Maelfu ya wahamiaji wawasili Ugiriki
Wahamiaji wakiwasili Ugiriki
Maelfu ya wahamiaji
wanaendelea kuwasili Ugiriki, bara huku serikali ikijiandaa kwa
mazungumzo ya kujadili mbinu za kukabiliana na wahamiaji wengi wanaofika
katika fuo za taifa hilo.
Meli mbili zilizobeba zaidi ya watu 4,200 zilisafiri hadi bandari ya Piraeus, usiku baada ya kuondoka kisiwa cha Lesbos.
Muungano wa Ulaya, EU kwa jumla unahangaika kukabiliana na kufurika kwa wahamiaji.
Mamia ya watu, wengi kutoka Mashariki ya Kati, bado wamekwama nje ya kituo cha reli nchini Hungary, baada ya polisi kuwazuia kusafiri kuingia EU.
Shirika linalodhibiti mipaka ya EU, Frontex, linasema wahamiaji 23,000 waliwasili Ugiriki wiki hii pekee likiwa ni ongezeko la 50% kutoka kwa idadi iliyowasili wiki iliyopita.
Zaidi ya watu 160,000 wamewasili Ugiriki kufikia sasa mwaka huu, idadi ambayo tayari imepita jumla ya wahamiaji waliotua huko mwaka jana.
Lakini katika tukio linaloonyesha hatari wanazokumbana nazo wahamiaji, ripoti leo zinasema Zaidi ya wahamiaji 11, wanaoaminika kuwa raia wa Syria, wanahofiwa kufa maji baada ya boti mbili kuzama zikiondoka Uturuki kuelekea kisiwa cha Kos nchini Ugiriki.
Serikali nchini humo inasema haina rasilimali za kuwahudumia wahamiaji wanaofika huko, lakini mashirika ya kutoa misaada yanasema serikali hiyo inaweza kufanya Zaidi ya inayofanya kwa sasa.
Jumanne, Rais wa Ugiriki, Prokopis Pavlopoulos, alimpigia simu mwenzake wa Ufaransa Francois Hollande na akamsihi kuhakikisha tatizo linalokabili Ugiriki linajadiliwa katika ngazi ya juu Ulaya.
Baraza la mawaziri la muda nchini Ugiriki, linatarajiwa kukutana baadaye leo.
Feri moja iliyobeba wahamiaji 1,749 kutoka Lesbos, iliwasili mji wa bandarini wa Piraeus, karibu na Athens, Jumanne jioni.
Nyingine, yenye karibu wahamiaji 2,500, ilitarajiwa kuwasili mjini humo mapema leo
Comments
Post a Comment