NAULI YA MABASI YA MWENDO KASI DAR, YAPANDA
Ukali
zaidi wa maisha kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam unakuja kutokana na
viwango vipya vya nauli za magari yaendayo haraka kuwa kati ya Sh. 500
hadi 900 kwa safari moja kwa mtu mzima.
Aidha,
nauli ya mwanafunzi itakuwa kati ya Sh. 250 na 450 kwa safari moja,
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra),
imetangaza jana.
Tangazo
la Sumatra kwa vyombo vya habari jana lilieleza kuwa, mamlaka hiyo
imepokea maombi ya nauli kutoka kwa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka Dar
es Salaam (Udart) ambao utatoa huduma ya usafiri wa umma katika kipindi
cha mpito.
Tangazo
hilo lilieleza kuwa, safari katika njia kuu pekee mathalani Kimara
Mwisho hadi Kivukoni itakuwa Sh. 700 kwa mtu mzima wakati nauli ya
mwanafunzi itakuwa Sh. 350. Hivyo kwenda na kurudi kwa mtu mzima itakuwa
Sh. 1,400 na mwanafunzi itakuwa Sh. 700.
Aidha, nauli ya pembezoni (Mbezi hadi Kimara Mwisho), itakuwa Sh. 500 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi itakuwa Sh. 250.
Pendekezo
lingine la nauli ni kwa abiria watakaopita njia ya pembezoni na kisha
njia kuu kama kutoka Mbezi-Kimara Mwisho hadi Kivukoni, nauli itakuwa
Sh. 800 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi itakuwa Sh. 400.
Safari
nyingine ni kwa abiria wanaotumia njia ya pembezoni, njia kuu halafu
njia ya pembezoni. Mfano wa safari hiyo ni wanaotoka Mbezi-Kimara Mwisho
hadi Morocco; nauli yao itakuwa Sh. 900 na wanafunzi itakuwa Sh. 450.
Meneja
Miundombinu wa Udart, Mohammed Kaganda, amesema wanategemea kuanza
rasmi kazi ya usafirishaji wa abiria kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni
mapema mwezi ujao.
“Mabasi
sasa yapo kwenye maji (kwenye meli baharini), tunategemea yatawasili
mwishoni mwa mwezi huu na tutaanza usafirishaji mwanzoni mwa Oktoba,
mwaka huu” alisema.
Hata
hivyo, alitoa mfano kuwa safari ya njia ya pembezoni, njia kuu na kisha
njia ya pembezoni itaokoa fedha za abiria kwa kuwa badala ya kulipa Sh.
1,700 sasa atalipa Sh. 900 kwa kuwa atatumia magari ya Udart.
Alisema mabasi yanayotegemea kuanza kazi katika kipindi cha awali ni 80 na kwamba yatafanyakazi sambamba na daladala za kawaida.
“Katika
awamu hii, daladala zitaendelea kufanyakazi kama kawaida lakini
hazitatumia njia za mwendo kasi, zitakuwa kwenye barabara hizi za
kawaida zinazotumika sasa,” alisema Kaganda.
Nauli
ya sasa kutoka Mbezi hadi Posta/Kivukoni ni Sh. 600 kwa mtu mzima
wakati kwa mwanafunzi ni Sh. 200 na nauli ya kutoka Mbezi hadi Kimara
Mwisho au Ubungo ni Sh. 400 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi ni Sh.
200.
Mara ya mwisho kwa Sumatra kupandisha usafiri wa daladala ilikuwa Aprili, mwaka 2013.
Hata
hivyo, kabla ya kupitishwa kwa nauli hizo za mabasi yaendayo kasi,
Sumatra imeitisha mkutano wa wananchi kwa ajili ya kupata maoni kuhusu
maombi hayo kwenye mkutano utakayofanyika Jumanne ijayo.
Comments
Post a Comment