TUME YA UCHAGUZI NEC YAMUONYA LOWASSA


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kitendo kilichofanywa na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa cha kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye, kamwe hakikubaliki.

Imesisitiza kuwa kitendo hicho, kinawagawa Watanzania na kuwapa mwelekeo wa kuchagua viongozi kwa misingi ya udini na ni ukiukwaji wa Kifungu cha 2.2 (i) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2015, kinachosema “Vyama vya Siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya Udini, Ukabila, jinsia au rangi.” 
 
Onyo hilo la NEC lilitolewa jana na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Damian Lubuva ikiwa ni muda mfupi tangu CCM ilipoitisha mkutano wa waandishi wa habari, kuzungumzia suala hilo, huku ikiitaka NEC kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wa kanuni wa mgombea huyo wa Chadema.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, NEC imewakumbusha wagombea na vyama kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ambayo walikubali kuyafuata kwa kutia saini Julai 27, mwaka huu. 
 
Ilisema inasikitisha kuona kiongozi au mgombea anatumia madhabahu kufanya kampeni na mbaya zaidi kuomba kura kwa misingi ya kidini.

“Kitendo kilichofanywa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye hakikubaliki,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. 
 
Alisema Tume inavikumbusha Vyama vya Siasa kuzingatia Kifungu cha 2.1 (k) cha Maadili kinachoelekeza vyama au wagombea kutotumia majengo ya Ibada kufanya kampeni, na pia vyama au wagombea kutowatumia viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao.

“Tunatumia fursa hii tena kuwaasa viongozi wa madhehebu yote ya dini kutoruhusu vyama au wagombea au wanachama wa vyama vya siasa kutumia nyumba za Ibada kufanya kampeni za uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.” 
 
Jaji Lubuva alisema mbali ya hilo, Lowassa na viongozi wengine wa Chadema wamekuwa na kauli za kuwaogofya wananchi kuwa ‘kura zitaibiwa’ na kwamba Tume itasababisha machafuko, bila kutoa ufafanuzi jambo ambalo ni hatari.

“Kauli hizo zinashangaza na kustaajabisha na ni kauli za hatari sana kipindi kama hiki, kwa sababu maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea, ambayo wagombea wote na vyama vya siasa walipewa, yana maelekezo kuhusu utaratibu mzima wa kupiga na kuhesabu kura katika ngazi ya kituo, kujumlisha kura katika ngazi ya kata, jimbo na taifa."

Akifafanua utaratibu ulivyo, Jaji Lubuva alisema taratibu zote hizo hushuhudiwa na Mawakala wa Vyama vya Siasa na Wagombea, ambapo kura zikihesabiwa ngazi ya Kituo, mawakala hupewa nakala ya matokeo katika fomu Na. 21A Kura za Urais, 21B Kura za Mbunge na 21C Kura za Udiwani. 
 
Alisema katika ngazi ya Jimbo, hesabu ya kura za kila kituo zilizopo pia katika nakala la Fomu 21A za Urais na 21B za Mbunge hujumlishwa na matokeo kujazwa katika fomu 24A kwa Rais na 24B Mbunge na Nakala ya matokeo wanapewa mawakala wa vyama na wagombea waliopo katika kituo cha kujumlishia kura ngazi ya jimbo.

Kwa upande wa ngazi ya Taifa, alisema Tume hujumlisha matokeo ya kura za Rais mbele ya wagombea na mawakala wa vyama na kutangaza matokeo. 
 
Aliongeza kuwa katika hatua hizo, Chadema wanapaswa kueleza wizi unafanyika wapi? “Jana Freeman Mbowe (Mwenyekiti Chadema Taifa) naye amesema kuwa Tume inaegemea Chama Tawala, hivyo itasababisha uvunjifu wa amani. Hili nalo ni tamshi lisilo la ukweli kabisa.

“Wakati wote Tume haiegemei wala kupendelea chama chochote katika kazi zake. Mbowe anajua hivyo, chaguzi zote Tume imefanya kwa kutegemea kura halali zote na ndiyo maana hata wabunge wa vyama vingine walitangazwa. "
 
Alisema viongozi wote hasa wakuu wanaogombea Urais, yafaa wawe waangalifu katika matamshi yao, vinginevyo matamshi ya aina hiyo yanaweza kujenga msingi wa vurugu baadaye.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakumbusha vyama vya siasa vijielekeze kwenye kutumia muda mwingi kuelezea Sera za vyama vyao ili ziweze kupimwa na wapiga kura, badala ya kuchochea uhasama kati yao na Serikali na Tume ya Uchaguzi. 
 
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, NEC haitasita kukifikisha chama au mgombea mbele ya Kamati ya Maadili ili aweze kuthibitisha kauli yake ;na anaposhindwa Kamati itaweza kutoa adhabu kali kwa chama au mgombea husika, ikiwa ni pamoja na kukatazwa kampeni kwa mhusika

Comments

Popular Posts