KAFULILA ADAI KUPORWA UBUNGE ..,,,,ASEMA ANAENDA MAHAKAMANI ILI ATANGAZWE KUWAMSHINDI
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila, ambaye ametangazwa kushindwa katika jimbo hilo uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, ameibuka na kusema anakusudia kwenda mahakamani ili atangazwe kuwa mshindi wa jimbo hilo.
Amedai
kwa mujibu wa kura alizokusanya kupitia mawakala wake katika vituo 182,
alishinda kwa kura 34,149 dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi
(CCM), Husna Mwilima, aliyepata kura 32,982, lakini tume ikamtangaza
kuwa mshindi.
Kafulila
alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi
wa habari kuhusiana na uchaguzi huo, akidai ameporwa ushindi wake na
nguvu ya dola imetumika kuhakikisha anakosa ushindi huo.
“Ninachofahamu
mimi ni Mbunge wa Kigoma Kusini, ila nilihujumiwa na watumishi wa tume
kwa kubadili matokeo yangu na kumtangaza mgombea wa CCM kuwa ni mshindi,
hivyo nitaenda Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kudai haki yangu na
kutangazwa mshindi,” alisema Kafulila.
Alisema
atakachokifuata mahakamani siyo kurudiwa kwa uchaguzi bali kuiomba
mahakama kumtangaza mshindi kwani ana vielelezo vyote.
“Wiki
ijayo nitakuwa nimekamilisha mipango ya kwenda mahakamani, nina fomu
zote 382 kutoka katika kila kata, vituo 182 vilivyotumika kupiga kura
zinazoonyesha idadi ya kura zangu. Nina imani mahakama haitatumia
mlolongo mrefu kutoa hukumu kwa sababu nina vielelezo vya kutosha,” alisema Kafulila.
Aliwataka
wananchi wa jimbo hilo kutokata tamaa na taarifa za kukosa ubunge wake
na kuwataka kuwa wavumilivu wakati wakisubiri maamuzi ya mahakama.
Kafulila
alipoulizwa sababu anayodhani kumkosesha jimbo hilo au kuibiwa ushindi
kama alivyodai, alisema kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Bunge
lililopita ya kuibua masuala ya ufisadi ikiwamo sakata la Tegeta Escrow.
Alidai
kudhibitisha kuwa njama zilitumika, aliwekewa ulinzi mkali wa dola
wakati wa upigaji kura na kipindi cha kusubiri matokeo.
“Nguvu
ya dola ilitumika sana ili kuhakikisha Kafulila ninashindwa, polisi
walikuwa ni wengi sana pia matokeo yalichelewa kutangazwa isivyo
kawaida,” alisema.
Kafulila
alisema alishangazwa na kitendo cha mawakala wa tume kuahirisha kazi ya
ujumuishaji wa kura mara kwa mara licha ya sheria ya uchaguzi
kutoruhusu.
“Kazi
ya ujumuishaji ilikuwa ikiahirishwa mara mbili na wakati mwingine
kuchukua zaidi ya saa 7 na saa 10 hali ambayo siyo ya kawaida,” alidai Kafulila.
Akizungumzia hatma yake juu ya kupiga vita ufisadi, Kafulila alisema ataendelea na harakati hizo.
Alisema
kwa sasa anaandaa vitabu vinavyozungumzia ufisadi kikiwamo kinachoitwa
‘Escrow Unfinished Business’, ambacho kinaelezea vizuri masuala hayo
ambayo amekuwa akiyapiga vita.
Uchaguzi
mkuu ulifanyika Oktoba 25, mwaka huu, katika Jimbo la Kigoma Kusini,
Mwilima wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata kura 34,453, dhidi ya
Kafulila aliyepata kura 33,382.
Comments
Post a Comment