VIONGOZI WA TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR WAANZA KUHOJIWA NA POLISI KUHUSU VURUGU YA UCHAGUZI
Vigogo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), wameanza kuhojiwa na Jeshi la Polisi Zanzibar baada ya kuvurugika kwa Uchaguzi Mkuu na kusababisha Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka huu.
Viongozi waliohojiwa na Polisi ni Makamishna na Watendaji wa tume hiyo akiwamo Makamu Mwenyekiti, Jaji Abdulhakim Issa Ameir.
Naibu
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Salum
Msangi, alithibitisha mjini hapa Mjini jana kuwa Makamishina wa Zec na
Watendaji, wameanza kuhojiwa na maofisa wa upelelezi kutoka Makao Makuu
ya Jeshi la Polisi Zanzibar Ziwani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alisema
hadi sasa uchunguzi umefikia hatua kubwa na baada ya kukamilika,
majalada ya uchunguzi yatapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar
(DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim, kabla ya wahusika kufikishwa mahakamani.
“Tunawahoji
Makamishna na Watendaji wa Tume, Makamu Mwenyekiti yeye tayari
tumemhoji, bado Mwenyekiti na maofisa wengine,” alifafanua DDCI Msangi.
Alisema
Polisi waliingia kazini baada ya kuripotiwa kuwa uchaguzi umevurugwa na
kazi inayofanyika ni kukusanya ushahidi na vielelezo kabla ya wahusika
kufunguliwa mashitaka kwa kuhujumu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema
uchunguzi huo umegawanyika sehemu tatu na kuwahusisha Tume, waathirika
na wananchi kutoka sehemu mbalimbali katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Aidha,
alisema kuna mambo mazito yameanza kuonekana tangu kuanza kufanyika kwa
uchunguzi, lakini alisema ni mapema kueleza uchunguzi huo utachukukua
muda gani kukamilika.
"Wahusika
watafikishwa mahakamni baada ya majalada ya uchunguzi kupelekwa kwa
Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar kabla ya kufikishwa mahakamani,"
alisema Msangi.
Hata
hivyo, Naibu Mkurugenzi huyo alisema hali ya Zanzibar ni shwari na
wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida tangu Zec ilipofuta
matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.
Akitangaza kufuta uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Zec, Jecha alisema kuna sababu tisa zimemfanya kuchukua hatua hiyo.
Alizitaja
kuwa ni pamoja na vituo vya wapigakura na idadi ya kura katika
visanduku zilikuwa nyingi kuliko idadi ya watu waliosajiliwa katika
daftari la wapigakura katika vituo vya uchaguzi.
Aidha,
alisema kuna visanduku vya kura viliporwa na kuhesabiwa nje ya vituo
kinyume na sheria pamoja na mawakala wa vyama kupigwa na kufukuzwa
katika vituo vyao vya kazi siku ya uchaguzi.
Tayari
Zec imetangaza rasmi katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu
kufutwa kwa uchaguzi huo na kuwataka wananchi kusubiri kutangazwa tarehe
ya kurudiwa.
Comments
Post a Comment