KATIBU WA TABOA ATAKIWA KUACHIA NGAZI

 

WANACHAMA wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) wamemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Enea Mrutu kuachia uongozi kwa madai ya kushindwa kufatilia maslahi yao serikalini.

Wanachama hao wamedai kuwa wamekosa imani na kiongozi huyo kwani hakuna majibu ya msingi anayotoa huku wao wakiendelea kupata hasara kwa mabasi walioagiza kushindwa kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Mweka Hazina wa chama hicho, Issa Nkya madai hayo ni pamoja na kushushwa kwa ushuru wa uingizwaji wa mabasi nchini kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 ambao ulikuwa ukitumika awali kutolea mabasi zaidi ya 40 yaliyokwama bandarini.
Alisema wanatoa siku tano kwa uongozi wa Taboa kufuatilia kwa nguvu zote suala hilo na kutoa majibu yenye utatuzi na endapo wasipofanya hivyo watalazimika kuvunja uongozi kwa kuitisha mgomo nchi nzima ili kuishinikiza serikali kuwasaidia.
“Tumekuwa hatupati majibu kutoka kwa serikali juu ya hatima ya mabasi yetu yaliyopo bandarini kwani wengine tulikopa benki kuingiza mabasi hayo na benki inasubiri kutukata, sasa sisi tutapata wapi fedha za kuwalipa,” alisema.
Kwa upande wake Mustaph Mwalongo alisema, wamekosa imani na katibu huyo kwani katika mkutano wao wa mwisho wa wamiliki wa mabasi waliazimia kuitisha mgomo lakini aliuzuia kwa madai ya kushughulikia suala lao.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa chama hicho akizungumza kwa njia ya simu alisema, amepata taarifa za kuwepo kwa malalamiko ya wanachama kwa muda mrefu kuwa ameshindwa kufuatilia madai yao serikalini lakini amekuwa akijitahidi kufuatilia suala lao.
Alisema amekuwa akifuatilia suala hilo na kuandika barua kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha na Waziri wa Uchukuzi pamoja na kukaa kikao na Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal bila kupata ufumbuzi.
Alisema wamekosa ushirikiano kutoka kwa serikali jambo ambalo linamkatisha tamaa na kuonekana hafanyi jitihada kwani kwa juhudi zake alijitahidi kuzima mgomo uliotaka kutokea kwa kuona kuwa serikali ingeweza kuwasaidia pasipo mgomo.
“Sioni sababu kwanini serikali ishindwe kutuhurumia ili tutoe magari yaliopo bandarini kwa ushuru wa awali wa asilimia 10 kwani mabasi hayo yaliagizwa mapema kabla ya ushuru kupanda kama suala la kushushwa kwa ushuru limeshindikana tuonewe huruma kwa hilo basi,” alisema

Comments