WATATU WA CHUKUA FOMU ZA URAIS

Moja kati ya watangania wa kuwania urais kwa chama cha UPDP anaejulikana kwa jina la FAHMI DOVUTWA

WAGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka vyama vitatu vya siasa nchini, wamechukua fomu za kuwania nafasi hiyo, huku wakikirushia Chama Cha Mapinduzi (CCM) tuhuma kutokana na changamoto mbalimbali za nchi. Wagombea hao walichukua fomu hizo kutoka Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dar es Salaam jana.

Aidha, mgombea wa UPDP, Dovutwa Dovutwa alikwama kwenye lifti ya jengo zilipo ofisi hizo za NEC, kwa dakika 10 wakati akishuka kutoka kuchukua fomu ya kugombea urais.
Dovutwa anayeelezwa kukwama kwenye lifti hiyo kutokana na kukatika kwa umeme, aliishutumu CCM kwa kukwama kwake akisema kuwa, ndicho kilichosababisha afikwe na kadhia hiyo.
“Tatizo si umeme bali ni CCM, hawa ndio wanaotufikisha hapa. Lakini, tumejizatiti ili watanzania wasikilize sera zetu. UPDP inawahakikishia kuwa tutazitekeleza sera zetu na kuondokana na matatizo kama haya,” alisema.
Baada ya muda huo, Dovutwa alifanikiwa kutoka ndani ya lifti na kushuka chini ya jengo hilo, kwa kutumia ngazi. Alipofika katika eneo walipokuwa wanahabari, mgombea huyo aliwaeleza kuhusu kukwama kwake kwenye lifti na kueleza kuwa ilikuwa ni kwa sababu ya CCM.
Akizungumzia wagombea kutoka vyama vilivyokwisha teua watakaovipeperushia bendera kugombea urais, Dovutwa alisema,” Siwaogopi kwa sababu wote wawili wanaovuma kwa sasa; Dk John Magufuli na Edward Lowassa ni wa CCM”.
Aliwataka watanzania kusubiri uamuzi utakaotokana na kura za Oktoba 25, kwa kuwa ndizo zitakazoamua nani ni rais. Katika hatua nyingine, aliomba aongezewe fomu za wadhamini kwa sababu 10 alizopewa kwa mikoa 10 nchini zinaweza kuharibiwa na wadhamini pindi watakapokosea kuzijaza. Kutokana na maelezo yake, NEC ilimweleza kuwa ingetoa majibu ya ombi hilo kesho.
Mtikila
Naye mgombea wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, alijigamba kuwa yeye ndiye mwanzilishi wa neno Ukawa, akimaanisha kifupi cha Umoja wa Katiba ya Watanganyika. Alisema Ukawa ya sasa inayotumika kama kifupi cha Umoja wa Katiba ya Wananchi ni nakala tu.
“Niwaombe wananchi msikubali kuchagua nakala, chagueni kitu halisi ambacho ni DP kwani sisi ndio waanzilishi wa Ukawa, hawa wenzetu wameidandia na kuichakachua,” Mtikila alisema.
Akizungumzia uchaguzi mkuu, alisema amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya urais kupitia DP, kwa kuwa hakuna nafasi ya mgombea binafsi. Mtikila alieleza kuwa, nafasi hiyo ya mgombea binafsi haipo kwa sababu haki ya raia imekosekana kimfumo.
Alisema, “Ingawa haki ya mgombea binafsi imekosekana, nitaendelea kuidai”. “...Nimezungumza na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damiani Lubuva kuhusu hili, ndio maana nimechelewa kutoka humo ndani, nilizungumza naye kuhusu uhalali wa kisheria na kukubalika kwa uwepo wa uchaguzi wa mwaka huu,” alisema.
Alisema, katiba ya nchi inatambua haki ya mtu kuchagua au kuchaguliwa, lakini katika mfumo wa sasa ni lazima mgombea nafasi ya urais na nyingine za kisiasa, atoke ndani ya vyama vya siasa.
Kwa mujibu wake, vyama vyote vya siasa nchini havina wanachama zaidi ya milioni saba, wakati idadi ya watu nchini ni zaidi ya watu milioni 44, jambo linalodhihirisha kuwa, idadi kubwa ya watu hawana itikadi za vyama, hivyo kukosa fursa ya kuchagua viongozi kupitia mgombea binafsi.
Mchungaji Mtikila alisema, suala la uongozi ni kipaji na kwamba wapo wananchi wenye vipaji ambao hawatokani na vyama vya siasa.
Alisema, “hao wangependa kugombea nafasi hiyo, lakini kwa kuwa hakuna fursa hiyo, wanakosa haki yao”. Aliwataka Watanzania wasikubali kurubuniwa na mafisadi wakati wa uchaguzi, bali wawapigie kura wagombea wasafi wenye uchungu wa kweli na nchi yao.
TLP
Mgombea mwingine aliyechukua fomu ni kutoka chama cha Tanzania Labour (TLP), Mac- Millan Lyimo aliyesema kuwa kiongozi bora huchaguliwa na Mungu na kwamba, upepo wa kisiasa unaovuma hivi sasa, utaangukia katika chama hicho.
“Tunaomba NEC isiegemee upande wowote bali itimize wajibu kwa kuzingatia haki,” alisema.
Wakati huo huo, mgombea huyo aliwaalika watangaza nia waliokatwa au kufukuzwa kwenye vyama vyao wajiunge na TLP, kwa sababu ina nafasi nyingi wanazoweza kuzitumia kupata uongozi, ukiwemo ubunge na udiwani.
Uchukuaji fomu NEC, utaendelea keshokutwa ambapo mgombea urais kupitia CCM, Dk Magufuli atachukua fomu siku hiyo na Agosti 5, mwaka huu, mgombea wa TADEA atachukua fomu.
Agosti 17, mgombea urais wa ACT atachukua fomu na ratiba kwa vyama vingine itaendelea kutolewa

Comments