MASHEHE WALIOTEKWA DRC WAREJEA
MASHEHE sita waliokuwa wametekwa na waasi nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia Congo (DRC) wamerejea nchini jana, huku wakieleza kuwa
kulitaja jina la Tanzania kumewaokoa na kifo kutoka kwa waasi hao.
Kitendo cha mashehe hao kutaja wanatokea Tanzania kimewasaidia kwani
kwa mujibu wao, waasi hao walisema hawana shida na Tanzania, lakini
Wakongo waliwadanganya hivyo hawawapendi.
Akizungumza baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, kiongozi wa mashehe hao, Mohammed Abdallah Khamis
alisema, wakiwa njiani kuelekea nchini humo walivamiwa na watu hao
wakiwa na silaha za kivita kisha kutekwa na kupelekwa porini.
“Mwanzo hatukuelewa kama ni wanajeshi wa serikali au wanajeshi wa
porini, tulipofika nao porini ndiyo wakajitambulisha wao ni askari wa
porini na wanahitaji fedha ili watuachie ama watatuua,” alisema Khamis.
Akisimulia jinsi walivyoishi porini alisema, walikuwa wanapata tabu
kwani hata chakula walikuwa wakipewa ndizi, maharage na magimbi ambayo
waliambiwa wale ili wasife, huku wakati mwingine wakiteswa na waasi hao
kwa kupigwa na magongo na vibao.
Alisema waasi hao walihitaji wapewe kiasi cha dola za Marekani 20,000
(zaidi ya Sh milioni 60) ili waweze kuachiwa. Khamis aliishukuru
serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizofanya ili kuhakikisha wapatikana
wakiwa salama. “Kwa kweli tunaipongeza sana serikali ya Tanzania na DRC
maana wamefanya juhudi kubwa sana za kutuokoa.
Bora kuishi mwaka mmoja gerezani lakini si kukaa na watu wale siku
moja,” alisema. Khamis alisema, hata hivyo baadaye waliachiwa na waasi
hao baada ya kuona hawana fedha lakini pia ni wazee, hivyo waliwaachia
kwa huruma na hasa kwa kuzingatia hawana shida na Watanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim akizungumza baada ya kuwapokea mashehe
hao alisema, wakati wote serikali ilikuwa ikifuatilia suala hilo ili
kujua usalama wao.
Hata hivyo, alisema kuna umuhimu kwa Watanzania wanaosafiri kwenda
katika nchi tofauti kwa shughuli mbalimbali kuhakikisha wanatoa taarifa
katika Balozi zilizopo katika nchi hizo ili serikali iwe na taarifa ya
Watanzania hao.
“Tunaishukuru sana serikali ya Congo na jamii nzima ya watu wa Goma
ambao walitoa msaada mkubwa na hata walinzi wa amani wa Congo
walishiriki vizuri katika kuhakikisha mnapatikana mkiwa salama,”
alisema.
Alisema kutokana na kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vikifuatilia
tukio hilo kwa ukaribu, hata baada ya kuachiwa kwa mashehe hao, vikosi
hivyo vilifanikiwa kuwakamata watekaji hao.
Balozi wa Tanzania nchini DRC, Anthony Cheche alisema, baada ya
kupokea taarifa hizo walifuatilia na baada ya kubaini ni Watanzania
ndiyo juhudi za kuwakomboa zikaanza. Alisema alikuwa akipokea simu
nyingi kutoka kwa vyombo vya habari na ndugu, jamaa na marafiki za
kutaka kujua hali za mashehe hao lakini wakati mwingine alilazimika
kuficha ukweli ili kuepusha kuhatarisha usalama wa mashehe hao.
“Tulipewa tahadhari kuwa kuna mazingira hatarishi, hivyo kuna baadhi
ya taarifa zikitolewa zinaweza kusababisha tukawapoteza watu wetu na
ndiyo sababu kuna taarifa nilikuwa nikiziminya,” alisema.
Baada ya kuachiwa kwa mashehe hao ambao wote ni wakazi wa Zanzibar,
walipokewa na Jeshi la DRC na kupewa ulinzi hadi Mji wa Goma ambapo
walikutana na viongozi wa mji huo pamoja na Balozi Cheche ambaye
waliondoka naye hadi mjini Kigali, Rwanda kwa ajili ya kurejea nchini.
Mashehe hao ambao walienda nchini humo kwa ajili ya kutangaza dini,
walirejea jana kwa ndege ya Shirika la Rwanda saa 9:55 mchana ambapo pia
jana hiyohiyo waliondoka saa 12:00 kuelekea Zanzibar kwa ndege ya
Shirika la Precision.
Comments
Post a Comment