KUFA AU KUPONA LEO KATIKA UWANJA WA TAIFA
PATASHIKA nguo kuchanika wakati leo timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itakapowakaribisha wenzao wa Nigeria ‘Super Eagles’ kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo wa kusaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Tanzania katika mechi hizo za kufuzu kwa ajili ya fainali hizo za Mataifa ya Afrika, imepangwa katika Kundi G pamoja na Nigeria, Misri na Chad. Kiviwango, Chad ndio iko chini ya Tanzania baada ya kushika nafasi ya 171 duniani wakati Tanzania ni ya 142 kwa mujibu wa viwango vya mwezi uliopita. Chad imepanda nafasi moja wakati Tanzania imebaki pale pale kwa mujibu wa viwango vilivyotolewa Septemba 3.
Misri kwa mujibu wa viwango hivyo vya ubora ilikuwa katika nafasi ya 52 lakini imepanda na kuwa ya 49 wakati Nigeria iko katika nafasi ile ile ya 53, hivyo ukiangalia ubora huo Tanzania iko chini kiviwango. Timu mbili za kwanza kutoka katika kundi ndizo zitapata nafasi ya kufuzu kucheza fainali hizo za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon mwaka 2017.
Ugumu wa mchezo huo Taifa Stars pamoja na kupiga kambi Uturuki kwa siku takribani nane, lakini ina kazi kubwa mbele yake ya kufanya ili kuibuka na ushindi dhidi ya vigogo hao wa Afrika kwani kambi hiyo ya Uturuki sidhani kama itakuwa imeisaidia sana timu hiyo. Pamoja na katika soka lolote linaweza kutokea, lakini ili Taifa Stars iifunge Nigeria inahitaji maajabu ya aina yake kwani kiuwezo, Super Eagles iko juu yao.
Kikosi cha Super Eagles kina wachezaji wenye uzoefu mkubwa na kambi ya maandalizi ya Uturuki sidhani kama itakuwa imeisaidia au imeiongezea kitu timu hiyo. Kimsingi hakukuwa na umuhimu wowote kwa timu hiyo kwenda kupiga kambi Uturuki kwani ingeweza kwenda katika moja ya mikoa ya Tanzania Bara au Zanzibar na kufanya mazoezi vizuri tena kwa utulivu mkubwa.
Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatakiwa kuwa makini sana kupanga mazoezi na mahali pa timu hiyo kupiga kambi, ili kuhakikisha inaenda mahali ambako mazoezi yake yatakuwa na tija kwa timu hiyo. Rekodi ya Nigeria Kirekodi Tanzania imefuzu mara moja tu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 zilipofanyikia Lagos, Nigeria wakati Super Eagles imefuzu mara nyingi huku ikitwaa taji mara tatu.
Mbali na kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, Super Eagles pia mara kadhaa imefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia wakati Taifa Stars haijawahi hata mara moja kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia. Nigeria mbali na kuwa mwenyeji wa fainali hizo za mwaka 1980, pia ilitwaa ubingwa mwaka huo pamoja na ile ya 1994 na 2013, hivyo Super Eagles imetwaa ubingwa huo mara tatu wakati Taifa Stars haijawahi kutwaa taji hilo.
Kikosi cha Nigeria kimesheheni wachezaji wanaocheza soka la kulipwa isipokuwa wachezaji kama wanne tu ndio wanaocheza Nigeria wakati Tanzania kuna wachezaji watatu tu wanaocheza nje ya nchi. Mechi za majaribio Taifa Stars ilipiga kambi Uturuki na kucheza mechi ya majaribio dhidi ya Libya na kufungwa mabao 2-1. Matokeo hayo hayatoi picha halisi ya uwezo wa Taifa Stars, kwani Libya sio miongoni mwa vigogo vya soka barani Afrika licha ya kuwa na kiwango zaidi.
Kwa mujibu wa viwango vya Fifa vya soka vilivyotolewa Septemba 3, Libya ilikuwa katika nafasi ya 98 lakini ikiwa imeporomoka mara nne kutoka viwango ilivyokuwa awali. Taifa Stars inatakiwa kupata mechi nyingi za majaribio na timu tofauti tofauti na zenye uwezo kama Ivory Coast, Ghana, Burkina Faso, Mali, Algeria, Congo na zingine zenye uwezo ili kuipa mazoezi na uzoefu wa kucheza na timu tofauti tofauti.
Stars iache kucheza mechi laini ambazo hazitaweza kuisaidia katika maandalizi yake ya mashindano ya kimataifa kwa kuwapa uzoefu wachezaji wake. TFF isitumie fedha nyingi kwa kuipeleka timu kucheza mechi ngumu ili iweze kuzoea mikikimikiki na kuona wenzao wanafanya nyingi mchezoni. Nigeria sasa iko chini ya mchezaji wa zamani wa kimataifa Sunday Oliseh aliyechukua nafasi ya Stephen Keshi aliyetimuliwa na Shirikisho la Soka la Nigeria huku Stars ikifundishwa na Charles Mkwasa.
Msimamo Kundi G Taifa Stars iko katika Kundi G na tayari imeshafungwa mabao 3-0 katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Misri uliofanyika huko Alexandria na leo ina kibarua cha kutafuta pointi na kurejesha matumaini ya kufanya vizuri. Kimsimamo, Taifa Stars iko katika nafasi ya mwisho ikiwa haina pointi sawa na Chad, lakini Chad ni ya tatu baada ya kufungwa mabao 2-0 na Nigeria, hivyo Nigeria wana pointi tatu sawa na Misri, lakini wanatofautiana kwa mabao ya kufunga.
Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo wake huo wa leo Jumamosi ili angalau kurudisha imani kwa mashabiki ya angalau kuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo. Tatizo la ushambuliaji Tatizo kubwa la Taifa Stars pamoja na klabu za Tanzania kwa ujumla ni ushambuliaji, hivyo wachezaji wake wanatakiwa kuwa makini na kutokosa mabao ovyo wanapokuwa katika nafasi nzuri.
Kama Taifa Stars watashindwa kurekebisha makosa yao ya ushambuliaji, basi safu ya ulinzi itakuwa na kazi ya kuzuia na baadaye kuruhusu mabao kutoka kwa wakali wa Nigeria wenye uchu wa mabao. Ushindi unawezekana Hakuna kisichowezekana katika soka pamoja na kazi ngumu ya kuifunga Nigeria, lakini jitihada zikifanyika na Stars kutofana makosa ya kizembe, basi timu hiyo inaweza kushinda au kuondoka na pointi moja kwa kutoka sare.
Kama Stars iliwahi kuvifunga vigogo vya Afrika, basi hata Nigeria wanafungika ila kinachotakiwa ni kucheza kwa ari na kujituma zaidi ili kufanya vizuri huku mashabiki wakitakiwa kushangilia bila kuchoka.
Comments
Post a Comment