MATOKEO YA UCHAGUZI,.MAWAZIRI WA TANO WA SERIKALI WAPIGWA MWELEKA
Mawaziri watano wa Serikali inayomaliza muda wake wameanguka kwenye uchaguzi majimboni mwao, sambamba na wagombea wengine maarufu wa Bunge lililopita baada ya matokeo ya kura zilizopigwa Jumapili kuanza kutangazwa jana.
Mawaziri
hao wanaungana na wabunge wengine maarufu wa Bunge la Kumi walioshindwa
kutetea majimbo yao, wakiwamo wa kambi ya upinzani ambao wameangushwa
na wagombea wa CCM.
Pia
wamo mawaziri wa zamani wawili, Cyril Chami na Omary Nundu walioanguka
kwenye uchaguzi, kwa mujibu wa matokeo ambayo yanaendelea kutangazwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema jana kuwa itakamilisha kazi ya kutangaza matokeo yote keshokutwa.
Mawaziri walioanguka kwenye uchaguzi huo ni Steven Wasira, Christopher Chiza, Aggrey Mwanri, Dk Steven Kebwe na Anne Kilango.
Katika
matokeo yaliyotangazwa jana, Wasira, kada maarufu na mwanasiasa mkongwe
aliyekuwa akitetea Jimbo la Bunda, alijikuta akiangushwa na mwanasiasa
kijana, Ester Bulaya, ambaye alihamia Chadema baada ya Bunge la Kumi
kumaliza muda wake.
Wasira,
ambaye alikuwa Waziri wa Kilimo na Chakula, alianza mchakato wa
uchaguzi mwaka huu kwa kuomba ridhaa ya CCM agombea urais, lakini
hakupitishwa. Bulaya, ambaye alikuwa mbunge wa viti maalum (CCM),
alipata kura 28, 508 na kumuacha mbali waziri huyo mkongwe aliyepata
kura 19, 126.
Mwingine
aliyeanguka ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwezeshaji na
Uwekezaji, Christopher Chiza ambaye ameangushwa na Bilago Samson wa
Chadema katika Jimbo la Buyungu. Waziri huyo alizidiwa kwa kura 104
baada ya Samson kupata kura 23,041 dhidi ya 22,934 za Chiza.
Lakini
hali haikuwa hivyo kwa Naibu Waziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri kwenye
Jimbo la Siha. Waziri huyo alizidiwa kwa zaidi ya kura 4,100 na mpinzani
wake kutoka Chadema, Dk Godwin Mollel aliyepata kura 22,746.
Katika
Jimbo la Serengeti, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Stephen
Kebwe pia alijikuta akipoteza nafasi ya kurudi bungeni kwa kura
alipoangushwa na Marwa Ryoba wa Chadema. Dk Kebwe alipata kura 39,232,
akiwa amezidiwa na mpinzani wake kwa zaidi ya kura 820.
Anne
Kilango, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu mwaka 2013 baada
ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyosababishwa na kashfa ya
Operesheni Tokomeza, ameangushwa na mgombea wa Chadema, Naghenjwa
Kaboyoko wa Chadema kwa tofauti ya kura 3,297.
Kilango
alipata kura 15,539 wakati mgombea huyo wa Chadema alipata kura 18,836.
Pia wabunge maarufu kama Vincent Nyerere (Musoma Mjini), James Lembeli
(Kahama Mjini) na Kyisieri Chambiri (Babati Mjini) wameangushwa.
Nyerere,
aliyekuwa akitetea kiti cha Musoma Mjini kwa tiketi ya Chadema,
aliachwa mbali na mgombea wa CCM, Vedastus Mathayo aliyepata kura 32,
836 dhidi ya 25,549.43 za Nyerere.
Lembeli,
ambaye alihamia Chadema muda mfupi baada ya Bunge la Kumi kumaliza muda
wake, aliachwa mbali na mfanyabiashara maarufu, Jumanne Kishimba
aliyepata kura 47,553 dhidi ya kura 30,122 za Lembeli.
Comments
Post a Comment