SERIKARI YALIPA MADENI YOTE KWA WAALIMU
SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu madeni ya walimu kwa kusema imeshalipa yote ya mwaka jana na kwa mwaka huu, orodha inaandaliwa. Orodha kwa ajili ya madeni ya mwaka huu,
inasubiriwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kabla ya malipo kufanyika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile alisema jana kwamba, wakati wa kulipa madeni ya mwaka jana, Wizara ya Fedha ilipokea orodha kutoka Tamisemi ikionesha madeni ya Sh bilioni 19.6. Baada ya kufanya uhakiki, walibaini madeni halali ni Sh bilioni 5.7 ambayo walilipa yote.
Hali inayoonesha kuwa kuna watumishi hewa ambao waliingizwa katika orodha hiyo ya madai. “Sababu za madai hayo kukataliwa ni pamoja na kukosa vielelezo, madai yaliyokwishalipwa, madai yasiyo ya mishahara kuwasilishwa kama mishahara, baadhi ya walimu kutotambuliwa na Halmashauri husika na makosa ya ukokotoaji na uandishi,” alisema Dk Likwelile.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam, Likwelile alisema madai ya walimu yako mara mbili ambayo ni mishahara pamoja na madai yasiyo ya mishahara.
Alisema mpaka sasa wizara haijapokea orodha ya madeni ya walimu kwa mwaka huu, hivyo wataanza kuyashughulikia baada ya kuhakikisha walimu wanapata fedha zao kwa wakati. Hata hivyo alisema upo umuhimu wa Tamisemi kuandaa orodha ya madeni na kuyahakiki kutoa orodha ambayo italipwa malipo halali.
Mkaguzi wa Ndani Mkuu, Mohammed Mtonga alisema kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa uhakiki ikiwemo kuongezwa kwa madai hewa, idara yake inapendekeza kuwa halmashauri zilizowasilisha madai yenye shaka, yasiyo halali au watumishi wasio na madai wawajibishwe kwa kuwasilisha taarifa zisizo sahihi.
Mapendekezo mengine ni kuwa halmashauri hizo zihakikishe zinatenga fedha kwa ajili ya kulipa madai halali ya watumishi wake, kuhakikisha kuwepo kwa rejesta ya madai ya watumishi ambayo hayajalipwa na yaliyolipwa
Comments
Post a Comment