MKUTANO WA UKAWA WAKATISHWA KWA VURUGU
JESHI la polisi mkoani Mtwara jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kurejesha hali ya amani katika mkutano wa Chadema uliofanyika katika viwanja vya Mashujaa mjini hapa.
Mkutano huo ambao vyama vya siasa vya upinzani vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) vilialikwa, ulikuwa na lengo la kuwatambulisha wasanii wa filamu na wa muziki wa kizazi kipya wanaomuunga mkono mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa.
Akizungumzia tukio hilo jana, Katibu wa Chadema mkoani hapa, Willy Mkapa, alisema lengo la tamasha hilo lilikuwa kumnadi mgombea wa urais pamoja na mgombea wa ubunge kupitia Ukawa, na kuwatambulisha wasanii wanaomuunga mkono Lowassa.
Alisema baada ya wasanii hao kutumbuiza na kuwadia muda wa hotuba ndipo vurugu zilipoanza ambapo inadaiwa kulikuwa na kikundi cha wafuasi wa mgombea ubunge wa Mtwara Mjini kupitia NCCR –Mageuzi, Uledi Hassan, kutaka mkutano huo usimnadi mgombea ubunge badala yake umnadi mgombea urais pekee.
Wafuasi hao wanadai kuwa wao kama NCCR wanamgombea wao, Chadema wana mgombea wao na vivyo hivyo CUF wana mgombea wao, hivyo isingekuwa vyema kumnadi mgombea mmoja.
Na baada ya mabishano yaliyochukua dakika kadhaa ndipo jeshi la polisi lilipoingilia kati na kutaka kuwaondoa wafuasi hao mkutanoni hapo.
Hali hiyo ilizua taharuki na polisi walilazimika kurusha mabomu ya machozi na kufyatua risasi hewani na kisha kufanikiwa kumkamata kijana mmoja aliyedaiwa kuongoza wenzake na kuondoka naye hadi Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa.
Katibu huyo wa Chadema alisema kwa mujibu wa viongozi wa juu wa vyama vinavyounda Ukawa, Jimbo la Mtwara Mjini anayetakiwa kuwa mgombea ni Nachuma Maftaha wa CUF na kwamba Chadema wanamuunga mkono, ndiyo maana mgombea wao amejitoa, lakini NCCR- Magenzi bado wanalazimisha mgombea wao awanie ubunge jimboni humo.
Comments
Post a Comment