MBUNGE WA CCM AIBUKA KWENYE KAMPENI ZA ACT WAZALENDO........POLISI WAMUONDOA KUEPUSHA VURUGU


Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), aliyemaliza muda wake, Ally Keissy jana aliibuka kwenye mkutano wa kampeni wa chama cha ACT-Wazalendo na kupinga maelezo kwamba mshahara wake wa ubunge ni zaidi ya Sh10 milioni.

Keissy aliwasili kwenye mkutano huo uliokuwa wa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira na mgombea mwenza wake, Hamad Yusuph Mussa uliofanyika Kijiji cha Namanyere, akiwa kwenye gari lake aina ya Toyota Land Cruiser.

Mgombea mwenza, Mussa alipopanda jukwaani, alianza kuhutubia kwa kuwaeleza wananchi kwamba mbunge wao, Keissy anayemaliza muda wake ameshindwa kuwaletea maendeleo, hivyo mwaka huu wasimpe kura zao.

“Niwaambie kitu, wabunge wenu akiwamo Keissy wanapata mshahara wa zaidi Sh10 milioni ndiyo maana akiwa bungeni kazi yake ni kupiga makofi kwa kushangalia kupitisha kwa bajeti ambayo haina masilahi kwa wananchi wa jimbo lenu,” alisema Mussa na kushangiliwa na umati ambao mmoja alisikika akisema:

“Sema baba sema, ujumbe umefika na mwenyewe yupo hapa.”

Kauli hiyo ilionekana kumkera Keissy, ambaye alinyanyuka alipokuwa ameketi na kwenda kwenye gari lake kuchukua ‘salary slip’ iliyogongwa muhuri wa Ofisi ya Bunge, ikionyesha kwa mwezi anapokea mshahara Sh3 milioni.

Akionyesha kukerwa na alichoeleza kuwa ni upotoshaji wa mgombea mwenza, Keissy alikwenda karibu na meza kuu na kumwita Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis na kumkabidhi nyaraka hiyo ili aipeleke jukwaani kwa mgombea mwenza aliyekuwa akiendelea kuhutubia.

Hata hivyo, Mussa alipopelekewa nyaraka hiyo aliwaambia wananchi: “Keissy anasema nimpige kidogo kidogo maana yamemchoma.” 
 
Keissy hakuonyesha kuridhika na majibu hayo na alionyesha ishara za kutaka kulazimisha nyaraka hiyo isomwe, kitendo kilichozuiwa na askari waliokuwa eneo hilo na kumtaka aondoke kwa kuwa mkutano huo ulikuwa haumhusu.

Awali, Keissy aliwaambia waandishi wa habari kuwa: “Uchaguzi wa mwaka huu ni mgumu kwa vyama vyote kutokana na uelewa na mwamko wa wananchi, hivyo siyo vibaya hata mimi kuhudhuria mkutano huu.

“Hakatazwi mtu kuhudhuria mikutano kama hii maana uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na miaka mingine na ACT-Wazalendo wana siasa nzuri na kitakuwa chama cha pili cha upinzani.”

Katika mkutano huo, Mghwira aliwaambia wananchi waliohudhuria kwamba viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza nchi hawana cha kujitetea kuhusu kusuasua kwa maendeleo nchini.

Alisema katika mikoa aliyotembelea, ameona jinsi gani Watanzania walivyopigika na ugumu wa maisha na hali hiyo inasababishwa na viongozi waliowapa dhamana ya kuwaongoza kutojali maendeleo yao. 
 
“Suluhisho pekee la hali hii ni ACT-Wazalendo. Tumejipanga ipasavyo kuwatumikia na endapo nikifanikiwa kuingia madarakani uchumi wa Taifa hili na thamani ya shilingi haitoshuka ili kuleta maendeleo kwenu,” alisema Mghwira.

Pia, aliwaahidi wakazi wa Katavi kubadilisha mfumo wao wa kilimo na kuwa kilimo cha biashara ili vijana wake wapate ajira na kuachana na kilimo cha kizamani na kuweka mfumo bora wa usambazaji wa pembejeo za kilimo.

Comments