DK. MAGUFULI AMWAGIA SIFA DK. SLAA


Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli jana aliwahutubia mamia ya wakazi wa Karatu na kummwagia sifa aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa ni kiongozi mwadilifu.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mbowe mjini Karatu, Dk Magufuli alisema Dk Slaa ni kiongozi wa upinzani ambaye alikuwa mwadilifu akitetea masilahi ya umma.

Alisema kama angekuwa anagombea katika jimbo hilo, angemwombea kura kwani ni mtu safi bila kujali chama chake.

Huku akishangiliwa na mamia ya watu wa Karatu, Dk Magufuli aliwataka kumuunga mkono Dk Slaa kwa uamuzi ambao amechukua.

Dk Slaa, alitangaza hivi karibuni kuachana na siasa za vyama na kujitoa Chadema baada ya kutoridhishwa na kujiunga kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika chama hicho

Comments