RAIS KIKWETE ATEUA MAKATIBU WA KUU 4 NA MANAIBU KATIBU WA KUU 5 WAPYA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa leo, Ijumaa, Oktoba 23, 2015, amewateua Makatibu Wakuu wanne wapya wa wizara mbali mbali.

Aidha, Rais Kikwete amewateua Naibu Makatibu Wakuu wapya watano, amewateua Makatibu Tawala wa Mikoa wawili na pia amewahamisha Naibu Makatibu Wakuu wawili.

Kwa mujibu wa uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua Ndugu Hab Mkwizu kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Profesa Elisante Ole Gabriel kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Dkt. Yamungu Kayandabila kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Mhandisi Omari Chambo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.

Aidha, kwa mujibu uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua Mhandisi Paul M. Masanja kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini; Dkt. Maria Mashingo kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ndugu Zidikheri M. Mundeme kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Wengine walioteuliwa kuwa Naibu Makatibu Wakuu ni Ndugu Tixon T. Nzunda ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Ndugu Emmanuel Kalobelo ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

Walioteuliwa kuwa Makatibu Tawala wa Mikoa ni Ndugu Eliakim Maswi ambaye anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara na Mhandisi Madeni Kipande ambaye anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.

Katibu Mkuu ambaye anahamishwa ni Bibi Sihaba Nkinga ambaye anakwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Wanawake, Jinsia na Watoto kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Naibu Makatibu Wakuu wanaohamishwa ni Ndugu John T. Mngodo ambaye anahamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutoka Wizara ya Uchukuzi na Ndugu Mwamini Juma Malemi ambaye anakwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Wateuliwa hao wote wataapishwa asubuhi ya kesho, Jumamosi, Oktoba 24, 2015, Ikulu mjini Dar es Salaam

Comments