ROSTAM AZIZ AMRUSHIA DK . SLAA MAKOMBOLA


Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, amemvaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, akimuita kuwa ni mtu mwongo, mbinafsi na mpotoshaji mkubwa.

Rostam alieleza hayo katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari kuhusiana na tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa dhidi yake jijini Dar es Salaam juzi, alipozungumza na vyombo vya habari kuelezea mambo kadhaa zikiwamo sababu za kujiondoa ndani ya Chadema.

Dk. Slaa alidai kuwa mwaka 2009 baada ya kutaja orodha ya mafisadi 11 nchini katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam,  Rostam alimpigia simu na kumtishia maisha.

Dk. Slaa pia alidai juzi katika mkutano wake na vyombo vya habari uliorushwa na vituo vitatu vya runinga kuwa Rostam anaifadhili Chadema.

Katika taarifa yake jana, Rostam alisema: “Nilimsikiliza Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willibrod Slaa jana (juzi) alipokuwa akizungumza katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

“Kwa mara nyingine kama ilivyo hulka yake miaka yote, Dk. Slaa kathibitisha pasipo na shaka kwamba yeye ni mbinafsi na mpotoshaji mkubwa.”

“Nimesikitishwa na kushtushwa japo sikushangazwa hata kidogo na hatua ya Slaa ambaye sasa anaonekana kukubuhu kwa uzushi kutoa matamshi ya namna hiyo.

"Sijapata hata mara moja kuwa na mawasiliano na Dk Slaa wakati wowote. Madai yake kwamba eti nilimtisha ni ya kupuuzwa na yasiyo na msingi hata kidogo,” alisema Rostam.

Rostam alieleza kuwa ni jambo lisiloingia akilini hata kidogo kwa watu wanaomfahamu Slaa kwamba anaweza kumtishia maisha na yeye akakaa kimya bila  kuchukua hatua ya kwenda polisi na kumshitaki halafu anakaa na jambo hilo kwa miaka yote hadi juzi ndipo alisema hadharani.

“Ili kuthibitisha madai yake hayo, namtaka Dk. Slaa kujitokeza hadharani na kutoa ushahidi wa jambo hilo,” alisema Rostam.

Huu ni uongo mwingine wa dhahiri. Namtaka Dk. Slaa kutoa ushahidi pia katika madai yake haya.
 
“Ni huyu huyu Dk. Slaa ambaye mwaka 2010 alizusha kwamba eti mimi, tukiwa na Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa tulikutana katika hoteli ya La Kairo, Mwanza na kupanga njama za kumuibia kura zake za urais,” alisema na kuongeza:

“Wakati Slaa akitoa madai hayo ya uongo, mimi nilithibitisha kwamba wakati huo nilikuwa Afrika Kusini na Rais Kikwete akiwa Lindi huku Lowassa akiwa Arusha. Ni wazi kwamba tusingeweza kukutana La Kairo kama alivyodai yeye.”

Kwa mujibu wa Rostam, Dk. Slaa kuna wakati alimzushia hadi Rais Kikwete alipodai kwamba alisafiri kwa usiku mmoja kwenda China kumtoa mwanaye aliyekuwa amekamatwa na vyombo vya usalama, kisha kurejea Dar es Salaam usiku huo.

“Ni Slaa huyu huyu ambaye mwaka 2010 wakati wa kampeni alifikia hatua ya kuutangazia umma wa Watanzania kwamba kulikuwa na malori yaliyobeba kura za CCM ambazo zingesaidia ushindi wa wizi yaliyokamatwa Tunduma. Malori hayo yalipokaguliwa yalibainika kuwa na mizigo ya kawaida,” aliongeza katika taarifa hiyo.

Comments