PROFESA LIPUMBA AJIVUA UANYEKITI CUF
Uamuzi wa Profesa Lipumba, mmoja wa
waasisi wanne wa Ukawa-Umoja wa Katiba ya Wananchi unaoundwa na vyama
vinne vya Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD-,unamaanisha anapoteza
wadhifa wake wa mwenyekiti mwenza wa umoja huo ambao umeamua
kushirikiana kwenye Uchaguzi Mkuu kwa kusimamisha mgombea mmoja kuanzia
ngazi ya urais hadi udiwani atakayeungwa mkono na vyama hivyo.
Wengine
walioongoza harakati za kuasisi Ukawa ni Freeman Mbowe, ambaye ni
mwenyekiti wa Chadema, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Emmanuel Makaidi
wa NLD.
Profesa Lipumba, mmoja wa wenyeviti wanne wa
Ukawa walioeleza sababu za kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kwenye umoja huo takribani siku 10 zilizopita, jana alieleza
kuwa ameamua kujivua wadhifa huo kutokana na vyama hivyo kukubali
kupokea watu walioshiriki kukataa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na
wananchi, kitu ambacho kilikuwa msingi wa kuundwa kwa Ukawa.
“Nimejitahidi
sana ndugu zangu kuvumilia, lakini dhamira inanisuta,” alisema Profesa
Lipumba mbele ya waandishi wa habari jana kwenye Hoteli ya Peacock baada
ya mkutano wa juzi aliopanga kufanyia ofisi za CUF kuzuiwa na
wanachama.
“Sisi tumekaa tunaipigia kelele Rasimu ya
Katiba ya (Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph)
Warioba lakini iliyopitishwa ni Katiba Inayopendekezwa sasa tunawachukua
waliopitisha ili waje kuisimamia. Hivi inaingia akilini?”
Comments
Post a Comment