WAGANGA WA ASILI WAPEWA SOMO KUHUSU TAALUMA YAO

 


BARAZA la tiba asili na tiba mbadala limetakiwa kuhakikisha waganga wote wanaotoa huduma kwa wateja wanasajiliwa ili kuepuka udanganyifu.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Rashid Seif wakati alipozungumza viongozi wa Baraza hilo katika maadhimisho ya Siku ya Tiba Asilia na Mbadala kwa bara la Afrika iliyofanyika hapo katika Wizara ya Afya Mnazi Mmoja mjini hapa.
Alisema wakati umefika kwa Baraza la Tiba Asili kusajili watu wenye sifa ambao watafanya kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na sio kuweka mbele maslahi ikiwemo kipaumbele fedha. Alisema hivi sasa wamejitokeza baadhi ya watu wanaojifanya waganga wa tiba asili wakiwadanganya wananchi kwa kujidai kwamba wanao uwezo wa kutibu maradhi mbalimbali.
Seif alisema watu wa aina hiyo kamwe wasiruhusiwe kuingizwa na kusajiliwa katika Baraza la Tiba Asili kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kuipaka matope taasisi hiyo.
Mapema Mfamasia Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Habib Ali alisema utafiti wa dawa asili umepata mafanikio makubwa ambapo hivi sasa wananchi wengi wamekuwa watumiaji wakubwa wengine wakipata nafuu kutokana na maradhi yanayowakabili.
Hata hivyo Ofisi ya Mfamasia Mkuu imekemea vikali baadhi ya waganga wa tiba asilia kutoa matangazo kwamba wanatibu ugonjwa wa Ukimwi.

Comments