MKUU WA JESHI LA POLISI ASEMA KUZIDISHA MUDA WA KAMPENI SI KOSA


Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu amesema hakuna sheria inayozuia wagombea urais, ubunge na udiwani kufanya kampeni zaidi ya saa 12 jioni isipokuwa ni kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza jana, IGP Mangu alisema hakuna mahali palipoandikwa, lakini kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na NEC na wadau wake, kinachofuata ni utekelezaji.

IGP Mangu alisema hayo baada ya kuulizwa hatua zinazoweza kuchukuliwa baada ya mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kuzidisha muda wa kampeni mjini Morogoro alikotumia dakika zaidi ya 15 juzi.
 
 Pia, wakati wa uzinduzi wa kampeni zake, Agosti 23 jijini Dar es Salaam, mgombea huyo alizidisha dakika 33. 
 
Jana mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa naye alimaliza mkutano wake wa kampeni Mbezi Dar es Salaam saa 12.15.

Mangu alisema kuzidisha muda wa mikutano yao ya hadhara baada ya saa 12.00 jioni ni kuvunja kanuni zilizowekwa na tume ingawa siyo kosa la jinai.

“Hakuna sheria inayozuia mkutano kufanyika zaidi ya muda huo. Ni kanuni tu ndizo zinasimamia hilo hivyo ni jukumu la Tume kuchukua hatua. Kwa askari wangu inakuwa ni changamoto kumlinda mhusika na kama maadui zake watamshambulia,” alisema.

Alisema jeshi lake linatumia weledi kusimamia haki na wajibu na kamwe haliwezi kuingilia makubaliano ya watu au taasisi yoyote kama ilivyo kati ya NEC na vyama vya siasa.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alirejea wito wake kwa vyama na wafuasi wake kuzingatia makubaliano yanayosimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Tunaendelea kuvikumbusha vyama vya siasa kuzingatia kanuni walizojiwekea na kuwaelimisha wafuasi wao juu ya maadili ya uchaguzi."

Alisema, maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015 Sura ya 2.1(c) inaviagiza vyama vyote vya siasa kufanya mikutano ya kampeni kati ya saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni.

Wabanduaji mabango
IGP Mangu alisema polisi itawafungulia mashtaka ya kuharibu mali wale wote watakaokamatwa kuhusika na kubandua au kuchana picha za matangazo ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.

“Kanuni na maadili ya uchaguzi zinazuia wanachama na wafuasi wa chama kimoja kuharibu matangazo au mabango ya kampeni ya mgombea wa chama kingine. Hivyo yeyote anayefanya hivyo anakiuka maadili waliyoafikiana baina na tume na vyama vya siasa,” alisema Mangu.

“Kama atajitokeza mlalamikaji, basi mlalamikiwa atakuwa na kesi ya kujibu juu ya kuharibu mali. Hizo picha ni mali ya mtu au chama fulani.”

Comments