TANESCO YAMSHTAKI ASKOFU GWAJIMA POLISI
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeishtaki polisi Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima kutokana na kuharibu miundombinu ya umeme katika maeneo ya shirika hilo Jumamosi iliyopita na kusababisha umeme kukatika kwa baadhi ya mikoa na Jiji la Dar es Salaam.
Kutokana
na kukatika kwa umeme kwa muda huo, shirika limepata hasara ya zaidi ya
Sh milioni 30 ambayo ni mapato kama kungekuwepo umeme mbali na usumbufu
mwingine waliopata kama kuwasha mitambo upya.
Meneja
Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin alisema shirika hilo limefungua
jalada namba 4397/2015 dhidi ya kanisa hilo katika Kituo cha Polisi
Kimara katika Manispaa ya Kinondoni kwa sababu hiyo.
Severin
alisema kuwa Agosti 29, mwaka huu kuanzia saa tisa alasiri hadi saa 12
jioni, umeme ulikatika katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa
iliyoungwanishwa katika gridi ya Taifa.
Alisema
baada ya uchunguzi wa kina waligundua chanzo cha kuzimika umeme siku
hiyo ilikuwa ni hitilafu ya umeme iliyotokea eneo la Ubungo Chai Bora
kwenye kanisa hilo la Askofu Gwajima.
“Watu
wanaosadikiwa kuwa watumishi wa kanisa hilo walikuwa wakishusha kontena
kwa kutumia crane (winchi) chini ya nyaya za umeme wakati wakinyanyua
kontena hilo liligusa laini ya msongo mkubwa wa kilovoti 132 inayopeleka
umeme Zanzibar,” alifafanua Meneja Uhusiano wa Tanesco.
Severin
alieleza kuwa tukio hilo lilisababisha mlipuko mkubwa ulioambatana na
kuzimika kwa kituo kikubwa cha kupoozea umeme na mitambo ya kuzalisha
umeme iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Kukatika
huko kwa umeme kuliathiri shughuli za uchumi na kijamii ikiwemo
mikutano ya kampeni za siasa kwa baadhi ya vyama iliyokuwa unaendeleo
katika Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine,” alisema ofisa huyo.
Siku
hiyo ilikuwa na uzinduzi wa kampeni za urais za Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na baadhi ya watu walihusisha tukio hilo kuwa ni
makusudi na hujuma za kisiasa; jambo linalothibitika si kweli.
Meneja
Uhusiano wa Tanesco alisisitiza kwamba kukatika kwa umeme siku hiyo,
haikuwa makusudi au kwa nia ya kuhujumu vyama vya siasa, kama ambavyo
imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu kwenye vyombo vya habari na hasa
mitandao ya kijamii.
Kwa
upande wake, Askofu Gwajima alipoulizwa kwa simu kuhusu tuhuma hizo,
alisema hana taarifa na ndiyo kwanza anazisikia kutoka kwa mwandishi,
licha ya kuwepo taarifa za Tanesco kuonana na uongozi wa kanisa hilo na
kuzungumzia jambo hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura alisema hajapata taarifa hizo na atazifuatilia.
Comments
Post a Comment