MAGUFULI ASEMA ATAKAEUA JAMBAZI HATOSHITAKIWA
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema serikali yake haitamshtaki askari polisi ikiwa ataua jambazi mwenye silaha.
Mgombea huyo alitoa ahadi hiyo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Mtwara.
“Katika
serikali yangu askari akimpiga jambazi mwenye silaha kwa risasi
hashtakiwi. Kila mara (majambazi) wanavamia vituo vya polisi, mbona
hawavamii kambi za jeshi, Jeshi la Kujenga Taifa au Ukonga FFU?, wanaona
polisi wana nidhamu sasa wanawaonea na kuwaua,” alisema Magufuli.
Mgombea
huyo wa urais wa CCM pia aliahidi kwamba ataboresha maslahi ya askari
polisi ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na wakiwa na furaha.
Kadhalika,
aliahidi kuwa akichaguliwa kuwa Rais, atahakikisha makusanyo ya kodi
kwa mwezi yanaongezeka mara mbili kutoka yanayokusanywa sasa ya Sh.
bilioni 900 hadi Sh. tirioni 1.8.
“Serikali
ya awamu ya nne ilikuwa inakusanya mapato ya kila mwezi Sh. bilioni
300, lakini sasa yameongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 900 kwa serikali
ya Magufuli nitahakikisha mapato yanafikia mara mbili ya haya,” alisema Dk. Magufuli.
Katika
hotuba yake iliyoanza saa 10:12 jioni, mgombea huyo aliyekuwa
akishangiliwa na umati uliojitokeza kumsikiliza sera zake, aliahidi pia
kuwapatia wananchi maendeleo.
Alisema
wingi wa watu waliojitokeza kumsikiliza unadhihirisha kuwa Watanzania
wanahitaji mabadiliko ya kweli ambayo yataletwa na CCM.
“Kwa
idadi hii kubwa ya watu inadhihirisha kuwa wana Mtwara na Watanzania
kwa ujumla sasa wanataka mabadiliko na siyo kusema mabadiliko tu bali ya
kweli na ndiyo maana urais. Nilipoomba urais sikuwa najaribu, nimekuwa
mbunge kwa miaka 20 hivyo naifahamu vizuri serikali na nafahamu mahali
serikali ilipolegea, nichagueni mimi niwatumikie,” alisema Dk. Magufuli.
Aidha,
aliahidi kujenga barabara zilizosalia kutoka Mtwara- Newala
-Tandahimba hadi Masasi. Mbali na hilo, aliwaahidi wananchi wa Mtwara
kuwa watajengewa bandari kubwa kama za Dar es Salaam na Tanga pamoja na
viwanda.
“Serikali
ya Magufuli ni ya viwanda, serikali ya Rais Kikwete imejenga kiwanda
cha saruji kinachomilikiwa na Dangote, mkinichagua nitamwaga viwanda
vingi zaidi ili vizalishe na kutoa ajira kwa watu wengi,” alisema na kushangiliwa.
Awali
jana akizungumza katika mkutano wa kampeni wilayani Tandahimba, mkoani
Ruvuma kabla ya kwenda Mtwara, Dk. Magufuli, alisema anatambua shida
wanaozopata wakulima wa korosho kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na
kuahidi kuzipatia ufumbuzi.
Wakulima
wa zao hilo mikoa ya Kusini mwa Tanzania wamekuwa wakiulalamikia
utaratibu huo kwa muda mrefu, wakisema ni wa kinyonyaji.
Dk.
Magufuli pia aliahidi kutatua matatizo ya wakulima wa korosho
kucheleweshewa fedha, kulipwa nusu na uhaba wa dawa na pembejeo
kuchelewa.
Akizungumza
katika mikutano ya kampeni katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya
Tandahimba, Dk. Magufuli alisema pia kuna wabadhilifu wa fedha za
wakulima ndani ya vyama vya ushirika na kwamba serikali yake itaondoa
kero hizo ili wakulima wanufaike na kilimo hicho.
“Nimesomea
Shahada ya Uzamivu ya masuala ya korosho, hayo ndiyo masuala yangu,
mnatakiwa kunufaika na korosho na pia maganda yake yanaweza kutengeneza
gundi na vitu vya kuzuia kutu, tutaongeza viwanda vikubwa vya korosho
ili kuongeza thamani ya mazao yenu mnufaike,” alisema.
Alisema atahakikisha bei ya korosho inaongezeka kutoka ya sasa ya Sh. 300 kwa kilo moja.
“Hapa
Tandahimba kuna vyama vingi vya ushirika lakini havifanyi vizuri,
tutaviimarisha vihudumie wakulima ipasavyo walipwe fedha bila kukopwa,
wanaodokoa fedha nitawadhibiti,” alisema.
Akizungumzia gesi, alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi kama gesi, mafuta, wanyama, madini na nyingine nyingi.
Alisema uchumi wa gesi utawezesha viwanda vingi kujengwa na watu kupata ajira.
Dk. Magufuli alisema gesi ni lazima inufaishe wananchi wa eneo husika kabla ya kunufaisha wengine.
“Gesi
imetoka hapa lazima wakazi wa hapa mnufaike kwanza, huwezi kuwa na gesi
inufaishe wengine, mpate umeme wa uhakika, ajira na uchumi wetu
ubadilike,” alisema.
Aidha,
aliwatahadharisha wananchi hao dhidi ya nchi za Ulaya zinazonyemelea
utajiri wa Tanzania na kwamba wasiruhusiwe kuwagawa Watanzania.
“Siku
zote vita ya panzi ni furaha ya kunguru, mtu akihubiri ugomvi, chuki
na kutokuwa na amani siyo mwenzetu, msikubali kuchonganishwa na
wanaotumika na wanaozitamani rasilimali zetu,” alisema.
Alisema
kugunduliwa kwa gesi kutawezesha ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati
na vikubwa kwa kuwa rasilimali hiyo inaweza kufanya mambo mengi ikiwamo
Tanzania kuwa na kiwanda cha ndege.
Comments
Post a Comment