MBINU MPYA ZA KUZUIA WIZI YA MAFUTA NIGERIA
Shirika la Kitaifa
la mafuta nchini Nigeria, NNPC, limesema litatumia ndege zisizo na
rubani kufuatilia safari za meli katika juhudi za kukabiliana na wizi wa
mafuta ambao umekithiri mno.
Shirika hilo la NNPC, limesema linataka kumaliza wizi wa mafuta ghafi katika muda wa miezi minane ijayo.
Nigeria ndio mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ghafi Afrika, lakini mapato kutokana na mafuta hayo hupungua sana kutokana na wizi na uporaji kwenye mabomba ya mafuta.
Rais mpya wa nchi hiyo, Muhammadu Buhari, ameapa kusafisha sekta hiyo.
Mafuta huchangia 70% ya mapato ya Nigeria, ambayo ndiyo nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika.
Lakini ripoti ya shirika la Chatham House ya 2013 ilisema mapipa 100,000 huibiwa.
Hiyo ni sawa na 5% ya jumla ya mafuta yanayozalishwa Nigeria kila siku.
Ripoti hiyo ilisema wizi ulikuwa ukifanyika katika "kiwango kikubwa", mashua zikitumiwa kusafirisha mafuta yaliyoibiwa kwa meli kubwa baharini ili yasafirishwe katika mataifa mengine.
Wanasiasa mashuhuri na maafisa wakuu jeshini wanadaiwa kuhusika katika biashara hiyo haramu.
Mkuu mpya wa NNPC, Ibe Kachikwu, pia alisema kampuni hiyo itafanya kazi kwa karibu na jeshi la majini la Nigeria kukabiliana na tatizo hilo.
Comments
Post a Comment