muhono,
Lucas Mwita, Paul Matongo na Charles Machage.
Kwa jimbo
jipya la Tarime Mjini wanaogombea ni Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka, Maico Kembaki, Philipo Nyirabu, Jonathani Machango, Ditu Manko
na Brito Burure.
Comments
Post a Comment