CHADEMA YAWATAKA WANANCHI KUJUMLISHA MATOKEO NA KUYASAMBAZA NA SIKUSUBILI NEC


Chadema imewataka wananchi kujumlisha matokeo yote yatakayotolewa kwenye vituo vya uchaguzi na kuyasambaza badala ya kusubiri kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza jana kwenye mkutano wa kampeni Jimbo la Kikwajuni mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Bara, John Mnyika aliwataka wananchi hao kutoondoka kwenye vituo vya kupigia kura, bali wasubiri hatua 200 kutoka vituo hivyo kupiga kura ili kulinda kura zao.

“Mjitokeze kwa wingi kupiga kura na baada ya kupiga kura mrudi nyuma hatua 200 kulinda ushindi wenu. Nina uzoefu na hili kwa sababu lilitokea jimboni kwangu mwaka 2010,” alisema na kuwataka Wazanzibari wasikubali kuibiwa kura zao.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee aliyeambatana na Mnyika katika kampeni za kumuunga mkono Salum Mwalimu anayegombea ubunge wa Jimbo hilo la Kikwajuni, aliwaeleza wananchi kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wa muhimu kwa sababu wakikosea kuchagua itawagharimu miaka mingine mitano.

Alisisitiza kuwa kama wanataka kuwa na mamlaka kamili, basi wamchague Edward Lowassa na Maalim Seif Sharif Hamad ili washirikiane kuanza upya mchakato wa Katiba. Aliwataka pia wamchague Mwalimu kuwa mbunge wao ili akaongeze nguvu katika mapambano bungeni na kuitetea Zanzibar.

“Moja ya ajenda kuu za Ukawa ni kuwa na Muungano wa serikali tatu, Zanzibar ikiwa ni mamlaka kamili. Wachagueni viongozi hawa ili mpate watetezi wenu watakaowaletea maendeleo,” alisema Mdee.

Awali, akiomba kura kwa wananchi, Mwalimu aliahidi kwamba akichaguliwa, atahakikisha anasimamia kikamilifu masilahi ya jimbo lake na Zanzibar kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa anatambua matatizo ya jimbo hilo na kuahidi kujitoa katika kuyatatua kwa sababu naye pia ni sehemu ya jamii hiyo. Aliwataka wananchi kumpigia kura kwa wingi Oktoba 25, ili atimize ahadi zake.

Comments