MKE WA DK. SLAA AFUNGUKA
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuzungumza na vyombo vya habari na kusema yupo salama, mke wake, Josephine Mushumbusi amekanusha tuhuma zilizozagaa kuwa ndiye aliyemshauri kiongozi huyo wa Chadema kujiuzulu na kumzuia kushiriki vikao muhimu vya chama.
Tetesi hizo zilivuma kwenye
mitandao ya kijamii na vyombo vya habari baada ya Dk Slaa kutoonekana
katika vikao muhimu vya Chadema na Ukawa, kuwa Mushumbusi hakupendezwa
na kitendo cha Lowassa kupitishwa kuwania urais chini ya mwavuli wa
Ukawa na badala yake alitaka Dk Slaa ndiye awe mpeperusha bendera.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo ambazo Mushumbusi amezikanusha, aliamua
alimfungia ndani Dk Slaa kama moja ya mbinu za kumzuia asishiriki
shughuli za kichama, tuhuma ambazo amezikanusha.
“Bosi
wako akija kukuomba ushauri utamsaidia, lakini akija akakuambia
ameshafanya maamuzi unaweza kupingana naye?” alihoji Mushumbusi akianza
kutoa maelezo yake na kuendelea:
“Wakati wa vikao
nilikuwa namwona (Dk Slaa) anachelewa kurudi kila siku, siku moja akaja
akaniambia uamuzi aliouchukua na mimi sikuwa na la kusema, nikachukua
shuka nikajifunika.”
Katika mahojiano yake ya kwanza na
Mwananchi baada ya kuzagaa kwa tetesi hizo, Mushumbusi pia alikana
kumfungia Dk Slaa ndani ya nyumba, akisema wakati maneno hayo yalipokuwa
yanazagaa, alikuwa nje ya nchi na wala hakujua kinachoendelea.
“Mwenyewe
najiuliza nini kinaendelea, siwezi kufanya kitu kama hicho. Nyumba
yangu ina milango miwili, nawezaje kumfungia mtu, tena mwanamume, hata
watoto siwezi kuwafungia. Kuna mambo mengine mwanamke huwezi kuyafanya
kwa mwanamume. Mwanamume ni mwanamume tu,” alisema.
Alisema
viongozi wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanafika
nyumbani kwake na walikutana na Dk Slaa na kuzungumza naye... “Kama
ningekuwa nimemfungia wangezungumza naye vipi?”
Mushumbusi alisema mwanamke anaweza kufanya chochote lakini kuna baadhi ya mambo ambayo mwanamume akiamua ni vigumu kumzuia.
Akifafanua
tuhuma za kumshinikiza Dk Slaa kujiuzulu Chadema, Mushumbusi alisema
kiongozi huyo wa Chadema ana uamuzi wake na yeye ni msaidizi tu ambaye
hana uamuzi wa mwisho kwenye familia.
Hata hivyo,
alisema endapo angeamua kumshawishi, uwezo wa kufanya hivyo anao lakini
yeye ni mwanamke mwadilifu anayependa mafanikio ya mumewe.
“Kwani unanionaje? Mimi ni ‘strong’ (nina nguvu), ningetaka ningefanya hivyo, nisingeshindwa,” alisema.
Pamoja na hayo, Mushumbusi alilalamika kuwa tuhuma hizo dhidi yake zimesababisha asisikilizwe kama ilivyokuwa awali.
Bila
kufafanua kwa undani, alisema kuna kundi linalounda propaganda hizo ili
abadili mtazamo kuhusu mumewe lakini jambo hilo haliwezi kutokea.
“Nilisema
nitampenda kama alivyo, sitajali chochote wala akiwa katika hali gani
au chama gani. Kazi yangu ni kumtia moyo ili kile atakachofanya
kifanikiwe,” alisema.
Auza mkaa
Mbali
na kukanusha vikali tuhuma hizo, Mushumbusi alisema alikwishajitoa
kwenye masuala ya siasa kwa miaka miwili sasa na badala yake ameamua
kufanya biashara ya kuuza mkaa.
“Nimenyamaza kimya,
nimekaa kando ninaendelea na biashara yangu ya kuuza mkaa, nipo mbali na
siasa na sitaki kujua kinachoendelea, kwanza hata mchakato wenyewe
siujui,” alisema.
Aliwashauri wanawake kuacha
kushabikia masuala yanayotokea ndani ya ndoa yake na kuwataka wavae
viatu anavyovivaa na wajue kuwa anapitia wakati mgumu
Comments
Post a Comment