SABABU 5 ZINAZOZUIA KUPATIKANA AMANI SUDANI KUSINI
Viongozi na wapatanishi wa mzozo wa Sudan wamekuwa wakiwa na mikutano kwa zaidi ya mwaka moja u nusu sasa bila mafanikio.
Pande zinazozozana nchini Sudan Kusini zinatarajiwa kufanya mazungumzo zaidi nchini Ethiopia hivi leo.
Leo ni siku ya mwisho ya mazungumzo ya amani kabla ya vikwazo vya kimataifa kuwekewa pande zote husika.
Wanajeshi wameripotiwa kuua watoto kuwabaka wanawake na kusababisha mamilioni ya watu kutoroka makwao.
Washirika wamekuwa wakishikilia kuwa mkataba wa kusitisha mapigano sharti utiwe sahihi hii leo.
Hivi ndivyo vizuizi vikuu vitano vinavyozuia kupatikana kwa amani Sudan Kusini.
1. Wapinzani wawili wakuu
Rais Salva Kiir na kiongozi wa
waasi Riek Machar wamewahi kutia sahihi mikataba kadhaa lakini wanavunja
makubaliano ya kusitisha vita na kurejelea mapigano.
Maswali Ibuka;
Je wanawajali raia wa Sudan Kusini wanaoendelea kuteseka ama ni maslahi yao wenyewe?
Je viongozi hao wawili wako tayari kujitolea ilikusimamisha mapigano?
Je iwapo mataifa jirani na Marekani watawawekea shinikizo itazaa amani ?
Je uchumi wa taifa unavyoendelea kuzorota unawahusu ?
Shinikizo kutoka kwa Marekani na mataifa jirani linazidi.
2. Serikali Mahuluti
Mataifa yenye ushawishi pamoja na Marekani yaani Igad Plus
yamekuwa yakishinikiza kuundwe serikali ya mseto itakayojumuisha
serikali ya rais Kiir na viongozi wa upinzani akiwemo bwana Machar.
Pendekezo hilo limepingwa na wahusika wakuu hata kabla ya mkondo wa mwisho mazungumzo ya mapatano kuanza.
Serikali ya rais Kiir haitaki kuweko kwa kundi la tatu huru litakalosimamia usalama karibu na Juba.
Vilevile Serikali inapinga majimbo matatu yaliyoathirika zaidi na mapigano kuwa chini ya waasi.
Majimbo hayo itakumbukwa kuwa ndiyo yenye mafuta mengi.
Kwa upande wao Upinzani nao unataka kuwa na usemi mkubwa zaidi katika serikali mahuluti
Mashirika
ya kupigania haki za kibinadamu nazo zimepinga mkataba huo wakisema
kuwa unatilia sisitizo kwa ugavi wa mamlaka miongoni mwa mabwenyenye
wachache wala sio kusisitizia kuwepo kwa njia ama mbinu za kuwawajibisha
viongozi wakuu katika serikali hiyo na yeyote ile itakayokuwa uongozini
Juba.
Aidha wangependa chimbuko la mzozo huu ushughulikiwe
ilikuzuia mapigano siku za usoni mbali na kuwachukulia hatua wale wote
ambao wametenda makosa ya kivita Sudan Kusini.
Kibwagizo ni kuwa
mpango huo wa kusitisha mapigano haupaswi kuangaliwa ni kama ndio
suluhisho la vita ila utumiwe kama mwanzo wa makubaliano ya amani baina
ya pande zote hasimu.
3. Mataifa jirani ya Sudan Kusini
Katika kipindi cha mwaka mmoja u
nusu uliopita viongozi wa mataifa jirani na Sudan Kusini wamekuwa
wakijaribu kuleta uwiano baina ya mahasimu hao wawili lakini bila
mafanikio.
Hii imetokana na kuwepo kwa ushawishi fulani na uhusika wao kwa njia moja au nyengine na hali ilivyo huko Sudan Kusini.
Uganda kwa mfano ilituma majeshi yake kuilinda mji mkuu wa Juba.
Sudan
kwa upande wake imewaruhusu wapiganaji waasi kukita kambi zao ndani ya
mipaka yake mbali na kuwahami kwa silaha nzito nzito.
Kenya kwa
upande wake ingependa kujishirikisha kwa sababu za kiuchumi huku
Ethiopia ikisisitiza kuwa ingependa kuongoza mpango wowote wa amani.
4. Kusambaratika kwa waasi
Uasi
chini ya bwana Machar ulikuwa wa kipekee;makundi ya waasi ambao
walikuwa wamekosana na serikali kwa sababu moja au nyengine yaliungana
na kuishambulia serikali.
Kulikuwa na makundi ya raia waliojihami
kwa silaha na vilevile kulikuwa na baadhi yao ambao walikuwa ni
wanajeshi walioasi jeshi la taifa la SPLA.
Kwa hivyo alipotangaza
kujitenga na kundi linaloshirikiana na Machar, Jenerali Peter Gadetand
Gathoth Gatkuoth alidai kutengwa na Machar.
Gatkuoth alidai hakufurahia
kuwa Machar alikuwa anafanya mazungumzo ya kurejea serikalini na
kugawana mamlaka na hasimu wao mkuu rais Salva Kiir.
Je iwapo makundi ya waasi yamegawanyika wale wanaomuunga mkono jenerali muasi Gatkuoth alidai ni wangapi ?
na wanauwezo wa kutibua makubaliano ya amani ?
Hilo ndilo linasubiriwa kubainika huko Ethiopia.
5. Ukabila
Mamilioni ya raia wa Sudan kusini wamezaliwa katika vita.
Vita vya kwanza kati ya waasi wa Kusini na Serikali ya Kaskazini vilidumu kwa muda mrefu kati ya mwaka wa 1955-1971.
Kizazi kizima cha raia wa Sudan Kusini walizaliwa na wakabalehe vita vya wenyewe kwa wenyewe vikiendelea.
Mara ya pili vita hivyo vilipoanza vilidumu kwa kipindi kirefu zaidi yaani kati ya mwaka wa (1983-2005).
Kwa
hivyo vizazi viwili vya wananchi wamezaliwa katika vita , kiasi cha
kuwa hata baada ya kupata uhuru wake mwaka wa 2011 amani haikudumu kwa
zaidi ya miaka miwili.
Vita vinavyoendelea hadi sasa vilianza desemba mwaka wa 2013.
Ubabe kati ya watu wa kabila la wa- Nuer na wa- Dinka, ndio uliotawala siasa za taifa hilo.
Inaaminika
kuwa watu wa kabila dogo la Bul Nuer waliisaidia serikali kukabiliana
na jamii kubwa ya wa-Nuer hii ni kumaanisha kuwa sasa kuna uhasama baina
yao na jamii ya watu wa kabila la Nuer.
Na kwa sababu matabaka mawili makubwa yamekuwa yakipigana na kulipiziana kisasi inakuwa shida mno kupata amani ya kudumu.
Comments
Post a Comment