RAIS WA MEXICO AMESEMA KIMBUNGA PATRICIA BADO NI HATARI

 Mexico


Rais wa Mexico ameonya kuwa Kimbunga Patricia bado kinaweza kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi huku mvua kubwa iliyotokana na kimbunga hicho ikiendelea kunyesha maeneo ya taifa hilo.

Rais Enrique Pena Nieto alisema Patricia, ambacho ndicho kimbuka kikali zaidi kuwahi kuripotiwa maeneo ya Amerika, kufikia sasa kimesababisha madhara madogo ikilinganishwa na ilivyotarajiwa.
Kituo cha kitaifa cha kufuatilia vimbunga cha Marekani (NHC) kilisema kimbunga hicho kilfikia ngazi ya tano, ambayo ndiyo ya juu zaidi.
Baadaye, kimbunga hicho kilishushwa ngazi na kuwekwa kwenye ngazi ya pili.
Kimbunga hicho kilifika maeneo ya magharibi mwa Mexico na kusababisha upepo mkubwa na mvua, lakini uharibifu mkubwa haukutokea.
Kituo cha NHC kilisema upepo huo ulikuwa umepunguza kasi hadi kilomita 155 kwa saa, kilipokaribia bara.
Kimbunga hicho kwa sasa kinaelekea maeneo ya kaskazini mashariki.
Majimbo ya Nayarit, Jalisco, Colima, Michoacan, na Guerrero ndiyo yaliyo hatarini, kituo hicho kimesema.
"Ripoti za kwanza za uharibifu zinaonyesha uharibifu uliotokea si mbaya kama ilivyotarajiwa kwa kimbunga cha ngazi hiyo,” Bw Pena Nieto amesema akihutubia taifa kupitia runinga.
Image caption Kimbunga hicho kimeandamana na upepo na mvua kubwa
Polisi nchini Mexico walisema visa pekee vilivyoripotiwa ni vya maporomoko madogo ya ardhi na kuanguka kwa miti.
Lakini serikali imeonya kuwa majivu kutoka kwa mlima wa Colima, ambao unatoa moshi, huenda yakachanganyikana na mvua kubwa na kusababisha maporomoko makubwa ya ardhi.
Watu 400,000 hukaa maeneo yaliyo hatarini, kwa mujibu wa Hazina ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga ya Mexico.

Comments