MTIKILA ACHUKUA FOMU YA URAIS
Mwenyekiti wa DP Mchungaji Christopher Mtikila akisaini nyaraka ya tume ya uchaguzi kuthititisha kupokea fomu ya kuwania urais |
Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Christopher Mtikila akigoma kusaini fomu za kugombea urais akitaka ufafanuzi wa mgombea binafsi, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa amekwama kwenye lifti za jengo lililopo katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC) kutokana na kukatika umeme.
Mchungaji Mtikila ambaye aliambatana na
mgombea mwenza Juma Metu Juma, alitaka ufafanuzi wa kutokuruhusiwa
kuwania urais akiwa mgombea binafsi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wakati Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) imeruhusu.
“Siondoki
hapa na wala sitaweza kuchukua hizi fomu hadi mniambie ni wapi nitapata
jibu la tume la kukiuka maagizo ya mahakama ya Afrika.
“Waandishi
embu subirini kwanza mkurugenzi wa uchaguzi aje hapa ilia atoe
ufafanuzi na nyie msikilize mkaandike ukweli kwa sababu hii siyo haki ni
sawa na kudharau mahakama,” alisema.
Baada ya kuzozana
na maofisa waliokuwa wakimkabidhi fomu hizo, walilazimika kumuita
mkurugenzi wa uchaguzi Kailima Ramadhani, ambaye alimwambia kwamba
sheria hairuhusu.
“Sisi tunafuata sheria mwenyekiti
kama hicho kipengele kingekuwapo tungekuruhusu uchukue fomu hizo, lakini
hapa tunabanwa na sheria tunaruhusu kutoa fomu kwa watu wanaotoka
kwenye vyama vyao,” alisema Ramadhani
Alisema ni vizuri
Mtikila angefuatilia kwa makini suala hilo ili sheria ipitishwe kwani
NEC wanachokifanya ni kufuata sheria zilizopo tu na si vinginevyo.
Baada
ya kumaliza maongezi Mtikila aliamua kuweka sahihi na kuchukua fomu
hizo kwa shingo upande huku akisema atakiwakilisha vyema chama chake
hicho.
Juni 13,2013 Mtikila alishinda kesi aliyofungua
AfCHPR, mjini Arusha akidai Tanzania inakiuka demokrasia inapozuia
wagombea binafsi.
Mchungaji Mtikila, ambaye ana
historia ndefu ya kukwaruzana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM),
alifungua shauri mahakama ya Afrika mwaka 2011 baada ya jitihada zake za
kupindua mabadiliko ya kikatiba yaliyofuta ugombea binafsi kugonga
mwamba kwenye mahakama za kitaifa.
Dovutwa
Mwenyekiti wa UPDP Fahmi Dovutwa alikwamba kwenye lifti kwa dakika kumi baada ya jana kuchukua fomu za kuwania urais.
Dovutwa
ambaye alikuwa wa kwanza kufika kuchukua fomu saa tatu asubuhi, akiwa
ameambatana na mgombea mwenza, alisema kwamba kukwama kwake kwenye lifti
ni hujuma iliyofanywa na baadhi ya wagombea wenzake wa urais.
Wakati
huohuo; Mgombea urais kwa tiketi ya TLP Maxmilian Lyimo, ambaye hakuwa
na mgombea mwenza alikuwa wa pili kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya
kuchukua fomu.
Mgombea huyo alifika saa 5:33 asubuhi
baada ya kuchukua fomu alisema kuwa upepo wa Uchaguzi Mkuu unaovuma
mwaka huu, haukuwahi kuvuma wakati mwingine wowote, hivyo inaashiria
kuwa nchi itapata kiongozi asiyetarajiwa na wengi.
“TLP
ni chama kisichochafua amani tangu kuasisiwa kwake, hivyo wananchi
waangalie amani ya nchi kwani ni bora kuliko kitu kingine,”alisema na
kuongeza:
“TLP bado kuna nafasi za uongozi kuanzia kata
hadi za ubunge, wanaoshindwa huko waliko tunawakaribisha kwa ajili ya
kuja kugombea nafasi hizo.”
Comments
Post a Comment