MAGUFULI MTEGONI ,,,, WANANCHI WAMPOKEA KWA MABANGO WAMTAKA AMNYANGANYE SHAMBA SUMAYE


Mgombea  urais kwa tiketi ya CCM,Dk. John Magufuli jana alikumbana na mtihani wa kwanza wa wananchi baada ya kupokewa na mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Miongoni mwa mabango hayo ni lile lililokuwa limeandikwa. Waziri Mkuu mstaafu Federick Sumaye arudishe shamba analomiliki kwani limegeuka pori,”.

Hali hiyo, ilitokea wakati msafara wa Dk. Magufili ukielekea  wilayani Mvomero.

Alipofika Kona ya Wami, alijikuta akipokewa na mabango mengine ambapo alilazimika kusimama kwa muda.

Baada ya kusimama, Dk. Magufuli alishuka kwenye gari lake na kumwita mgombea ubunge wa Jimbo la Mvomero, Sadik Murad asome kwa sauti mabango hayo mbele ya wananchi hao.

Murad, alisoma bango hilo lililokuwa limeandikwa ‘Magufuli chukua shamba la Sumaye’.

Kutokana na maneno hayo, Dk. Magufuli aliwajibu wananchi hao kwa kifupi na kusema amesikia kilio chao na kuahidi kukifanyia kazi.

“Nimesikia ombi lenu wananchi nitalishughulikia,” alisema kwa kifupi Dk. Magufuli.

Akihutubia wananchi wa Wilaya za Mvomero, Kilindi na Handeni kwa nyakati tofauti jana, Dk. Magufuli alisema ameziona changamoto zinazokabili wilaya hizo, ikiwamo adha ya barabara na migogoro ya ardhi inayosababisha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

“Nipo hapa Kilindi, napenda kuwaahidi lazima tujenge barabara ya kutoka Handeni, Kilindi kupitia Mvomero , Ifakara, Malinyi hadi Wilaya ya Namtumbo.

“Najua kuna watu wamekuwa wakichochea migogoro ya ardhi, ikiwamo mpaka kati ya Kilindi na Kiteto. Kuna viongozi wanahongwa ng’ombe sasa jueni sasa ni mwisho wenu.

“Ukiacha hao kuna baadhi ya watu hapa Tanga, wamechukua mahekta ya ardhi na kwenda kukopa mikopo benki na leo hii wamekua mabilionea, huku wananchi wakibaki maskini,” alisema.

Comments