WABUNGE 51 WAANGUKA KURA ZA MAONI
Dar es Salaam. Wakati vyombo vya juu vya baadhi ya vyama vya siasa vikiwa vimeanza hatua za mwisho za kupitisha wagombea wa ubunge na udiwani tayari kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, hadi juzi wabunge 51 walikuwa wameanguka kwenye kura za maoni za ndani ya vyama vyao.
Idadi
hiyo ni takriban asilimia 14 ya wabunge 357 wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, inayojumuisha waliochaguliwa na wananchi na wa viti maalumu,
ambao waliamua kwenda kupambana majimboni.
Miongoni mwa
walioanguka ni mawaziri wa Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, ambao walikuwa wakitetea viti vyao majimboni.
Kati ya wabunge hao walioanguka, wawili wanatoka Chadema, wanne CUF na wengine 45 waliosalia wanatoka CCM.
Matumaini
pekee yaliyosalia kwa wabunge hao ambao baadhi yao wamekata rufaa
kupinga matokeo ya kura za maoni, ni huruma za vikao hivyo ambavyo
vinaweza kubadili matokeo ya baadhi ya majimbo, hasa ambayo taratibu
zilikiukwa na ushahidi wa kuwapo matumizi ya rushwa.
Wakati
wabunge walioanguka Chadema wanasubiri kwa hamu kikao cha Kamati Kuu
kilichoanza juzi kupitia majina hayo, wa CCM wanasubiri mfululizo wa
vikao vinavyoanza leo hadi Agosti 13, wakati mchakato kupitisha wagombea
wa NCCR-Mageuzi bado.
Kwa wabunge wa CUF, hakuna matumaini kutokana na vikao vya juu vya chama hicho kukamilisha kazi yake hivi karibuni.
Mbali
na walioanguka, wabunge waliopita katika kura za maoni lakini vyama
vyao vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), nao watalazimika
kusubiri hadi vyombo hivyo vya mchujo vitakapomaliza kazi, kujua kama
wamepita.
Hiyo inatokana na makubaliano ndani ya umoja huo ya kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Kwa
mujibu wa makubaliano ya vyama hivyo vinne; Chadema, CUF, NLD na NCCR -
Mageuzi- kinachooonekana kina nguvu kwenye jimbo fulani ndicho mgombea
wake ataachiwa kupeperusha bendera ya umoja huo, jambo ambalo vyama
hivyo vilisema vimekamilisha kazi ya mgawanyo kwa asilimia 95.
Wakati
Chadema, CUF, NCCR na NLD wakisubiri utekelezwa wa makubaliano hayo,
wabunge wa CCM watakuwa njiapanda baada ya chama hicho kueleza kuwa
hakitarudia makosa ya mwaka 2010 ya kupingana na maoni ya wanachama kwa
kutengua matokeo ya kura za maoni.
Profesa wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jamidu Katima alisema kuanguka kwa
wabunge hao kunatokana na wengi wao kutoonekana majimboni baada ya
kupewa dhamana ya kuongoza wananchi.
“Kama kiongozi
umepewa dhamana, lakini huonekani jimboni basi ni dhahiri wananchi
watakukataa. Wakikuona unachukua fomu watakushangaa lakini ujue
watakukataa kwa sababu huwatatulii kero zao kama ulivyoahidi awali.”
Profesa
Katima alisema kwa sasa Watanzania wameamka, hivyo ni vigumu
kudanganyika na kwamba kama kiongozi hatumii vyema dhamana aliyopewa,
wananchi watamuacha apumzike kwa amani.
Maoni kama hayo
yalitolewa na mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk Alexander Makulilo ambaye alisema zipo sababu chekwa za
baadhi ya mawaziri kushindwa kwenye kura za maoni, mojawapo ikiwa ni
makundi na kushindwa kutimiza ahadi.
Kujaribu mtu mwingine
Dk
Makulilo alisema ni rahisi kwa wananchi kuacha kumchagua kiongozi baada
ya kuona hajatimiza kile alichoahidi hivyo wakaona wajaribu kiongozi
mwingine pengine atawatatulia kero zao.
Kuhusu kuanguka
kwa wanasiasa nguli wa CCM, mhadhiri huyo alisema sababu nyingine ni
siasa za makundi ambako kundi moja tu linaweza kufanya juhudi ili
mwingine ashindwe.
“Sasa hivi tunazungumzia mtu
kuanguka katika chama chake, kwa hiyo siasa za makundi ndani ya chama
hicho inaweza kusababisha kuanguka katika kura za maoni,” alisema.
Sababu
nyingine aliyoitaja Dk Makulilo ni wimbi la vijana na kuwa inawezekana
wananchi wanahamia kwa wanasiasa vijana zaidi baada ya kuona wengine
amekaa madarakani kwa muda mrefu.
Pia, aliitaja rushwa
kuwa miongoni mwa sababu za kuanguka kwani inawezekana kuwa mgombea
mwenzake ametoa fedha au yeye ametoa, lakini mwingine ametoa nyingi
zaidi.
“Nadhani umeona jinsi ambavyo Takukuru
wamekamata wagombea wengi kwa tuhuma za rushwa kwa hiyo hapana shaka
kuwa suala la rushwa lilikuwepo,” alisema.
Utafiti wa Twaweza
Idadi
ya wagombea hao walioanguka katika hatua ya awali inaashiria kuanza
kutimia kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza mwishoni
mwa mwaka jana ambao ulionyesha kuwa nusu ya wabunge wataanguka kwenye
kura za maoni.
Comments
Post a Comment