waziri awashukia watenda mgodini
Mirerani. Waziri wa Nishati ya Madini, George Simbachawene amewataka wawakilishi wa Serikali kwenye Mgodi wa Tanzanite One kutekeleza wajibu wa kulinda masilahi ya Taifa.
Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Sky Associate Ltd.
Akizungumza
wakati wa kuzindua kamati ya pamoja ya kuendesha mgodi huo, Waziri
Simbachawene alisema wakati mbia Sky Associate akifanya kazi nzuri, mbia
mwingine ambaye ni Kampuni ya Serikali ya Stamico, watendaji wake
hawaonekani kutekeleza wajibu wao kikamilifu.
“Hatujaona faida yenu hapa...sioni uwajibikaji wenu, hakikisheni mnalinda masilahi ya Serikali,” alisema Simbachawene.
Waziri
Simbachawene alisema haiwezekani watendaji wa Serikali katika mgodi huo
wawe sehemu ya malalamiko, badala ya kushirikiana na mwekezaji kuongeza
uzalishaji.
Hata hivyo, waziri huyo aliipongeza Sky
Associate kwa kuendelea kupanua mgodi huo na kuagiza kampuni hiyo
kutekeleza ahadi zake, ikiwamo kusaidia jamii inayozunguka mgodi huo.
Aliwataka
watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha wanaondoa matatizo
ya mipaka katika mgodi huo na kuhakikisha kila mchimbaji anachimba
katika eneo lake.
Mwenyekiti wa kamati ya kuendesha
mgodi huo, Faisal Juma alisema watahakikisha wanatekeleza ahadi zote
walizokubaliana na Serikali katika kuhakikisha pande zote zinanufaika.
Juma alisema tayari ahadi nyingi zimetekelezwa na wanaendelea kuhakikisha Watanzania wananufaika na Madini ya Tanzanite.
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Sky Associate, Hussein Gonga alisema kama wabia
wanaishukuru Serikali kwa kuzindua kamati hiyo, kwani itasaidia
uwajibikaji na uwazi katika kufanya kazi.
Kwa upande
wake, Kamishna wa Madini, John Nayopa alisema wizara itaendelea
kusimamia sheria za uchimbaji madini na kudhibiti uuzwaji holela madini
ya Tanzanite.
“Tayari imeundwa kamati ya maridhiano
baina ya wachimbaji wadogo na wawekezaji, tuna imani itasaidia kupunguza
migogoro ya Mirerani,” alisema Nayopa
Comments
Post a Comment