JK:KUWENI WAZI NA FEDHAZA WAFADHILI

 
RAIS Jakaya Kikwete amezitaka asasi za kiraia kuweka wazi fedha wanazozipata kutoka kwa wafadhili na namna wanavyozitumia, na wanapotakiwa na Serikali kutoa taarifa hizo wasione kama wanaingiliwa utendaji wao.

Mwito huo ulitolewa na Rais Kikwete jana alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa Takwimu Huria Kanda ya Afrika (Africa Open Data) uliofanyika kwa mara ya kwanza Afrika na kuhudhuriwa na washiriki kutoka nchi 30 za Afrika ambapo Tanzania ilikua mwenyeji.
Rais Kikwete alisema watu wanahitaji kujua asasi hizo zinafanya nini, fedha wanazozipata zinatumikaje na pia serikali inaweza kuhitaji taarifa hizo kwa sababu za kiusalama, hivyo wasione usumbufu wanapotakiwa kutoa taarifa hizo.
“Asasi hizi zinapoulizwa taarifa zao ziwe wazi lakini ukiuliza wanaona wanaonewa, serikali inapata fedha kutoka kwa wafadhili hao, lakini ukiwauliza inaonesha kama kuwaingilia, serikali taarifa zake zinakua wazi tu,” alisema Rais Kikwete.
Kikwete alisema serikali kwa kiasi kikubwa inajitahidi kutoa taarifa kwa umma zinazohusu takwimu katika mambo ambayo ni wazi, vivyo hivyo iwe katika sekta binafsi pamoja na asasi hizo ili kuweka uwajibikaji.
Aidha, Rais Kikwete alisema ni vizuri wananchi wakajua fedha zimepokewa kiasi gani, lini, kwa shughuli gani na kama matumizi yaliyokusudiwa yameweza kufanyika ipasavyo na hiyo haimaanishi kuwaingilia katika majukumu yao.
Akielezea Tanzania ilivyotekeleza masuala ya takwimu huria, alisema serikali yake iliweza kuajiri wahasibu 780 katika halmashauri mbalimbali hapa nchini ili kuondoa hati chafu, jambo ambalo limefanikiwa na sasa ni halmashauri zisizozidi mbili ambazo hazijafanikiwa.
“Niliwaambia halmashauri zote lazima ziajiri wahasibu hao na baada ya muda mfupi hali ya kuwa na hati chafu ikapotea, lakini haitoshi kuwa na hati safi pekee lakini sasa inaonyesha kwa uwazi fedha zinatumikaje,” alisema Rais Kikwete.
Alisema katika suala hilo serikali pia iliamua kuanza kujadiliwa kwa uwazi taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bungeni na hatua kuchukuliwa kwa taasisi ambazo hesabu zake hazitakuwa sawa.
“Haitoshi tu kusema kila kitu kiko sawa pasipo kuhusisha tukio halisia na usimamizi mzuri utasaidia Tanzania watu kuona moja kwa moja...hata hivyo hatuwezi kufika mahali tukasema kila jambo la serikali liwe wazi, hiyo haiwezi kuwa sahihi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kuna mambo ambayo serikali haiwezi kuweka wazi na hii ni kwa sababu za usalama wa nchi au unyeti wa jambo lenyewe na hivyo kuliacha mpaka pale ambapo linakuwa tayari kuwekwa wazi.
Akieleza mafanikio ambayo yamefikiwa kwa kuwa na uwazi alisema, katika sekta ya madini serikali imeweza kuweka wazi ni madini kiasi gani yanapatikana, kilichouzwa na pia ni kodi kiasi gani imeweza kukusanywa katika sekta hiyo.
Aidha Rais Kikwete alisema kutokana na kwamba takwimu huria inasaidia katika kuinua uchumi wa nchi basi ni vema nchi za Afrika kukumbatia mfumo huo ili kuongeza uwajibikaji katika sekta zote.
“Kuna haja kwa bara la Afrika kukumbatia masuaa haya kwa ajili ya kuboresha utendaji katika sekta zote, hii ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi,” alisema.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema ni jambo la fahari kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kwanza katika bara la Afrika ambao una lengo la kudumisha uwazi wa utoaji takwimu mbalimbali na katika sekta mbalimbali ambao ni kichocheo cha maendeleo.
Alisema thamani ya mfumo huo inaharakisha maendeleo ya nchi na pia kutoa nafasi kwa wananchi kushuhudia maendeleo ya nchi na pia mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali na kuweza kuhoji.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird alisema matumizi mazuri ya utoaji taarifa za takwimu yatasaidia kuondokana na umasikini. Bird alizitaja nchi ambazo zimenufaika katika suala hilo mbali na Tanzania kuwa ni pamoja na Kenya, Ghana, Liberia, Malawi, Tunisia na Nigeria ambapo alisema kwa nchi ya Kenya wakulima wameweza kuwafikia wafanyabiashara moja kwa moja bila kupita kwa watu wa kati na hivyo kupata faida nzuri katika mazao yao

Comments