WANDISHI WA HABARI WAPEWA SOMO KUHUSU UCHAGUZI
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi zao na kuzijua Sheria za Tume ya Uchaguzi (ZEC) ikiwemo kufahamu kwamba chombo chenye uwezo wa kutangaza matokeo ya urais wa Zanzibar ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Kassim Ali wakati alipozungumza na waandishi wa habari akiwakumbusha utekelezaji wa majukumu yao katika kampeni za uchaguzi mkuu hadi kutangazwa kwa matokeo ya urais.
Alisema ni marufuku kwa chombo cha habari kutangaza matokeo ya uchaguzi yaliyobandikwa katika vituo vya kupigia kura,kwani kazi hiyo ni ya Tume. Alifahamisha kwamba kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria kwani kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“ Waandishi wa habari mnatakiwa kuzifahamu sheria za uchaguzi ambapo ni marufuku kwa chombo cha habari kutoa matangazo yaliyobandikwa katika vituo vya kupigia kura kwa sababu hiyo ni kazi ya Tume,” alisema.
Alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imejizatiti kuhakikisha kwamba inatekeleza majukumu yake ikiwemo kusimamia uchaguzi mkuu kuwa huru kwa mujibu wa sheria.
Aidha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha alikumbusha wajibu wa waandishi wa habari kuhakikisha jamii inapata habari zilizosahihi na ukweli bila ya kuleta migogoro kwa jamii.
“Sisi tume ya uchaguzi hatumiliki vyombo vya habari kwa ajili ya kufikisha taarifa hizo kwa wananchi...... hiyo ni kazi yenu kwa hivyo mnatakiwa kutoa taarifa hizo kwa usahihi wa hali ya juu,” alisema.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni Piga kura yako kwa amani na utulivu kwa maendeleo ya nchi na kudumisha demokrasia.
Comments
Post a Comment