CCM WASHIKANA UCHAWI BAADA YA KUPOTEZA JIMBO LA BUNDA


BAADHI ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bunda wamemtuhumu mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa, Chacha Gimanwa, kwamba alichangia jimbo la Bunda Mjini kuchukuliwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Vijana hao walitoa tuhuma hizo, juzi wakati wakitembea matembezi ya amani ya kushangilia ushindi wa mgombea urais wa CCM, Dk Jonh Magufuli katika mitaa mbalimbali ya mji wa Bunda. 
 
Katika uchaguzi mkuu uliopita CCM ilipoteza jimbo hilo, baada ya Stephen Wasira aliyekuwa akitetea kiti hicho kushindwa na mgombea wa Chadema, Ester Bulaya.

Hata hivyo Wasira ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza alidai kuwa katika uchaguzi huo kulikuwa na hujuma.

Wanachama hao wa CCM wakiwa wamebeba mabango baadhi yao walisikika wakimtaja moja kwa moja Gimanwa kwamba ndiye alisababisha CCM kushindwa katika jimbo hilo na kuomba uongozi wa juu wa chama hicho umchukulie hatua.

Hata hivyo, Gimanwa akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu jana alisema kuwa tuhuma hizo hazina msingi wowote na kwamba kamwe hawezi kukihujumu chama chake.
 
“Hicho ni kikundi cha watu wachache tu wanaotaka kuniharibia jina.Mimi kura yangu ni moja na wapiga kura ni wengi, sasa iweje mimi nisababishe mgombea wa jimbo la Bunda mjini ashindwe?” Alihoji. 

 Alisema yeye kama mwenyekiti wa CCM alikuwa akifanya kampeni pia katika jimbo la Bunda vijijini, na siku tatu kabla ya uchaguzi mkuu alirudi tena Bunda mjini na kuendelea na kampeni.

Comments